Jumatano 29 Oktoba 2025 - 16:03
Uenezaji wa Dini (Tabligh) Katika Zama za Akili Bandia (AI); Je, Mimbari ya Jadi Bado ina Ufanisi?

Hawzah/ Hujjatul Islam wal-Muslimin Sharifi amesema: Leo kuna programu ambazo zinawezesha "mazungumzo na hadithi" au "mazungumzo na tafsiri". Mhubiri anaweza kutumia mifumo hii kupata rasilimali pana na za kuaminika katika kila mada.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, katika zama za kidijitali, mipaka kati ya elimu, mawasiliano na uenezaji wa dini imebadilika; akili bandia kama mojawapo ya mafanikio muhimu ya teknolojia, sasa ina jukumu la kuamua katika uzalishaji wa maudhui na uwasilishaji wa ujumbe wa kidini. Hata hivyo, je, mimbari ya jadi bado ina ufanisi na ina athari?

Kuhusiana na hili, tulifanya mazungumzo na Hujjatul Islam wal-Muslimin Ahmad Hussein Sharifi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Qom, mahojiano yenyewe ni kama ifuatavyo:

Katika miaka ya hivi karibuni, akili bandia imekuwa mojawapo ya matukio ya kuamua katika anga ya kidijitali. Kwa mtazamo wako, kuingia kwa teknolojia hii katika uwanja wa uenezaji wa dini kunaweza kuwa na athari gani?

Jawabu

Ukweli ni kwamba akili bandia imeleta mabadiliko makubwa katika namna ya kuielewa jamii na kuzichambua tabia za hadhira. Zamani, tulitumia zana kama vile dodoso na mahojiano ya ana kwa ana kwa ajili ya uchunguzi wa maoni na kuelewa masuala ya watu, lakini leo chanzo kilicho wazi zaidi na sahihi zaidi ili kuielewa jamii ni data zinazotokana na uchambuzi wa akili bandia na data za kidijitali.

Kwa mfano, kituo cha tabligh cha Hawzah kinaweza, kwa kuchunguza tabia za watumiaji wa mtandao, injini za utafutaji na mitandao ya kijamii, kufikia uelewa wa kina wa hali ya kiakili na mahitaji ya watu katika kila eneo. Data hizi zinaonesha kwamba katika kila mji au kundi kuanzia vijana hadi watu wazima, ni masuala gani yanawatatiza, watu wanafikiria zaidi kuhusu mada gani na wanatafuta maudhui gani. Taarifa kama hizi ni za thamani kubwa kwa ajili ya kupanga mikakati ya tabligh.

Umeashiria kuwa data hizi zinaweza kubadilisha mwelekeo wa tabligh. Je, akili bandia inaweza kuwa chombo chenye ufanisi katika mchakato wa tablighi yenyewe?

Jawabu

Ndiyo, hasa hivyo. Akili bandia si kwa ajili ya kuwachambua hadhira tu, bali pia ni chombo chenye nguvu kwa mhubiri (Muballigh) mwenyewe. Leo kuna programu ambazo zinawezesha "mazungumzo na hadithi" au "mazungumzo na tafsiri". Mhubiri anaweza kutumia mifumo hii kupata rasilimali pana na za kuaminika katika kila mada, na kwa muda mfupi zaidi kufikia uelewa wa kina na sahihi zaidi kwa mada husika.

Hii inamfanya mhubiri kuepuka mtazamo wa upande mmoja katika uwasilishaji wa maudhui; yaani, kwa mfano, asione hadithi moja pekee, bali aweze kuchambua uhusiano wake na hadithi na tafsiri nyingine nyingi. Jambo hili linaongeza ubora wa kielimu na kina cha maudhui ya uenezaji.

Je, tunaweza kusema kwamba akili bandia sambamba na mimbari za jadi, vimefungua njia mpya kwa ajili ya uenezaji wa dini?

Jawabu

Ndiyo, mimbari ya jadi bado ina nafasi yake maalum na baraka zake na inapaswa kuhifadhiwa. Lakini sambamba na hiyo, mimbari za kidijitali na za mtandaoni zimeibuka ambazo hadhira yake ni kubwa zaidi, tofauti zaidi na yenye akili zaidi. Maneno yanayochapishwa katika mtandao si tu yanadumu kwa vizazi bali pia yanakuwa ya kimataifa; watu kutoka duniani kote wanaweza kuyaona na kunufaika nayo.

Kwa sababu hiyo, mimbari kama hiyo inahitaji utafiti wa kina zaidi, umakini zaidi na mtazamo wa kimataifa kutoka kwa mhubiri. Uenezaji katika mtandao si tu kuwasilisha ujumbe, bali ni aina ya mazungumzo na hadhira ya kimataifa.

Moja ya changamoto kwa wahubiri (Muballighina) katika uwanja wa kimataifa ni kizuizi cha lugha. Akili bandia inaweza kutoa msaada gani katika eneo hili?

Jawabu

Hii ni mojawapo ya baraka kubwa za akili bandia. Leo zana za tafsiri zinazotegemea akili bandia zimeendelea sana kiasi kwamba mtu anaweza, kwa kuzungumza tu kwa lugha ya Kifarsi, kuwasilisha ujumbe na fikra za Kiislamu au dhana za Mapinduzi ya Kiislamu kwa lugha kadhaa hai duniani, bila yeye mwenyewe kuwa na ujuzi wa lugha hizo. Akili bandia hutoa tafsiri laini na sahihi na hii ina maana ya kuenea kwa haraka na kwa upana ujumbe wa Uislamu na Mapinduzi katika pembe zote za dunia.

Kwa ujumla, unalitathmini vipi jukumu la teknolojia hii katika siku zijazo kwenye uenezaji wa dini?

Jawabu

Akili bandia si tu chombo cha kusaidia, bali ni jukwaa kuu kwa ajili ya mabadiliko ya uenezaji wa dini katika dunia ya kisasa. Kuanzia uchambuzi wa hadhira hadi uzalishaji wa maudhui, tafsiri, na hata mwingiliano na watumiaji katika mtandao, yote haya leo yako kwenye kuwahubiria waumini wa dini. Matumizi ya akili ya teknolojia hii yanaweza kusababisha uenezaji wa kina zaidi, uwasilishaji sahihi zaidi wa ujumbe na kuanzisha mawasiliano ya kimataifa kati ya fikra za kidini na mwanadamu wa kisasa. Ujio wa akili bandia katika skta ya tabligh ni fursa ya kihistoria ambayo haipaswi kupuuzwa.

Mwisho wa ujumbe

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha