Ijumaa 13 Februari 2026 - 19:10
Maadhimisho ya Milenia ya Hawza ya Najaf Yaanza; Msisitizo juu ya Kufufua Turathi za Sheikh Tusi

Hawza/ Hafla ya ufunguzi wa kikao cha awali cha kongamano la kwanza la kielimu la kuadhimisha miaka elfu moja ya Hawza ya Kielimu ya Najaf Ashraf ilifanyika Jumatano, tarehe 11 February, chini ya usimamizi wa Haram tukufu ya Hadhrat Abbas (as) katika mji wa Najaf.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, hafla ya ufunguzi wa kikao cha awali cha kongamano hilo iliandaliwa na Kituo cha Sheikh Tusi kwa ushirikiano na Kamati Kuu ya Kufufua Turathi na Chuo cha Tafiti za Kishia cha Toronto, chini ya usimamizi wa Ataba Tukufu ya Hadhra Abbas (a.s) mjini Najaf Ashraf.

Kaulimbiu ya kongamano hili imetangazwa kuwa: “Hawza ya Kielimu ya Najaf Ashraf, miaka elfu moja ya urithi wa kielimu”, na anuani yake ni: “Turathi za Sheikh Tusi katika fikra za Kiislamu na Magharibi; mitazamo ya kisasa.”

Katika tukio hili la kitamaduni, watafiti na shakhsia za kielimu kutoka zaidi ya nchi saba duniani walihudhuria.

Hotuba ya ufunguzi ya msimamizi wa Kisheria wa Ataba Tukufu ya Hadhra Abbas (a.s)

Hotuba ya ufunguzi ilitolewa na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad Safi, Msimamizi wa Kisheria wa Ataba ya Hadhrat Abbass (as). Akiwashukuru wajumbe wa kielimu walioshiriki kutoka ndani na nje ya nchi, alisisitiza: “Madrasah ya Ahlul-Bayt (a.s) inamiliki turathi kubwa na ambayo bado haijafahamika kikamilifu.”

Msimamizi huyo wa Kisheria, akigusia nafasi ya kipekee ya Shaykh al-Tusi huko Baghdad na mazingira magumu ya zama hizo, alieleza kuwa kuhama kwake kuja Najaf kulikuwa ni hatua ya kihistoria katika historia ya kielimu ya mji huo, na akasema: “Baada ya kupita miaka elfu moja, fikra na athari za Sheikh Tusi bado ziko hai na zinaendelea kuwa na taathira.” Pia alizipongeza juhudi kubwa za taasisi zilizoandaa kongamano hilo.

Taarifa ya Kamati Kuu ya Kufufua Turathi

Baadaye, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Abdulhakim Safi, msimamizi wa Kamati Kuu ya Kufufua Turathi, katika hotuba yake aliielezea Najaf kuwa katika karne nyingi imekuwa kitovu cha uzalishaji wa fikra za Kiislamu na uelewa wa kidini.

Alibainisha kuwa mradi wa kuadhimisha milenia ya Hawza ya Najaf Ashraf ulianza miaka kadhaa iliyopita ukiwa na mihimili minne mikuu: uandishi, utafiti, uandaaji wa vikao na makongamano, na kufufua turathi za Sheikh Tusi. Aidha alitangaza kuchapishwa kwa kazi tatu mpya zenye thamani kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa Najaf.

Shukrani za mtafiti wa Kanada kwa nafasi ya Ataba Tukufu ya Hadhrat Abbas (a.s)

Dkt. Fini Khitia, Mkuu wa Taasisi ya Tafiti za Kishia nchini Kanada, katika hotuba yake aliisifu nafasi ya Ataba Tukufu ya Hadhrat Abbas (a.s), katika kuadhimisha Sheikh Tusi, na kueleza kuwa msaada na wezesho uliotolewa umeimarisha ushirikiano wa kielimu.

Uzinduzi wa kazi mbili mpya

Katika sehemu nyingine ya hafla hiyo, vitabu viwili vipya vilivyohakikiwa na kuchapishwa na Kituo cha Sheikh Tusi vilizinduliwa:

1. Rasa’il al-Fadhil al-Fasharki cha Allama Sheikh Muhammad Baqir Fasharki Isfahani (1252–1314 H).

2. Hidayat al-Anam fi Hukm Amwal al-Imam cha Allama Sheikh Abdullah Mamaqani (1290–1351 H).

Vikao vya kielimu vya ufunguzi

Katika kikao cha kwanza cha kielimu kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha al-Murtadha (a.s), tafiti mbili ziliwasilishwa:

1. Ulinganishi wa vitabu vitatu vya Amaalī vya hadithi

Mwasilishaji: Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Muhammad Jawad Shubayri Zanjani, mtafiti na mwalimu wa darasa la Kharij katika Hawza ya Qom.

Utafiti huu ulichambua kwa kulinganisha Amaalī za Saduq, Mufid na Tusi, na kueleza changamoto za nakala zilizopo za Amaalī ya Sheikh Tusi. Mtafiti alisisitiza umuhimu wa kuifanyia kazi upya kwa msingi wa nakala za maandishi ya mkono.

2. Mageuzi ya fikra ya Mahdawi kwa anuani: “Kutoka Ghaybah hadi Ghaybah” (kutoka Ghaybah ya Nu‘mani hadi Ghaybah ya Sheikh Tusi)

Mwasilishaji: Dkt. Mathieu Terrier, Mkurugenzi wa Masomo ya Utafiti wa Dini mjini Paris.

Utafiti huu ulilinganisha mbinu za waandishi wawili (Nu‘mani na Sheikh Tusi) katika kutumia riwaya na akili kuthibitisha ghaiba ya Imam, na ukaonesha jinsi fikra ya kielimu ya kalamu ilivyohama kutoka kutegemea riwaya pekee hadi kuelekea hoja za kiakili.

Pia mtazamo wa Sheikh Tusi kuhusu ulazima wa kuwepo Imam, suala la badaa, na ukosoaji wake kwa wanaodai kuwa na mawasiliano na Imam wa Zama (a.f) ulichambuliwa katika utafiti huo.

Kuwatambua watafiti walioshiriki

Mwisho wa kikao hicho, Msimamizi wa Ataba Tukufu ya Hadhrat Abbas (a.s) aliwashukuru washiriki wa mkutano na kuzipongeza juhudi zao za kielimu katika kuandaa tafiti zilizochangia kuimarisha kongamano na kubainisha vipengele vya kifikra vya mada husika.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha