Jumapili 31 Agosti 2025 - 00:40
Waziri Mkuu wa Lebanon amuomba Sheikhul-Azhar kuzuru Lebanon

Hawzah/ Ofisi ya habari ya Nawaf Salam, Waziri Mkuu wa Lebanon, imeripoti kwamba yeye pamoja na ujumbe wake wakiwa mjini Cairo walikutana na Ahmad al-Tayyib, Sheikhul-Azhar

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, katika mkutano huo Waziri Mkuu wa Lebanon alimuweka Sheikhul-Azhar katika hali ya kufahamu maendeleo ya karibuni nchini Lebanon na kusisitiza kwamba Lebanon, kwa muundo wake wa aina mbalimbali za Waislamu na Wakristo, inahitaji msaada wa Azhar katika kuimarisha roho ya udugu na uvumilivu wa kibinadamu, na katika kukabiliana na hotuba za uchochezi wa mgawanyiko na upendeleo wa kidini.

Katika muktadha huo, Nawaf Salam alimualika Sheikhul-Azhar kutembelea Lebanon kabla ya mwisho wa mwaka huu wa Miladia, akisisitiza kwamba uwepo wake jijini Beirut utakuwa ujumbe wa mshikamano kwa Walebanoni wote na utaakisi nafasi ya kihistoria ya Azhar katika kueneza utamaduni wa mazungumzo na maelewano ya pamoja.

Kwa upande mwingine, Sheikhul-Azhar alilipokea vyema ombi hilo na alipendekeza kwamba ziara yake ijayo nchini Lebanon ifanyike sambamba na mkutano wa Kiislamu utakaofanyika Beirut kwa ajili ya kuthibitisha misingi ya hati ya udugu wa kibinadamu na uraia, ambayo inathibitisha utamaduni wa kuvumiliana, amani na maisha ya pamoja.

Aidha, alisisitiza juu ya kujitolea kwa Azhar katika kutekeleza nafasi yake ya kimataifa ya kupambana na misimamo mikali na juhudi za kueneza utamaduni wa wastani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha