Kwa mujibu wa idara ya kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, katika mkutano wa kwanza wa maandalizi ya kongamano la kimataifa la ulinganizi mpya wa dini uliofanyika nchini Georgia, mada kuu ya majadiliano na kubadilishana fikra baina ya washiriki ilikuwa ni “Ulinganizi mpya na athari zake katika kulinda na kuimarisha taasisi ya familia”. Tukio hili limefanyika sambamba na mwezi mtukufu wa Rabiul-Awwal na katika siku za karibu na furaha ya kuzaliwa Mtume mtukufu wa Uislamu, Bwana Muhammad (saw), huku kikihudhuriwa na shakhsia mashuhuri katika uwanja wa ulinganizi wa kidini na kitamaduni, wakiwemo Hujjatul-Islam wal-Muslimin Husseini Nishaburi, rais wa Kituo cha Kimataifa cha Qur’ani na Ulinganizi cha Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu, manaibu wa Idara ya Waislamu wa Georgia na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake Waislamu ya nchi hiyo.
Katika kikao hiki, umuhimu wa ulinganizi mpya wa dini kwa kuzingatia nafasi ya familia na jukumu lake katika kulinda misingi ya kijamii ulijadiliwa, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Husseini Nishaburi, sambamba na kushukuru msaada wa Ubalozi wa Kitamaduni wa Iran na jitihada mahsusi za Bwana Ramin Ighdaf pamoja na Jumuiya ya Wanawake Waislamu wa Georgia, alieleza tofauti ya mtazamo wa Uislamu na Magharibi katika dhana ya mwanadamu, alisisitiza kuwa mtazamo wa Magharibi kuhusu mwanadamu hauna chanzo wala hatima iliyo wazi, ilhali mtazamo wa Kiislamu unamchukulia mwanadamu kama kiumbe kinachomkubali Mungu na khalifa wake duniani, aliyeumbwa kwa lengo na maana mahsusi.
Rais wa Kituo cha Kimataifa cha Qur’ani na Ulinganizi, akirejea katika mafundisho ya Ayatullah Jawadi Amuli, alikumbusha dhana ya “Inna lillahi wa inna ilayhi raji‘un”, na akafafanua kuwa Uislamu kwa msingi wa akili na kiroho, unaitambua familia kama taasisi takatifu, aliitambulisha familia kuwa ndiyo mazingira bora zaidi kwa kukuza vipawa na msingi muhimu zaidi wa kulinda jamii, na akasisitiza kwamba ulinganizi wa dini katika mitandao wa kijamii ni njia mpya na ya lazima katika kuimarisha misingi ya familia.
Katika muktadha huu, tovuti mbili maalumu katika uga wa ulinganizi wa kidini na familia zenye majina ya Ailemiz.niz na Dinimiz.net zilibuniwa na kuzinduliwa, tovuti hizi zimeundwa kwa lugha ya Kiazari kwa lengo la kueneza misingi ya Kiislamu na kuinua uelewa wa kidini.
Bwana Ramin Ighdaf, aliyekuwa rais wa zamani wa Idara ya Waislamu wa Georgia na mbunifu na mtoaji maudhui ya tovuti hizi, katika hotuba yake aligusia mipango ya Kimagharibi chini ya jina la “usawa wa kijinsia” na madhara yake mabaya kwa misingi ya familia za Kiislamu. Alionya kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali na programu za kielimu zinazojengwa juu ya thamani za Kimagharibi kama vile ufeministi na kuchelewesha ndoa, zinahesabiwa kuwa tishio kubwa kwa taasisi ya familia na utamaduni wa kitaifa.
Mkutano huu wa maandalizi, ambao umefanyika kama utangulizi wa kongamano la kimataifa la ulinganizi mpya wa dini, umehesabiwa kuwa hatua muhimu katika mshikamano na uratibu wa wahusika wa ulinganizi wa kidini na kitamaduni kwa ajili ya kulinda na kuimarisha taasisi ya familia katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ni vyema kueleza kwamba kongamano la kwanza la kimataifa la ulinganizi mpya wa dini litafanyika katika mwezi wa Dey wa mwaka huu kupitia anuani ya IFPNR.IR.
Maoni yako