Ijumaa 23 Mei 2025 - 00:15
Akili Mnembe na Tahaddi (Changamoto)

Muujiza wa Qur'ani hauishii tu katika vipengele kama maudhui, mpangilio, ufasaha na balagha, au kutokuwapo kwa hitilafu, bali una vipengele vingine vya kimiujiza kama vile muujiza wa kielimu na habari za ghaibu kuhusu yaliyopita na yajayo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika enzi ya akili Mnembe, maswali mengi yameibuka kuhusu masuala mbalimbali ya kidini katika kukabiliana na akili Mnembe. Miongoni mwa maswali hayo ni kuhusu changamoto ya Qur'ani (tahaddi) na akili Mnembe, ambapo wataalamu wa Kituo cha Kitaifa cha Kujibu Maswali ya Kidini wamejibu maswali hayo, fuatana nasi kwa swali na jibu hilo.

Swali:

Kwa kuzingatia kuwa akili Mnemba imetengenezwa na mwanadamu, je, ikitokea kwamba akili mnemba italeta kitabu kama Qur'ani au sura kama za Qur'ani, je hilo litakuwa jibu kwa changamoto (tahaddi) ya Qur'ani na kulingana nayo? Je, Qur'ani itakoma kuwa muujiza na ya kimungu? Na ikiwa hivyo, Qur'ani itakuwaje bado iwe kitabu cha mwisho cha kimungu na chanzo cha uongofu na furaha ya wanadamu hadi Siku ya Kiyama?

Jibu:

Utangulizi

Qur'ani Tukufu imewalingania wale wanaokanusha kuwa Qur'ani ni ya kimungu kuleta sura kama za Qur'ani. Ulingano huu unajulikana kwa jina la "tahaddi", na lengo lake ni kuthibitisha kuwa Qur'ani ni muujiza na ni ya kimungu. Sasa swali ni hili: ikiwa akili mnemba italeta sura kama za Qur'ani, je hili litakuwa jibu kwa tahaddi ya Qur'ani na kuonesha kuwa Qur'ani si muujiza wala si ya kimungu?

Maudhui ya jibu:

Akili mnemba

Akili mnemba, kwa ujumla, ni uwezo wa mfumo au mashine kuiga utendaji wa kiakili wa mwanadamu kama vile kujifunza, kuhoji, kutatua matatizo, kuelewa lugha asili, kutambua mifumo na kufanya maamuzi. Akili hii inalenga kuwafanya mashine ziweze kutekeleza kazi ambazo kwa sasa zinahitaji akili ya kibinadamu. Kuna aina mbalimbali za akili mnemba, kila moja ikiwa imeundwa kwa ajili ya matumizi maalumu. Baadhi ya aina zake humuwezesha mashine kujifunza kwa kutumia data na kutambua mifumo bila ya kuwekewa mipango mahususi, na kutekeleza majukumu tata.

Walengwa wa tahaddi

Allah katika aya tano za Qur'ani Tukufu amewaita wale wanaokanusha kuwa Qur'ani ni ya kimungu kuingia vitani na kuleta mfano wake. Amesema: Je, si nyinyi mnadai kuwa Qur'ani si ya kimungu? (1) Mtume ameibuni kutoka kwake mwenyewe? (2) Hivyo basi, nanyi pia mnaweza kuleta mfano wake. (3) Basi msitosheke kwa maneno, bali wekeni madai yenu katika vitendo, na leteni Qur'ani kama hii, au hata sura kumi, au angalau sura moja tu inayofanana na sura zake.

Kulingana na aya ya 88 ya Suratu al-Isra', lau majini na watu wakikusanyika pamoja na kusaidiana, hawataweza kuleta mfano wa Qur'ani hii. Katika aya ya 38 ya Suratu Yunus, wapinzani wa uungu wa Qur'ani wameambiwa wamwite yeyote asiyekuwa Allah mwezaye kuwasaidia kuleta sura kama za Qur'ani. Changamoto kama hiyo inarudiwa pia katika aya ya 23 ya Suratu al-Baqara na aya ya 13 ya Suratu Hud, ambapo wanaambiwa watake msaada kwa yeyote asiyekuwa Mungu; na katika Suratu Hud imeelezwa kuwa tahaddi ni ya sura kumi badala ya moja. Kwa kuwa tahaddi bado ipo, na tamko la "من دون الله" linajumuisha kila kitu, basi hata akili mnemba imo ndani ya tahaddi hiyo.

Uwezekano wa akili mnemba kujibu tahaddi ya Qur'ani

Akili mnemba ina kasi kubwa ya kuchakata taarifa na inaweza kuchakata kiasi kikubwa sana cha data kwa muda mfupi na kwa usahihi wa hali ya juu, jambo linalopunguza makosa na kuongeza ufanisi. Hata hivyo, bado ina mapungufu na vizingiti vikubwa katika masuala kama ubunifu wa kipekee, hoja ya kiakili, uelewa wa hisia za kibinadamu na mengineyo na haya yote bado ni duni hata kulinganisha na akili ya binadamu.

Zaidi ya hayo, muujiza wa Qur'ani hauishii tu katika vipengele kama maudhui, mpangilio, ufasaha, balagha, kutokuwa na hitilafu, athari za kiroho na uwezo wake wa kuwaongoza watu, bali una vipengele vingine vya kimiujiza kama vile muujiza wa kielimu na habari za ghaibu kuhusu yaliyopita na yajayo ambavyo akili mnemba haiwezi kuvigezea.

Jambo jingine ni kwamba maana ya "mfano wa Qur'ani" si kwamba mtu aige Qur'ani na kuleta sura inayofanana nayo kwa nje tu, bali sura itakayowasilishwa kama jibu kwa tahaddi ya Qur'ani ni lazima iwe, pamoja na kuwa na uzito kama Qur'ani, ni ya kipekee na huru kabisa isiyokuwa na uhusiano na Qur'ani.

La muhimu zaidi ni kwamba, kwa kuzingatia uhusiano kati ya kiumbe na Muumba, ikiwa Qur'ani ni ya kimungu basi hakuna chanzo kingine kinachoweza kuleta mfano wake; kwa kuwa hakuna kiumbe yeyote aliye kama Allah, ili kile anachokileta kiwe kama kile kilicholetwa na Allah.

Tija ya maelezo

Akili mnemba inaweza kuchambua mifumo ya lugha ya Qur'ani na kutunga maandishi mapya yanayofanana nayo kwa nje, lakini hatupaswi kusahau kwamba tahaddi ya Qur'ani kwa binadamu ni zaidi ya kuunda maandishi yanayofanana kimuundo. Muujiza wa Qur'ani uko katika ukweli wa ndani wa maudhui na roho ya kimungu ndani yake ambayo hayawezi kufikiwa na zana au uwezo wa kibinadamu kama akili mnemba. Sifa hizi ndizo zinazolifanya Qur'ani kuwa kitabu cha uongofu hadi Siku ya Kiyama.

Kwa maelezo zaidi:

Najjarzadegan, Fathollah, "Tahlil-e Hamānandnapaziri (I‘jaz) Qur’an dar Amuzeh'a-ye Qur’an wa Sunnat", Tehran, Samt, chapa ya kwanza, 1397 H.Sh.

Vyanzo:

1. Sura al-Muddaththir, aya 24 na 25.
2. Sura an-Nahl, aya 103; Sura at-Tur, aya 33 na 34.
3. Sura al-Anfal, aya 31.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha