Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maudhui kamili ya ujumbe wa Mtukufu Ayatollah Makarim Shirazi ni kama ifuatavyo:
Bismillāh-ir-Rahmān-ir-Rahīm
«وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِی آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِی الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُمْ مِنَ الطَّیِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَی كَثِیرٍ مِمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِیلًا»
Kwa kuanza hotuba yangu, ninaona ni wajibu kulaani mashambulizi ya kikatili na kinyume cha sheria la utawala wa Kizayuni na Marekani dhalimu dhidi ya nchi yetu pendwa, aidha, nawapa mkono wa rambirambi familia za mashahidi wa hujuma hii, vilevile, nawashukuru kwa dhati waandaaji na washiriki wote wa mkutano huu adhimu na natumaini kuwa kikao hiki cha kielimu kitakuwa hatua muhimu katika kurejesha haki halisi za mwanadamu.
Kwa mtazamo wa dini za mbinguni, na hasa Uislamu, “mwanadamu” ni kiumbe mwenye heshima na utukufu. Hata hivyo, kiumbe huyu mtukufu anapopotoka kutoka kwenye njia ya maumbile na uadilifu na akaanza kukiuka haki, basi Mwenyezi Mungu humuita dhalimu mno (ظلوم).
Kwa miaka mingi sasa, dhana tukufu ya “haki za binadamu” imegeuzwa kuwa kichekesho na chombo cha unyonyaji mikononi mwa madola dhalimu na ya kihalifu, kwa kivuli cha maneno haya mazuri, wamefuatilia maslahi yao haramu na kwa kisingizio hicho wamefanya dhuluma kubwa zaidi dhidi ya mataifa na jamii bila hata kuwaheshimu binadamu au kushikamana na haki zao, ushahidi bora wa hili ni hali ya leo ya ukanda wetu.
Katika mwaka uliopita, watu wote duniani walishuhudia jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza, maelfu ya wanawake, watoto na watu wasio na hatia waliuawa au kufukuzwa kwenye nyumba zao kwa sababu ya ukatili uliofanywa na utawala huo wa Kizayuni – utawala ambao wenyewe ni zao la fikra za kikoloni na za kiuadui wa binadamu wa Magharibi.
Pia hatupaswi kusahau jinai zilizotokea hivi karibuni dhidi ya nchi yetu ya Kiislamu ambapo watu wasio na hatia waliuawa kikatili majumbani mwao, Je, hawa wanyonge hawakuwa na haki ya msingi kama haki ya uhai na usalama? Je, walikuwapo kwenye uwanja upi wa vita?!
Kwa uwazi kabisa, lazima tuseme kuwa mtazamo wa Magharibi juu ya mwanadamu na haki zake ni wa kimaslahi na wa kuchagua kwa upendeleo, kila inapokuwa hakuna maslahi yao au tamaa ya kutawala, hutoa kauli nzuri kuhusu haki za binadamu, lakini pindi tu maslahi yao yanapohusika, mhanga wa kwanza huwa ni haki za binadamu zenyewe.
Kamwe tusikubali kudanganywa na kauli za kupendeza za Magharibi, haki za binadamu wanazodai ni dhana tupu isiyo na msingi, hawana imani na heshima ya mwanadamu wala hawazingatii misingi wanayoidai kwa maneno.
Nasaha yangu kwa wataalamu wote waliopo kwenye uwanja huu ni kwamba, kwa mwangaza wa elimu na kufichua ukweli, waonyeshe sura halisi ya wanaodai uongo kuwa ni watetezi wa haki za binadamu mbele ya fikra za umma duniani, na wasiruhusu dhana hii tukufu ipotoshwe na kuharibiwa na wale wanaozivunja kwa vitendo.
Mwisho wa ujumbe wangu, ninatangaza chuki na kuchukizwa kwangu na jinai zisizo na haya zinazofanywa na utawala huu wa bandia na waungaji mkono wake wa Kimagharibi, hasa serikali ya Marekani, ninatoa rambirambi kwa ajili ya mashahidi wa watu wanyonge wa eneo hili, hasa ndugu zetu Waislamu waliouawa na utawala wa Kizayuni wa kimataifa na wale wanaouunga mkono, vilevile, nawapongeza watu wa muqawama na vikosi vya kijeshi kwa sababu ya kusimama kwao na kujitetea mbele ya wavamizi. Ninamuomba Mwenyezi Mungu aupe Umma wa Kiislamu usalama wa kudumu na ushindi kamili na wa mwisho kwa wanyonge duniani kote dhidi ya madhalimu na mabeberu.
Wassalamu ‘alaykum wa rahmatullah
Qom – Nāsir Makarim Shirazi
Maoni yako