Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Abbas Ka‘abi, katika mwendelezo wa silsila ya darsa za tafsiri ya Qur’ani Tukufu zilizofanyika katika Kituo cha Kielimu na Kitamaduni cha Imam Hussein (a.s.) mjini Qom, alitafsiri aya za mwanzo za Suratul-Hashr na kwa kuchambua kisa cha kihistoria cha Mayahudi wa Bani Nadhir, akakielezea kuwa ni funzo kwa Umma wa Kiislamu katika kipindi chote cha historia.
Naibu Mwenyekiti wa Jumuia ya Walimu wa Hawza ya Qom, mwanzoni mwa hotuba yake, akirejelea historia ya vita vya Bani Nadhir, alisema: Bani Nadhir walikuwa miongoni mwa makabila ya Kiyahudi yaliyoishi pembezoni mwa Madina, waliokuwa wamefunga mkataba na Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na wakatia saini Katiba ya Madina. Wao kwa kutumia kifurushi cha upenyezaji wa kiuchumi, kijamii na nguvu za kisiasa, pamoja na mahusiano waliyokuwa nayo na wanafiki wa Madina kwa upande mmoja na washirikina wa Quraysh kwa upande mwingine, walinuia kuuangusha utawala mchanga wa Kiislamu.
Aliongeza kuwa: Kiongozi wa njama hiyo alikuwa Ka‘b bin Ashraf, ambaye alielekea Makka akiwa na wapanda farasi arobaini na akashirikiana na washirikina wa Quraysh ili kuudhuru upande wa Uislamu. Baada ya kushindwa kwa dhahiri kwa Waislamu katika vita vya Uhud, walidhani Uislamu uko katika kilele cha udhaifu na wakati wa shambulio la mwisho umefika.
Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wateule wa Uongozi alibainisha: Njama hiyo ilishindwa kwa mpango wa busara wa Mtume (s.a.w.w.) na uongozi wa Amirul-Muuminin Ali (a.s.). Watu kumi miongoni mwa viongozi wa Bani Nadhir waliangamia, na Ka‘b bin Ashraf pia aliuawa kabla ya mapambano makuu katika operesheni maalumu.
Kuhusisha ushindi na irada ya Mwenyezi Mungu; ujumbe mkuu wa aya
Ayatullah Ka‘abi akirejelea aya tukufu: “Hamkudhani kwamba watatoka, na wao walidhani ngome zao zitawalinda na (adhabu ya) Mwenyezi Mungu”, alifanya uchambuzi wa kifasihi na kitafsiri wa aya hiyo na kusema: Mwenyezi Mungu katika aya hii kwa tamko la mkazo anaonesha upekee, na anasema ushindi huu ulikuwa kazi ya Mungu peke yake. Enyi Waislamu, kamwe hamkudhani katika mawazo yenu kuwa mtaweza kuwaondoa kwa nguvu namna hii.
Aliendelea: Bani Nadhir walikuwa na ngome tano imara sana ambazo kwa mtazamo wa kimaada zilionekana haziwezi kupenyeka. Walidhani ngome hizo zitawazuia kushindwa, lakini Mwenyezi Mungu anasema hata mkiwa katika minara imara, mauti na maangamizi yatakufikieni.
Mwakilishi huyo wa Baraza la Wanazuoni alisisitiza kuwa; aya hii ni funzo katika historia yote na kwenye jamii zote, akasema: Binadamu daima hufikiri kwa mantiki ya kimaada na hudhani nguvu zake za kimaada zitamzuia kushindwa, lakini Mwenyezi Mungu ni Mtukufu na Mwenye hekima; ngome na maboma kamwe hayawezi kuzuia maangamizi ya madhalimu na wakandamizaji.
Akitaja mifano kutoka historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, aliongeza: Imam Khomeini (r.a.) wakati Khorramshahr ilipokombolewa, mara moja alisema: “Khorramshahr imekombolewa na Mungu.” Na pale mapinduzi ya kijeshi ya Tabas yaliposhindwa, alisema: “Mchanga huu ulikuwa askari wa Mungu.” Huu ndio uaminifu kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu unaosababisha ushindi.
Uchambuzi wa kifasihi wa aya; ihtimali tatu kwa pamoja
Ayatullah Ka‘abi katika sehemu nyingine ya hotuba yake alifanya uchambuzi wa kifasihi wa aya ya pili ya Suratul-Hashr na kusema: Kuhusu uhusiano wa aya hii na aya iliyotangulia (tasbihi ya Mungu), kuna ihtimali tatu ambazo inaonekana yote yanaweza kukubalika kwa pamoja:
Alifafanua: Uwezekano wa kwanza ni kuwa aya hii ni sentensi mpya isiyohusiana moja kwa moja na tasbihi, bali ni kwa ajili ya kumtukuza na kumhimidi Mwenyezi Mungu na kuonesha wazi nguvu Zake. Uwezekano wa pili ni kuwa aya hii ndiyo sababu ya tasbihi; kwa sababu Mwenyezi Mungu ametakasika kutokana na kuwa, wavunja ahadi waasi waweze kuwashinda waja Wake wateule. Uwezekano wa tatu ni kuwa, ni ishara kwa sifa ya “Al-Aziz Al-Hakim” katika aya iliyotangulia.
Alibainisha kuwa, katika istilahi ya balagha tamko hili huitwa “upekee wa madai”; yaani, kazi zenu enyi Waumini mbele ya kazi ya Mungu si chochote, na yote mliyoyapata ni kwa wasaa wa Mwenyezi Mungu.
Watu wa Kitabu; tofauti kati ya ukafiri wa kiitikadi na ukafiri wa kisiasa
Mwakilishi wa Baraza la Wanazuoni aliendelea kufafanua ibara “wale waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu” na akauliza: Inawezekanaje Watu wa Kitabu, wanaomuamini Mungu na Siku ya Kiyama, waitwe makafiri?
Akajibu: Ukafiri hapa una maana mbili: kwanza ni ukafiri kwa Unabii na Utume wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) unaopelekea ukafiri kwa Mungu; lakini jambo muhimu zaidi ni kuwa ukafiri katika aya hii una maana ya kukataa dola na serikali ya Kiislamu na kuvunja mkataba dhidi ya Katiba ya Madina.
Ayatullah Ka‘abi akieleza kuwa, Watu wa Kitabu wako katika makundi mawili, alisema: Kundi la kwanza ni Watu wa Kitabu walio chini ya mkataba ambao licha ya kutoukubali Uislamu, wanakubali sheria za dola ya Kiislamu na wanaishi kwa amani. Qur’ani Tukufu inasema: “Maadamu wao wanashikamana nanyi kwa ahadi, nanyi shikamaneni nao.” Kundi la pili ni wale wanaosimama dhidi ya dola ya Kiislamu na kufanya mapinduzi na uasi. Bani Nadhir walikuwa miongoni mwa kundi hili.
Alisisitiza: Sababu ya kupigana na Mayahudi wa Bani Nadhir haikuwa tu kwa sababu hawakumuamini Mungu au Mtume, bali kwa sababu walisimama dhidi ya dola ya Kiislamu na wakaupinga utawala wa Kiislamu.
Jinsi nguvu ya bandia ilivyoangamia
Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni alitafsiri ibara isemayo; “kwa mkusanyiko wa kwanza” na kusema: “Hashr” maana yake ni kukusanya na kufukuza. “Hashr ya kwanza” maana yake ni mara ya kwanza wavunja ahadi hawa kufukuzwa na kuhamishwa kuyatoka makazi yao. Hii ilikuwa fahari kwa Uislamu kwamba, awamu ya kwanza ya kufukuzwa na kushindwa kwa fedheha iliwashukia wao.
Aliongeza: Ibara “Mungu aliwajia kwa upande ambao hawakutarajia” ina maana kuwa; Mwenyezi Mungu aliwapiga pigo kutoka sehemu ambayo haikuingia katika mawazo yao. Kama ilivyo katika aya inayosema kuwa, Mwenyezi Mungu hubomoa miundombinu ya ustaarabu wa batili wa kimaada. Ustaarabu unaojengwa juu ya batili, uonevu, ufisadi na dhulma, ni kama jengo lenye msingi dhaifu, huanguka kwa msukumo mdogo tu.
Ayatullah Ka‘abi akifananisha hali ya Bani Nadhir na ustaarabu wa Magharibi wa kimaada alisema: Marekani pamoja na mapambo na maonesho yake ya nguvu, iko katika njia ya kusambaratika. Leo ustaarabu wa Magharibi unakabiliwa na migogoro mikubwa kama mgogoro wa uongozi, mgogoro wa kiroho, mgogoro wa familia, mgogoro wa usalama na pengo la kitabaka. Haya si maneno yetu tu; hata Wamagharibi wenyewe wanakiri kuwa Uislamu barani Ulaya na Magharibi kwa ujumla unaendelea kwa kasi na kwa mwendo wa kupaa.
Ushindi wa kisaikolojia wa upande wa haki
Mwakilishi wa Baraza la Wanazuoni akirejelea ibara isemayo “na akatupa hofu katika nyoyo zao”, alisema: “Kutupa” hapa ni kwa maana ya kurusha kwa nguvu na kwa ghafla. Mwenyezi Mungu aliingiza kwa ghafula hofu kali katika nyoyo zao. Saa moja kabla walikuwa katika kilele cha nguvu na kiburi, ghafla mambo yakavurugika.
Akaeleza kuwa; Mwenyezi Mungu ameweka miongoni mwa sababu za ushindi wa upande wa haki ni kuvunjika kisaikolojia na kiroho kwa adui. Aliongeza: Nilisema katika darsa zilizopita kuwa; Imam wa Zama (a.f.) atashinda kwa zana tatu: Waumini, Malaika na hofu pamoja na ushindi wa kisaikolojia dhidi ya adui. Hata katika medani ya vita vya kisaikolojia, upande wa haki ndio mshindi.
Kubomoa nyumba kwa mikono yao wenyewe
Ayatullah Ka‘abi akifafanua ibara isemayo “wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini”, alisema: Baada ya Mtume (s.a.w.w.) kuwapa Bani Nadhir onyo la kuondoka Madina ndani ya siku kumi hadi ishirini na nne, mwanzoni walipinga. Abdullah bin Ubayy (kiongozi wa wanafiki) aliwaahidi msaada wa watu elfu mbili, na washirikina wa Kiquraysh pia waliwatumia ujumbe kuwa wako pamoja nao.
Aliendelea: Walipoona upinzani haukuzaa matunda na Mtume (s.a.w.w.) akaanza kuizingira na kukata mitende yao, Bani Nadhir walijisalimisha na wakakubali kuondoka kwa sharti la kuchukua mali zao. Mtume alisema hamwezi kubeba silaha na zana kuu, lakini mnaweza kubeba fanicha kwa ngamia. Walianza kung’oa mbao na milango ya nyumba zao ili waichukue. Kisha Waislamu wakaingia na kubomoa yaliyobaki.
Falsafa ya kutajwa kwa visa vya kihistoria katika Qur’ani
Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni, akirejelea aya ya 111 ya Suratu Yusuf: “Kwa hakika katika visa vyao kuna mazingatio kwa wenye akili”, alisema: Falsafa ya kutajwa kwa visa hivi vyote katika Qur’ani ni kuchukua funzo kutokana na mwisho wa kuvunja ahadi, upenyezaji wa unafiki na kusimama dhidi ya mfumo wa Kiislamu.
Alibainisha: Bani Nadhir kwa kutumia vibaya kushindwa kwa dhahiri kwa Waislamu, walijaribu kueneza taswira ya udhaifu wa dola ya Kiislamu, kuwachochea maadui wa nje na kudhoofisha misingi ya utawala wa kidini. Leo pia mitandao ya upenyezaji, unafiki na vita vya kimtazamo na kimedia vya adui, kwa muundo huohuo, inalenga kuharibu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika fikra za umma.
Mafunzo manne kutokana na fitna ya Bani Nadhir katika zama za leo
Ayatullah Ka‘abi akisisitiza ibara isemayo: “Basi chukueni funzo, enyi wenye kuona”, alitoa masomo manne muhimu kutokana na tukio hili la kihistoria katika hali ya sasa:
1. Wajibu wa kukata vyanzo vya nguvu za wachochezi wa fitna
Alisema: Ni lazima tukate vyanzo vya mamlaka ya wachochezi wa fitna. Hatua thabiti na wazi dhidi ya usaliti ni sharti la utulivu na usalama. Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) hakuwahi kuruhusu usaliti wa Bani Nadhir ufasiriwe baadaye kwa visingizio kama kusema hatukukusudia, tulikosea, au tunataka kufidia. Mara tu alipogundua kuwa hawapo tena pamoja na Uislamu na dola ya Kiislamu na wamechukua upande mwingine, hakuruhusu jambo hilo kuwa la tafsiri, na alikataza muamala wa kulegeza mambo.
Aliongeza: Lau angelilegeza mambo, huenda fitna ingezimika kwa muda, lakini baadaye wachochezi wangepata fursa ya kujijenga upya. Hatua ya kuwafukuza Bani Nadhir na kukata vyanzo vya nguvu zao ilisababisha mpango wa mapinduzi ushindwe. Huu ni mwongozo wetu leo katika kukabiliana na upenyezaji na fitna za ndani.
2. Kujiepusha na matumaini ya uongo kwa waliodanganywa
Ayatullah Ka‘abi alisema: Mara nyingi katika fitna, wanafiki hudanganya kundi la watu na kuwasukuma mbele. Baada ya vumbi la fitna kutulia, waliodanganywa hujutia, lakini majuto hayo huwa hayana faida. Unafiki usio na gharama ni hatari na huleta maangamizi. Aliendelea: Wanafiki daima huingiza matumaini ya uongo kwa watu wasio na uzoefu na kuwasukuma uwanjani, lakini wakati wa mgogoro huwaacha peke yao; kama ilivyokuwa kwa Abdullah bin Ubayy na wenzake, waliowaahidi Bani Nadhir msaada wa watu elfu mbili lakini baadaye wakawaacha.
Alibainisha: Uzoefu wa fitna za karibuni unaonesha kuwa wale wanaotegemea ahadi za nje na msisimko wa ndani, mwishowe hukumbana na kushindwa na kuvunjika moyo. Mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kutegemea irada ya kitaifa na uongozi wa busara na jasiri, ni thabiti na wa kudumu; na hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa taifa la Iran.
3. Wajibu wa kuwasafisha wachochezi wa fitna
Alisema: Wachochezi wa fitna lazima, kwa mujibu wa kauli ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, “wawekwe majivu.” Nguvu ya kitaifa na uratibu kati ya diplomasia na medani ni kizuizi imara dhidi ya adui. Kama Mtume (s.a.w.w.) alivyoisafisha Madina kutokana na tishio, leo pia nguvu ya ulinzi, nguvu ya makombora na usalama wa mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu vinaweza kuwa nguzo ya kuaminika kwa diplomasia ya nchi.
Ayatullah Ka‘abi alisisitiza: Muamala wa kulegeza mambo na kunyamaza mbele ya vitisho si tu hauzuii, bali humfanya adui awe jasiri zaidi.
4. Kubadilika kwa zana na kudumu kwa mantiki ya kukabiliana
Mwakilishi wa Baraza la Wanazuoni alisema: Zana zinaweza kubadilika. Zamani maadui walijikusanya nyuma ya ngome zao, lakini mantiki ya tishio na kukabiliana ni ileile. Waasi wa zama zetu, kama Bani Nadhir, kwa kuusaliti Uislamu na Mapinduzi, kwa msaada wa vita vya kisaikolojia, mitandao ya kimedia pinzani na operesheni za upenyezaji, hutengeneza mazingira ya uchochezi na msisimko wa kijamii.
Aliongeza: Vita vya Bani Nadhir vinatufundisha kuwa, ikiwa upenyezaji, unafiki na mapinduzi hayatachukuliwa kwa uzito, usalama wa taifa utaingia hatarini. Hivyo, kukabiliana kwa busara, kwa uwazi na kwa uthabiti na adui ni sharti la kulinda uadilifu na utulivu wa kijamii.
Onyo muhimu la Kiongozi wa Mapinduzi kwa vyombo vya usalama na mahakama
Ayatullah Ka‘abi katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake alirejelea matamshi ya hivi karibuni ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khamenei, na kusema: Mtukugu huyo katika mkutano na watu wa Azerbaijan ya Mashariki alitoa onyo muhimu kwa vyombo vya usalama na mahakama ambalo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
Akinukuu kauli ya Kiongozi Mkuu, alisema: “Vyombo vya usalama na mahakama vina wajibu wa kuwachukulia hatua za kisheria na kwa uadilifu wale wanaoandamana, kushirikiana na kuwa na sauti moja na adui — iwe kwa vitendo, kwa maneno au kwa uchambuzi. Mimi si mfuasi wa ukali usio na sababu, lakini kulegeza mambo bila sababu pia kama ukali usio na sababu, huipa nchi hasara.”
Naibu Mwenyekiti wa Jumuia ya Walimu wa Hawza ya Qom, mwishoni alibainisha: Ustaarabu wa kimaada wa Magharibi pamoja na mapambo yake umejengwa juu ya misingi dhaifu ya batili, uonevu, ufisadi na dhulma, na uko katika njia ya kusambaratika; kama ilivyokuwa ngome imara za Bani Nadhir zilivyoanguka kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu.
Maoni yako