Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika siku za mwanzo za wiki hii, viongozi wa Uingereza walielezea mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ghaza kuwa jambo la kushangaza na la kusikitisha. Hata hivyo, kwa waandamanaji wanaopinga mauaji ya halaiki na jinai za Israel, kauli hizi hazitoshi! Wao wanataka Israel kuacha kabisa kupiga mabomu kwenye mahospitali, shule, na makazi ya watu wasio na hatia.
Katika muktadha huo, kwa uratibu wa makundi yanayofanya kazi katika sekta ya misaada ya kibinadamu na pia kampeni ya kushikamana na Palestina, maandamano makubwa na ya amani yaliandaliwa nchini Uingereza, na maelfu ya watu walihudhuria.
Maandamano hayo yalikuwa ni tamko rasmi la kulaani Israel. Pamoja na hayo yote, Uingereza bado inaendelea kupitisha sheria za kuuza silaha kwa Israel dhalimu. Moja ya vibali hivyo ni mauzo ya vipuri vya ndege ya kivita aina ya F-35 kwa Israel. Bw. John Rees, ambaye ni mwandishi wa habari na mwanaharakati wa kisiasa, alisema: "Waziri Mkuu amepoteza nchi na watu wake kwa sababu ya suala la Palestina. Kabla ya matamko haya, nilijua kwamba viongozi wa nchi ni wanafiki na waongo, lakini sasa kila mtu amethibitisha hivyo."
Kampeni ya Kushikamana na Palestina pia ilisisitiza kwamba: "Lazima tuitake serikali yetu iache kushiriki katika jinai za Israel."
Maoni yako