Jumatatu 23 Februari 2026 - 10:45
Tahadhari ya Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad kuhusu dalili za utawala wa kigeni nchini Iraq

Hawza/ Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad, huku akisisitiza kwamba; uhuru wa Iraq ni kipaumbele cha kitaifa, alionya kuhusu uelekezaji wa kimakusudi wa vyombo vya habari na kuhusu mabadiliko ya kikanda, na akataka kuwepo kwa uangalifu wa kina wa kisiasa pamoja na kushikamana na misingi ya kitaifa mbele ya utawala wa kigeni.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mwalimu mashuhuri wa Hawza ya kielimu ya Najaf Ashraf, katika khutuba za Swala ya Ijumaa ya jana, tarehe mosi Esfand 1404, alisisitiza kwamba: Hali ambayo Iraq inakabiliana nayo leo si tofauti na mabadiliko yanayoendelea katika eneo hili, bali ni sehemu ya taswira pana ya kikanda ambapo maslahi ya madola ya kimataifa na ushindani mkubwa vimefungamana.

Alisema: Wananchi wa Iraq katika miongo mitatu iliyopita wamepitia hatua ngumu na zenye changamoto nyingi, na kulinganisha hali ya kabla ya mwaka 2003 na hali ya baada yake kunaonyesha tofauti kubwa; “hata hivyo, jambo hili halimaanishi kunyamaza mbele ya makosa au kukubali hali ambayo haijibu matakwa ya wananchi.”

Ayatullah Mousawi aliongeza kuwa: Ukosoaji unaoelekezwa kwa mchakato wa kisiasa unatokana na nia ya dhati ya kujenga “dola huru, yenye nguvu na ya kitaifa”; dola inayotegemea wananchi wake, inayolinda haki za raia wake — hususan tabaka zilizonyimwa na za wanyonge.

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad, akilikosoa muundo wa sasa wa kisiasa, alibainisha kuwa: Mfumo huu uliundwa kwa uungwaji mkono na usimamizi wa Marekani na bado uko chini ya athari za mambo ya nje yanayozuia maendeleo na mageuzi yake. Alikumbusha kwamba: Marekani haitafuti mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa mfumo wa kisiasa wa Iraq, kwa kuwa inautathmini kuwa unaendana na maslahi yake.

Mwalimu huyu wa Hawza ya kielimu ya Najaf alionya kuhusu “uelekezaji wa kimakusudi wa vyombo vya habari” na akawataka wananchi wa Iraq washikamane na misingi na thabiti za kitaifa, juu yake ikiwa ni uhuru kamili na kukataa aina yoyote ya utawala wa kigeni.

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alisisitiza: Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii wakati mwingine vinaweza kutumika katika kuelekeza maoni ya umma kwa mujibu wa ajenda za nje; kwa hiyo, uangalifu wa kisiasa unaojengwa juu ya misingi na ulio mbali na mihemko ni jambo la lazima.

Ayatullah Mousawi aliendelea kwa kugusia mabadiliko ya kikanda na kusema: Iraq iko katika kiini cha matukio ya eneo hili, na mvutano unaoendelea kati ya Marekani na Iran hauishii tu huko Tehran, bali unaathiri mizani yote ya Mashariki ya Kati.

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliongeza kusema: Mapambano yoyote makubwa yatakuwa na athari pana ambazo hazitayahusu tu mataifa ya eneo hili, bali pia mfumo mzima wa kimataifa; hasa katika hali ambayo ushindani uliopo kati ya Marekani na China unaendelea kuongezeka.

Aidha, alizungumzia faili la mazungumzo ya nyuklia kati ya Washington na Tehran na kubainisha: Kurudiwa kwa misimamo mikali na ya vitisho si lazima kumaanishe kutokea kwa vita karibuni, na lugha ya vitisho mara nyingi hutumika katika mfumo wa shinikizo la kisiasa.

Ayatullah Mousawi alisisitiza kuwa: Uzoefu wa zamani umeonesha kwamba; “mahesabu ya kijeshi hayaamuliwi tu kwa msingi wa nguvu ya juu juu, bali pia mambo kama subira, azma na maandalizi yana nafasi ya kuamua.”

Mwisho, Imamu wa Sala ya Ijumaa wa Baghdad alikumbusha kwa kusema: Wajibu wa wananchi wa Iraq ni kuimarisha msimamo wa kitaifa na huru na kuunga mkono kila kilicho katika mwelekeo wa kulinda mamlaka na umoja wa nchi. Kwa kukataa “sera ya maagizo ya kigeni”, alisisitiza kwamba: Mustakabali wa Iraq unapaswa kuamuliwa kwa irada na maamuzi ya wana wa ardhi hii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha