Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, kufuatia baadhi ya matendo na maneno ya dharau dhidi ya matakatifu ya madhehebu ya Kiislamu, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Maraji‘ wakubwa wa taql'id, kwa kutoa fatwa mbalimbali, wamesisitiza juu ya uharamu wa kisheria wa mienendo kama hiyo, wameonya kuhusiana na athari hatarishi zinazo tokana na vitendo hivyo, huku wakivitaja kuwa ni usaliti dhidi ya Uislamu na ni sawa na kuwatumikia maadui wa umma mmoja, na wakataka watu wote kuheshimiana, kujiepusha na kuchochea mifarakano na kuimarisha mshikamano kati ya Waislamu.
Mtukufu Ayatullah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu:
“Mimi, kama wanavyosema maulamaa na wapenzi wengi wa umma wa Kiislamu, natangaza tena kwamba kila kauli na kitendo kinachoweza kuchochea moto wa mifarakano baina ya Waislamu, na vilevile matusi dhidi ya matakatifu ya madhehebu yoyote ya Kiislamu au kukufurisha baadhi ya madhehebu ya Kiislamu, ni sawa na kuihudumia kambi ya ukafiri na ushirikina, ni usaliti dhidi ya Uislamu na ni haramu kisheria.”
Pia, kuhusu kushiriki katika vikao vinavyotusi matakatifu ya madhehebu mengine ya Kiislamu, amesema: “Kila aina ya kauli, matendo au mwenendo ambao katika zama hizi unampa adui kisingizio au unasababisha mifarakano na mgawanyiko baina ya Waislamu, ni haramu kisharia.”
Ayatullah al-‘Udhma Sistani:
Marja‘ mtukufu Ayatullah al-‘Udhma Sistani, katika jibu lake kwenye istifta ya mmoja wa wafuasi wake aliyemuuliza kuhusiana na kundi lililomtukana ‘Umar bin Khattab, Sahaba wa Mtume (s.a.w) na Aisha, mke wa Mtume (s.a.w), amelaani vikali kitendo hicho na kukitaja kuwa ni kinyume na maadili na mwenendo wa Ahlul-Bayt (a.s.).
Ayatullah al-‘Udhma Makarem Shirazi:
“Hakupaswi kufanya dharau ndogo hata moja dhidi ya matakatifu ya Ahlus-Sunna,” pia katika barua yake kwa Sheikh al-Azhar ameeleza kuwa Mar'aji‘ wote na baadhi ya wanazuoni wa Kishia wanajiepusha na matusi na maneno mabaya dhidi ya baadhi ya Masahaba.
Ayatullah al-‘Udhma Wahid Khorasani:
Katika darsa yake ya fiqhi, amekataa kutoheshimu makhalifa wa Ahlus-Sunna na akawaomba wanafunzi wake kujiepusha na matusi na dharau dhidi ya makhalifa wa Kisunni.
Katika sehemu nyingine amesema: “Haifai kuwa na uadui na wafuasi wa madhehebu mengine na wala kutusi matakatifu yao; kuwalaani na kuwatukana wakubwa wao si jambo halali, kwani jambo hilo linawaweka mbali na Ahlul-Bayt pamoja na elimu zao.”
Ayatullah al-‘Udhma Jawadi Amuli:
Katika ujumbe wake kwa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu amesema: “Kudharau matakatifu ya Kishia au Kisunni, ni dharau na udhalilishaji wa kinyama dhidi ya imani na itikadi ya pande zote mbili, ni haramu, na kuchochea mifarakano na kuhatarisha mshikamano wa umma wa Kiislamu na ni dhambi kubwa.”
Ayatullah al-‘Udhma Nuri Hamedani, Ayatullah al-‘Udhma Alavi Gurgani na Ayatullah al-‘Udhma Hashimi Shahrudi; pia wamesema kuwa, kutusi makhalifa na matakatifu ya Ahlus-Sunna si jambo halali.
Vilevile Ayatullah Madani Tabrizi, amekataza kutusi matakatifu ya dini yeyote ya mbinguni, hususan madhehebu ya dini tukufu ya Uislamu, na amesema kuwa; kila kitendo kinachosababisha mgawanyiko miongoni mwa umma mkubwa wa Kiislamu na kuleta hasara za mali au roho kwa Waislamu ni haramu na ni kinyume cha sheria ya Kiislamu.
Vyanzo:
Tovuti rasmi ya khamenei.ir
Tovuti ya habari ya Hawzah
Tovuti ya Porsman Daneshjuyi
Maoni yako