Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Nadhir Ayyad, Mufti wa Jamhuri ya Misri, alisisitiza kuwa, mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa msamaha wa Mwenyezi Mungu na msimu mkubwa wa kiimani wa kurekebisha maadili, kuimarisha mahusiano, na kuendeleza thamani za huruma na mshikamano wa kijamii.
Mufti wa Misri alieleza kuwa, Ramadhani inapaswa kuwa kituo halisi cha kujitathmini na kuyafanya upya maisha ya kiroho, si msimu wa kupita wa ibada tu, bali ni fursa ya kuhuisha nyoyo, kurekebisha mwenendo, na kujenga nafsi juu ya ukweli na ikhlasi.
Aliongeza kuwa, mwenye kufanikiwa ni yule anayeutumia vyema mwezi huu ili uwe mwanzo wa maisha yaliyo karibu zaidi na Mwenyezi Mungu na yenye manufaa zaidi kwa taifa na jamii.
Ramadhani: Shule ya kujitakasa na kulea maadili
Mufti alieleza kuwa, Ramadhani ni shule kubwa ya kujitakasa nafsi, kurekebisha tabia, na kuimarisha uwajibikaji binafsi na wa kijamii. Ndani yake, mtu hujifunza subira, huwakumbuka wahitaji, na kuhuisha hisia za mshikamano wa kijamii.
Alibainisha kuwa, Ramadhani ni mwezi wa Qur’ani, mwezi wa kuilinda ndimi dhidi ya maudhi, na mwezi wa kuimarisha uhusiano wa kifamilia.
Alisisitiza kuwa, kufunga hakukuamrishwa ili iwe msimu wa ubadhirifu au anasa, bali ni kwa ajili ya kumjenga mtu katika uchamungu (taqwa), kujidhibiti, na kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu.
Wito wa unyenyekevu na kuepuka ubadhirifu
Mufti wa Misri alihimiza kurejesha roho ya urahisi na kuepuka kujionesha katika mwezi huu, akisisitiza kuwa kula na kunywa kupita kiasi hakulingani na lengo la swaumu.
Alisema kuwa; asili ya kufunga ni kuhisi hali ya wahitaji na kudhibiti matamanio. Ubadhirifu hudhoofisha madhumuni ya swaumu, na mtu anapaswa kutumia sehemu ya gharama zake katika sadaka na matendo ya kheri.
Swaumu ya kweli: Kulea nafsi na kumjenga binadamu
Mufti alieleza kuwa; swaumu ina vipengele vya malezi ya kina vinavyopita kuacha kula na kunywa tu. Swaumu humfundisha mtu subira, udhibiti wa matamanio na hisia, na nidhamu ya kuheshimu wakati na mipaka.
Alikumbusha hadithi ya Mtume Muhammad (saww):
“Yeyote asiyeacha kusema uongo na kuutenda, basi hana haja ya kuacha chakula na kinywaji chake.”
Mshikamano wa kijamii na wajibu wa pamoja
Alieleza kuwa, kijamii swaumu huamsha hisia za kuwajali maskini na wahitaji. Ndiyo maana Ramadhani huhusishwa na sadaka, zaka ya fitri, na meza za iftari, kwa kuwa ibada haipaswi kutenganishwa na huruma ya vitendo na mshikamano wa kweli.
Tahadhari kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii
Mufti aliwataka Waislamu, hasa vijana, kusimamia vizuri matumizi ya teknolojia ndani ya Ramadhani, kuitumia kwa manufaa, elimu, na kuimarisha uhusiano mwema, si kwa kupoteza muda au kutumbukia katika maovu.
Alionya kuwa; ikiwa mitandao ya kijamii itageuka kuwa chanzo cha uzembe, uzushi, kusengenya au maudhui yasiyofaa, huenda isibatilishe swaumu kisheria, lakini hupunguza thawabu zake na kuondoa roho ya ibada.
Nafasi ya taasisi za kidini
Mufti alieleza kuwa; taasisi za kidini zina jukumu muhimu la kuiongoza jamii katika mwezi wa Ramadhani, si tu kwa kutoa hukumu za kifiqhi, bali pia kwa kusahihisha fikra na kuimarisha uelewa wa wastani wa dini.
Alitaja jukumu la Dar al-Ifta al-Misriyyah, ambalo huchambua na kufuatilia maudhui ya kidini yanayosambazwa, hasa katika mitandao ya kijamii, na kutoa majibu ya kielimu na yenye mizani dhidi ya fatwa zisizo sahihi au zenye misimamo mikali.
Fatwa katika zama za sasa: Kati ya yasiyobadilika na yanayobadilika
Mufti alifafanua kuwa; fatwa hubadilika kulingana na wakati, mahali na hali za watu, huku ikihifadhi mizani kati ya misingi isiyobadilika ya Sheria na mabadiliko ya uhalisia wa maisha.
Alisisitiza kuwa; kufanya upya katika utoaji wa fatwa hakumaanishi kubadilisha hukumu za Sheria, bali ni kuboresha njia na lugha ya kuwasilisha hukumu hizo ili ziweze kuwafikia watu na vizazi vipya kwa ufanisi zaidi.
Mwisho, alihimiza Waislamu kuufanya mwezi wa Ramadhani kuwa msimu wa kurejea katika mizani, nidhamu, na uhusiano wa kweli na Mwenyezi Mungu, ili kufanikisha malengo ya kiroho na kijamii ya swaumu.
Maoni yako