Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani na Shirika la Habari la Palestina Wafa, walowezi wa Kiyahudi wa Israel tarehe 23 Februari 2026 waliushambulia Msikiti wa Abu Bakr Al-Siddiq uliopo katika kijiji cha Tal, kati ya Sara na Tal karibu na Nablus, huko Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Waumini waliokwenda msikitini kwa ajili ya kuswali swala ya mwanzo wa wakati waliona moshi mweusi, sehemu zilizoteketea kwa moto, vioo vilivyovunjika pamoja na michoro ya grafiti yenye maudhui ya kibaguzi iliyochorwa juu ya kuta za msikiti.
Wakazi wa eneo hilo walilaani shambulio hilo na kusema kuwa; lengo lake halikuwa tu jengo la msikiti, bali pia dini na itikadi za Waislamu, hasa kwa kuzingatia kwamba shambulio hilo limetokea katika mwezi wa Ramadhani ambao ni mwezi mtukufu kwetu na ni wakati wa kufunga na kufanya ibada.
Wizara ya Masuala ya Kidini ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilibainisha kuwa; mashambulizi kama hayo dhidi ya misikiti katika Ukingo wa Magharibi yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni, na kwamba katika mwaka uliopita pekee, matukio kadhaa yaliripotiwa.
Shambulio hilo limeongeza mvutano mpana zaidi ndani ya Ukingo wa Magharibi na limezua wasiwasi miongoni mwa waangalizi wa kikanda na kimataifa kuhusu ulinzi wa maeneo ya ibada katikati ya migogoro inayoendelea.
Chanzo: Al Jazeera
Maoni yako