Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Muhammad Hassan Jafari, Imamu wa Ijumaa wa mji wa Skardu Baltistan, Pakistan, kutikana na mnasaba wa kuwadia Wiki ya Umoja alitoa ujumbe wake, sambamba na kutoa pengezi kwenye siku hizi tukufu kwa Umma wa Kiislamu, alisisitiza kwamba njia pekee ya kuondokana na matatizo na njama za maadui ni kushikamana na umoja na mshikamano.
Matini ya ujumbe huu ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرحمن الرحیم
Alhamdu lillahi Rabbil-‘alamin, na rehema na amani zimshukie Bwana wa Manabii na Mitume, Muhammad na Ahlul-Bayt wake watoharifu pamoja na maswahaba wake wateule wote.
Wiki ya Umoja ambayo hufanyika kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul-Awwal, kwa hakika ni dhihirisho la umoja na undugu wa Umma wa Kiislamu. Katika siku hizi tukufu, Waislamu duniani wanasherehekea kuzaliwa Mtume Mtukufu, Bwana Muhammad Mustafa (saw) kwa mapenzi na utii, na wanafanya ahadi ya kuufanya mwenendo wake wenye nuru kuwa dira ya maisha yao binafsi na kijamii.
Imam Khomeini (r.a.) kwa ubunifu wa kutangaza Wiki ya Umoja, alipeleka ujumbe wa wazi kwa Umma wa Kiislamu kwamba Waislamu wanapaswa kuepukana na tofauti za kimadhehebu na kufarakana, na kurejea kwenye roho halisi ya Uislamu, yaani undugu, udugu na mshikamano. Qur’ani Tukufu inatoa amri kwa uwazi:
«وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِیعًا وَلَا تَفَرَّقُوا»
“Shikamaneni nyote kwa kamba ya Mwenyezi Mungu, wala msifarakane.”
(Aali Imran: 103)
Imamu wa Ijumaa wa Skardu aliendelea kubainisha: Leo Umma wa Kiislamu unakabiliwa na changamoto kubwa kama vile kudhulumiwa kwa watu wa Palestina na mataifa mengine yaliyo chini ya dhulma, kadhia ya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia), na njama za kikoloni, bila shaka, suluhisho la matatizo haya ni umoja na mshikamano wa Waislamu, ikiwa Umma wa Kiislamu utasimama pamoja kama ndugu, hakuna nguvu yoyote itakayoweza kuwadhoofisha.
Aidha aliwataka wananchi wa Pakistan, hususan watu wema wa Gilgit-Baltistan, kuadhimisha Wiki ya Umoja si kwa kuiona tu kama tukio la kidini, bali kama fursa ya kuimarisha mshikamano wa Waislamu, Alihimiza kwamba kwa kupitia kufanya mipango na mikutano ya kuleta mshikamano katika misikiti, shule na mikusanyiko, mazingira ya kuleta ukaribu wa nyoyo yawekwe.
Mwishoni mwa ujumbe alisema: Namwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atupatie sisi sote tawfiki ya kuhudumia Uislamu na Waislamu, utukufu na hadhi ya Umma wa Kiislamu, maendeleo na ustawi wa Pakistan, na msaada kwa wanyonge na wanaonyanyaswa, Amin, ya Rabbal-‘alamin.
Wassalamu ‘alaykum
Sheikh Muhammad Hassan Jafari, Imamu wa Ijumaa wa mji wa Skardu Baltistan, Pakistan
Maoni yako