Jumamosi 3 Januari 2026 - 14:59
Anae Pinga kwa Hoja Tunajadiliana nae, Ama Muhuni na Mfanya Vurugu, Yafaa Awekwe Panapostahiki

Hawza/ Sambamba na maadhimisho ya heri ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa baraka Amirul-Muuminina, Bwana Ali (a.s), maelfu ya familia tukufu za mashahidi wa vita vya siku 12 (Mashahidi wa Uthabiti), leo asubuhi walikutana na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi, katika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa heri ya Kiongozi wa Waumini, Ali bin Abi Taalib (a.s), na pia katika kumbukumbu ya sita ya kuuawa kishahidi Jenerali Qassem Soleimani, alipokutana na familia tukufu za mashahidi wa vita vya siku 12 (Mashahidi wa Uthabiti), alieleza kuwa uadilifu na uchamungu wa Amirul-Muuminina ni vilele viwili vinavyohitajika na nchi, na ni sifa za lazima kabisa kwa uongozi katika jamii. Akitilia mkazo umuhimu wa kuwa macho na kuimarisha umoja wa kitaifa mbele ya “vita laini” vya maadui, alisema: Vita hivi vinavyojengwa juu ya udanganyifu, uongo, tuhuma na uvumi ndivyo vile ambavyo maadui wa serikali ya Alawi walivianzisha baada ya kushindwa kijeshi mbele ya Imam Ali (a.s), ili kuzuia kufikiwa malengo yake.

Ayatollah Sayyid Ali Khamenei alitaja siku ya kuzaliwa Amirul-Muuminina kuwa siku ya kipekee katika historia kwa kuzingatia mahali pa kuzaliwa—yaani Nyumba ya Mwenyezi Mungu (Kaaba)—na pia kwa kuzingatia aliyeyezaliwa humo. Akaongeza: Miongoni mwa sifa zake za kipekee, leo tunahitaji kwa dharura zaidi sifa mbili, yaani “uadilifu na uchamungu”, na kwa kumfanya kiongozi wa Wachamungu kuwa kigezo, tunapaswa kuelekea kwenye vilele hivi viwili ambavyo Amirul-Muuminina alisimama juu yake; ingawa katika njia hii tumepata maendeleo fulani, bado tuna umbali kabla ya kufikia pale tunapopaswa kufika.

Kiongozi wa Mapinduzi, akifafanua mbinu mbalimbali alizotumia Imam Ali bin Abi Taalib (a.s) katika kutekeleza uadilifu, alisema: Wakati mwingine alitekeleza uadilifu kwa huruma, kuhudumia wanyonge na familia zisizo na walezi; wakati mwingine kwa Zulfiqar na ukali wa kimungu; na wakati mwingine kwa lugha fasaha, hekima na ufafanuzi.

Alimtaja Amirul-Muuminina kuwa chanzo cha jihadi ya ufafanuzi (jihadi ya kubainisha haki) na akaongeza: Amri yake ya kiutawala kwa Malik al-Ashtar imejaa maudhui yanayotekeleza uadilifu.

Ayatollah Khamenei, akielezea mbinu za Imam Ali (a.s) kuhusu uchamungu, alisema: Wakati mwingine Amirul-Muuminina alidhihirisha uchamungu katika mihraabu ya ibada, swala na kunyenyekea mbele ya Mola, kiasi cha kuwafanya malaika wa Arshi washangae na wahusudu; wakati mwingine alitekeleza kwa subira, ukimya na kuacha haki yake binafsi ili kulinda umoja wa Waislamu na kuzuia migawanyiko; na wakati mwingine kwa kusimama kifua mbele katika nyakati ngumu kama Lailatul-Mabit na vita vya Mtume (s.a.ww).

Akitilia mkazo umuhimu wa watu wote, hususan viongozi, kufuata mbinu za uchamungu za Amirul-Muuminina, aliongeza: Uadilifu wa Alawi pia ni hitaji la lazima na la dharura zaidi kwa nchi, na leo—tofauti na Mashia katika historia—hatuna udhuru wowote wa kutofuatilia au kutotekeleza uadilifu; kwa sababu tunayo Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu na mfumo wa Alawi.

Kiongozi wa Mapinduzi, akieleza vikwazo vya utekelezaji wa uadilifu na uchamungu, alisema: Wakati mwingine hofu, wakati mwingine shaka na kuzingatia urafiki, na wakati mwingine kumjali adui, huzuia kazi; lakini bila kuzingatia mambo yasiyo na msingi, lazima tuendelee kuelekea kuendeleza uadilifu na uchamungu.

Akielezea umakini wa wananchi na viongozi kwenye jambo muhimu katika maisha ya Amirul-Muuminina, alisema: Inapaswa kuzingatiwa kuwa kiongozi wa wachamungu katika mapambano yote ya kijeshi wakati wa Mtume (s.a.ww) na katika miaka ya utawala wake alikuwa mshindi, lakini mbinu mbalimbali za maadui walioshindwa—za kudanganya na kuwadhoofisha watu—mara nyingi zilizuia kufikiwa kwa malengo ya Imam Ali (a.s).

Kiongozi wa Mapinduzi alieleza kuwa kueneza uvumi, kutumia uongo, udanganyifu, kupenyeza (upelelezi) na mbinu zinazofanana, au kwa lugha ya leo “vita laini”, vilikuwa sera za maadui wa kiongozi wa Wachamungu ili kuwapunguzia watu ari na kueneza hofu katika jamii ya wakati huo. Akasema: Watu wanapolegea, kufikia kwa malengo inakuwa vigumu; kwa sababu kwa mujibu wa sunna ya Mwenyezi Mungu, kazi iko mikononi mwa watu na hufanywa na wao.

Ayatollah Khamenei alitaja lengo la adui katika vita laini kuwa, kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa watu na kueneza hofu ndani ya taifa. Akasema: Kama ilivyokuwa katika zama za Amirul-Muuminina kwa kueneza uvumi na uongo ili kuwafanya watu wawe na mtazamo mbaya, leo pia vitendo hivyo vinafanywa vivyo hivyo; hata hivyo, taifa la Iran limeonyesha kwamba katika nyakati ngumu na kila panapohitajika uwepo na msaada wake, linasimama imara na humvunja moyo adui.

Alitaja motisha kubwa ya taifa la Iran kuwa chanzo cha wasiwasi kwa wenye nia mbaya, na akaongeza: Moja ya zana za adui na baadhi ya watu waovu au wazembe katika uwanja wa vita laini ni kukanusha mafanikio na uwezo wa taifa la Iran, kwa kuwa kupuuza uwezo wa kitaifa huandaa mazingira ya kudharauliwa na kujisalimisha mbele ya adui.

Alisema; kutumwa setilaiti tatu angani kwa siku moja na maendeleo ya kushangaza katika nyanja mbalimbali za kisayansi nchini—ikiwemo anga, baioteknolojia, uganga, matibabu, nanoteknolojia, na viwanda vya ulinzi na makombora—kuwa ni mifano ya kazi kubwa za taifa na vijana wake mahiri. Akasema: Adui na kwa bahati mbaya baadhi ya watu ndani ya nchi huficha maendeleo haya makubwa yaliyopatikana chini ya vikwazo na hawayafikishi kwa wananchi.

Ayatollah Khamenei aliongeza: Sababu iliyomlazimisha adui kuomba kusitishwa kwa vita, na baadaye pia kutuma ujumbe kuwa hataki kupigana nanyi, ni nguvu na uwezo wa taifa la Iran; hata hivyo, hatuamini maneno ya adui mwovu, mdanganyifu na mwongo.

Akitaja wastani wa umri wa miaka 26 wa wanasayansi walioshiriki katika kurusha setilaiti tatu za hivi karibuni, alisema huu ni mfano wa utajiri mkubwa wa rasilimali watu wa taifa la Iran. Akaongeza: Wakati yule Mmarekani msemaji wa upuuzi anapozungumza kuhusu taifa la Iran, husema maneno mabaya kiasi fulani na kutoa udanganyifu na ahadi kiasi fulani; lakini kwa bahati nzuri leo taifa la Iran—na hata dunia nzima—imemtambua Marekani, na fedheha yake imedhihirika duniani.

Kiongozi wa Mapinduzi alisema kumjua adui kwa uhalisia kuwa ni mafanikio makubwa, na akaongeza: Watu katika vita vya siku 12 walijionea ukweli wa Marekani. Hata wale waliodhani kuwa suluhisho la matatizo ya nchi ni makubaliano nao, walitambua kuwa katikati ya mazungumzo, serikali ya Marekani ilikuwa ikijiandaa kuchora mipango ya vita.

Alisisitiza umuhimu wa kuwa makini dhidi ya vita laini, kueneza hofu na uvumi wa adui, na akataja mabilioni ya dola yanayotumika kusambaza kauli za uongo ndani ya Iran kupitia vituo vya televisheni na vyombo vya habari. Akasema: Lengo lao ni kuidhoofisha nchi na kuvuruga umoja wa kimiujiza wa taifa katika vita vya siku 12. Hivyo, jambo muhimu zaidi ni kuzingatia uadui wa adui, umoja wa ndani, na kwa mujibu wa Qur’ani: “Wenye nguvu dhidi ya makafiri, wenye huruma baina yao.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akirejea mikusanyiko ya wiki iliyopita ya wafanyabiashara, alisema: Soko na wafanyabiashara ni miongoni mwa tabaka zilizo waaminifu zaidi kwa mfumo na Mapinduzi ya Kiislamu, na tunawajua vizuri; hivyo haiwezekani kwa jina la soko na wafanyabiashara kupambana na Jamhuri ya Kiislamu.

Alitaja malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kuporomoka kwa thamani ya fedha ya taifa—ambako husababisha kuyumba kwa mazingira ya biashara—kuwa ni malalamiko ya haki. Akaongeza: Mfanyabiashara anasema ukweli anaposema kuwa kwa hali hii hawezi kufanya biashara; jambo hili linakubaliwa pia na viongozi, na Rais mheshimiwa pamoja na viongozi wengine wa juu wanatafuta tiba ya tatizo hili.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongeza: Hata hivyo, katika tatizo hili pia mkono wa adui umo kazini, na kuyumba na kupanda bila mpangilio kwa bei ya fedha za kigeni kunakosababisha kutokuwepo kwa uhakika miongoni mwa wafanyabiashara si jambo la kawaida; kwa mikakati mbalimbali lazima kuzuiwe, na viongozi wanafanya juhudi katika uwanja huu.

Ayatollah Khamenei akasisitiza kuwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu tatizo hili ni ya haki, alisema: Lakini kisichokubalika ni kusimama kwa baadhi ya watu waliopandikizwa au vibaraka wa adui nyuma ya wafanyabiashara na kutoa kauli mbiu zinazopinga Uislamu, Iran na Jamhuri ya Kiislamu.

Akitilia mkazo kauli kwamba “kulalamika ni haki, lakini kulalamika ni tofauti na kufanya fujo”, alisema: Viongozi wanapaswa kuzungumza na wanaolalamika, lakini kuzungumza na mfanya-fujo hakufai; bali lazima akae mahali pake.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongeza: Kwamba watu fulani, chini ya majina na vyeo mbalimbali, kwa nia ya uharibifu na kuleta ukosefu wa usalama, wajipange nyuma ya wafanyabiashara waumini, wenye afya ya kimaadili na kimapinduzi, na kwa kutumia vibaya malalamiko yao wafanye fujo, jambo hilo halikubaliki kabisa.

Alisena kutumia fursa kuwa ni kazi ya kudumu ya adui, na akarejea uwepo wa viongozi uwanjani, akasema: Jambo muhimu ni utayari wa jumla wa taifa na kuimarisha vipengele kama imani, ikhlasi na vitendo vile vilivyomfanya Soleimani awe Soleimani. Jambo muhimu ni kutojali dhidi ya vita laini na uvumi wa adui, na kusimama imara, kifua mbele, kwa nguvu kamili dhidi ya madai yake ya kibabe kwa viongozi, serikali na taifa.

Ayatollah Khamenei alisisitiza: Hatutarudi nyuma mbele ya adui, na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuamini uungaji mkono wa watu, tutamwinamisha adui mpaka apige magoti.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akirejea kuingiliana kwa kumbukumbu ya kuuawa kishahidi kwa shahidi mkubwa Haj Qassem Soleimani na tarehe 13 Rajab, alisema: Sifa tatu—imani, ikhlasi na vitendo— ndizo zilikuwa sifa kuu za shahidi huyo mpendwa, ambaye alihesabiwa kuwa binadamu kamili na wa kina katika zama zetu.

Alisema imani ya kina kwa Mola na msaada wa Mwenyezi Mungu, na imani kwa lengo, kuwa ni sifa bainifu ya Jenerali wa watu. Akaongeza: Haj Qassem alikuwa mtu wa ikhlasi ya kimungu, na hakufanya kazi kwa ajili ya sifa au kusifiwa na watu.

Kiongozi wa Mapinduzi, akitukuza uwepo wa Jenerali Soleimani katika nyanja zote muhimu, alisema: Yeye, tofauti na baadhi ya watu wanaoelewa vizuri na kuzungumza vizuri lakini hawachukui hatua, alikuwepo katika kila uwanja uliotakiwa; iwe ni katika kulinda na kuelekeza harakati za Mapinduzi na kukabiliana na uhalifu huko Kerman, au katika Kikosi cha Quds, kutetea Haram, kupambana na Daesh, na nyanja nyingine.

Ayatollah Khamenei akirejea athari dhahiri na ya kipekee ya Jenerali katika masuala nyeti na muhimu zaidi ya kisiasa ya eneo, aliongeza: Haj Qassem alijitahidi sana kuwalea na kuwafundisha wapiganaji wenzake na vikosi vilivyo chini ya amri yake; na kwa sababu ya sifa hizi, kaburi lake linazidi kuwa takatifu na lenye heshima kila mwaka, na umati mkubwa wa watu kutoka maeneo ya mbali, hata kutoka nchi nyingine, huenda kulizuru kaburi lake.

Kiongozi wa Mapinduzi pia, akirejea uwepo wa familia za mashahidi wapendwa wa vita vya siku 12 katika kikao hicho, alisema: Kikao hiki kimeandaliwa kwa kutukuza, kuheshimu na kuadhimisha mashahidi wote wa utetezi mtukufu wa siku 12 na familia zao—iwe ni majenerali waliotamani jihadi na shahada, wanasayansi wenye uwezo mkubwa, au mashahidi wengine.

Akasitiza: Majina ya mashahidi hawa wote yatabaki katika historia, na tunapaswa kunufaika na baraka za majina haya matukufu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha