Jumatatu 27 Aprili 2026 - 00:00
Tunaunga mkono mazungumzo ya ndani nchini Lebanon

Hawza/ Naibu Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, katika makao ya baraza hilo huko Al-Hazmiyya, alimkaribisha “Jeanine Hennis-Plasschaert”, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali al-Khatib, Naibu Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, katika makao ya baraza hilo huko Al-Hazmiyya, alimkaribisha “Jeanine Hennis-Plasschaert”, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon. Katika mkutano huo, hali inayozunguka Lebanon katika kivuli cha mashambulizi ya Israel ilijadiliwa, na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa aliwasilisha masuala kadhaa, miongoni mwayo ni “uwezekano wa kuitisha mazungumzo ya ndani nchini Lebanon chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, hasa kati ya viongozi wa kidini, pamoja na mahusiano kati ya Lebanon na Syria.”

Sheikh al-Khatib katika mkutano huo alisisitiza kwamba; kuna hatua zinazochukuliwa za kuandaa kikao kitakachowahusisha viongozi wa kidini ili kupunguza mvutano wa ndani na kuzuia fitina yoyote ambayo Israel inataka kuichochea.

Alisema: Sisi tunaunga mkono mazungumzo, na tunatarajia Rais Joseph Aoun aitishe mazungumzo kama hayo, na mkakati wa kitaifa wa ulinzi uwe kiini cha mazungumzo hayo.

Naibu Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia alisisitiza: Ni muhimu kwetu kwamba; Umoja wa Mataifa uwe na mchango hai na uchukue nafasi muhimu katika masuala yetu, lakini kwa masikitiko hata Umoja wa Mataifa haujaepukana na mashambulizi ya Israel.

Akiwa na mshangao alisema: Inawezekanaje Israel iwe na kiti katika Umoja wa Mataifa, ilhali waziri mkuu wake anasimama na kuonesha ramani ya “Israel Kubwa” na kutangaza malengo yake ya kiuchokozi? Hii si dola, bali ni kikundi kilichojengwa juu ya uhalifu na jinai, na maadamu wanaendelea kwa mtazamo huu, hakutakuwa na amani katika eneo hili.

Sheikh al-Khatib aliongeza: Israel imemuua mwandishi wa habari “Amal Khalil”, na yeye si mhanga wa kwanza miongoni mwa waandishi wa habari; kabla yake pia walilengwa mashahidi kama Ali Shu‘ayb, Fatima na Muhammad Fattouni. Hizi ni jinai za wazi za kivita ambazo Umoja wa Mataifa unapaswa kuzilaani.

Alisisitiza pia: Hatutaruhusu kuvutwa katika fitina ya ndani ambayo Israel inaitaka ili kupitia humo ifikie malengo ambayo imeshindwa kuyapata katika medani ya kijeshi na kisiasa. Wale Walebanoni walipitia miaka 15 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe bila kufikia matokeo. Nchini Lebanon kuna watu wenye hekima wanaopinga mzozo wa ndani, japokuwa kuna sauti zisizo na mpangilio, lakini sauti ya wenye hekima ni yenye nguvu zaidi.

Naibu Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon pia alisisitiza: Tunataka mahusiano bora zaidi na dola ya Lebanon, hasa na Rais, na tunakataa aina yoyote ya matusi au vitisho dhidi yake; kwa sababu tunaheshimu nafasi ya urais. Ni kwa manufaa yetu kuwa dola ya Lebanon iwe imara na yenye uwezo wa kulinda mamlaka yake na kuwatetea wananchi wake, ili kupunguza mengi ya kujitolea na mateso.

Mwisho, Sheikh al-Khatib alibainisha: Pia tunataka mahusiano bora ya kindugu na Syria na ndugu zetu Wasyria. Kati yetu na Wasyria kuna mahusiano ya kindugu, na matatizo ya zamani yalitokana na migogoro ya ndani ya Syria. Tunataka mahusiano ya nchi hizi mbili yapangwe katika mfumo wa kiserikali, na hivi karibuni baadhi ya masuala yameshughulikiwa katika mfumo huo.

Tunaunga mkono mazungumzo ya ndani nchini Lebanon

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha