Jumamosi 30 Agosti 2025 - 17:11
Vikosi vya Marekani kuondoka Makao ya Operesheni za Pamoja Baghdad

Hawzah/ Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbali mbali, katika utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili kati ya nchi hizo mbili, inatarajiwa kuwa vikosi vya Marekani siku ya Jumamosi vitaanza kuondoka mjini Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, vyanzo mbali mbali kwenye vyombo vya habari vimeripoti kuwa, katika utekelezaji wa makubaliano hayo, vikosi vya Marekani vitaanza kuondoka Baghdad siku ya Jumamosi.

Vyanzo hivyo pia siku ya Ijumaa vilibainisha kwamba vikosi vya Marekani vitaondoka katika Eneo la Kijani lenye ulinzi mkali ambalo linajumuisha vituo vya kidiplomasia vya Magharibi, makao ya serikali rasmi, pamoja na uwanja wa ndege wa Baghdad na makao ya amri ya operesheni za pamoja.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyoafikiwa mwaka uliopita (2024) baina ya pande za Iraq na Marekani, inatarajiwa Marekani itaendelea kuweka sehemu ya wanajeshi wake kwa mwaka mmoja zaidi katika eneo la Kurdistan.

Serikali ya Iraq imethibitisha mara kadhaa kwamba awamu ya kwanza ya kuondoka kwa vikosi vya Marekani, ambavyo vipo katika muktadha wa muungano wa kimataifa dhidi ya Daesh, itakamilika Septemba 2025, huku awamu ya pili ikitarajiwa kukamilika mwaka 2026.

Ni vyema kutambua kuwa takriban wanajeshi 2,500 wa Marekani bado wapo Iraq kama sehemu ya muungano huo, na idadi yao ilipungua baada ya kushindwa kwa Daesh nchini humo mwaka 2017.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha