Jumanne 28 Oktoba 2025 - 14:13
Kutoka mafunzo ya biashara hadi utoaji wa mikopo midogo kwa wanawake wasio na waume

Hawza/ Runinga ya Al-Masirah imeonesha uzoefu wa Taasisi ya Maendeleo Khayrat al-‘Atā’, ambayo imegeuka kutoka mpango wa kujitolea wa wanawake wachache hadi kuwa taasisi inayoongoza katika uzalishaji, ikithibitisha uwepo wa wanawake wa Kiyemeni katika uwanja wa maendeleo na kujitegemea chini ya kaulimbiu: “Kutoka katika msaada hadi maendeleo… na kutoka katika uhitaji hadi uzalishaji.”

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika mazingira ya vita na kuzingirwa, watu wa Yemen daima wamesimama imara kwa kujitoa kwao — si tu katika kulinda uhuru na nchi yao dhidi ya mhimili wa uovu wa Magharibi, Waarabu na Uzayuni — bali pia katika wakati ambao serikali nyingi za Kiarabu zimewaacha Wapalestina, watu wa Yemen hawakuacha kuisaidia Palestina. Wameendelea kuwatetea Wapalestina kwa njia mbalimbali — kiuchumi, kisiasa na kijeshi — katika bara na baharini.

Nafasi ya pekee ya wanawake wa Yemen

Wanawake wa Yemen wamekuwa na nafasi maalumu katika mapambano haya. Wakiwa bado na jukumu la uzazi, wamebeba pia majukumu mazito ya familia kutokana na kutokuwepo waume, watoto au ndugu zao walioko mstari wa mbele au waliouawa kishahidi.

Mwanamke wa Kiyemeni, kwa kusimama imara mbele ya matatizo, amelipa gharama kubwa kwa vita vilivyoiharibu nchi yao. Baada ya kupoteza mume, mwana au jamaa, amejikuta akibeba mzigo maradufu, akiwa ameachwa peke yake katikati ya kuporomoka kwa huduma za msingi na ukosefu wa mahitaji ya lazima kwa maisha bora. Mkate, maji na umeme havichukuliwi tena kama vitu vya kawaida; vimekuwa vitu vya anasa visivyopatikana.

Ujasiri na uthabiti wa wanawake wa Yemen

Hata hivyo, licha ya mazingira haya magumu, wanawake wa Yemen hawajanyamaza wala kukata tamaa; wamekabiliana na maisha kwa ujasiri, wakapambana na hali ngumu na kuthibitisha uwezo wao katika bidii na ubunifu. Mwanamke wa Kiyemeni anaonekana katika sura mbalimbali — akiwa mama anayewalea watoto wake, au mfanyabiashara anayetafuta riziki yake, au mwalimu anayewasha taa za elimu, au daktari anayepooza maumivu, au mwandishi wa habari anayeeneza ukweli, au mwanaharakati anayepigania amani na haki, au askari polisi anayelinda usalama na kuihudumia jamii.

Runinga ya Al-Masirah ilionesha tena uzoefu wa Taasisi ya Maendeleo Khayrat al-‘Atā’, ambayo kutoka katika mpango wa kujitolea wa wanawake wachache, imekuwa taasisi inayoongoza katika uzalishaji, ikiimarisha ushiriki wa wanawake wa Yemen katika maendeleo na kujitegemea, chini ya kaulimbiu: “Kutoka katika msaada hadi maendeleo… na kutoka katika uhitaji hadi uzalishaji.”

Kuhusu taasisi ya Khayrat al-‘Atā’

Taasisi hii ilianzishwa mwaka 2018, wakati wa mzingiro na uvamizi, kama mpango wa kuwahamasisha wanawake kujifunza na kupata ujuzi wa kujitegemea kwa kujibu mahitaji ya jamii. Baadaye ilipanuka na kuwa kituo cha elimu, kisha kuwa taasisi kamili ya maendeleo yenye viwanda vidogo vya uzalishaji na miradi midogo inayotoa mikopo yenye riba ndogo kwa familia maskini na familia za mashahidi.

Katika kipindi cha shughuli zake, taasisi hii imeweza kuwapa mafunzo na ujuzi mamia ya wanawake katika nyanja za ushonaji, urembo wa vitambaa (embroidery), uchakataji wa bidhaa za chakula, pamoja na utengenezaji wa manukato na uturi. Wanawake wengi wameweza kuanzisha biashara zao binafsi na kuboresha hali ya maisha ya familia zao.

Uwekezaji kwa ajili ya mustakabali wa jamii

Katika muktadha huo, Bi. Shadha Abdulhamid al-Mu’ayyad — afisa wa mahusiano ya umma na vyombo vya habari wa Taasisi ya Maendeleo Khayrat al-‘Atā’ — alieleza kuwa taasisi hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii kupitia elimu na kuwapa stadi, ikiwaruhusu kutoka katika kundi la wapokeaji wa misaada na kuwafanya kuwa wazalishaji wanaochangia katika uchumi wa taifa.

Katika mahojiano yake na kipindi “Dirisha la Misaada ya Kijamii” kinachorushwa na runinga ya Al-Masirah, al-Mu’ayyad alibainisha kuwa taasisi hiyo inatekeleza programu kadhaa kuu, zikiwemo: Mpango wa Al-Khayrat, wa kusaidia familia zinazozalisha kupitia mikopo midogo, Mpango wa Surāt al-Khayrat, wa kutoa misaada ya kifedha na isiyo ya kifedha kwa familia maskini, kwa lengo la kuzibadilisha ziwe familia zinazojitegemea na Mpango wa Ujenzi wa Uwezo (Capacity Building) unaolenga kutoa mafunzo ya ushonaji, urembo wa vitambaa, uchakataji wa chakula na ufundi wa mikono.

Hadithi ya mama wa shahidi aliyefanikiwa

Bi. al-Mu’ayyad pia aligusia hadithi za mafanikio zinazotia moyo za wanawake waliotoka sifuri hadi kujitegemea. Miongoni mwao ni mama wa shahidi ambaye, baada ya kupokea mkopo mdogo, aliweza kufungua bufe shuleni na hivyo kupata chanzo thabiti cha kipato kwa ajili ya familia yake. Akasema kwamba simulizi kama hizi ndizo zinazoakisi kwa vitendo dhamira ya taasisi hiyo — kubadilisha magumu ya maisha kuwa fursa halisi na zenye tija.

Al-Mu’ayyad kuhusu changamoto za ufadhili, malengo makubwa na mipango ya maendeleo

Al-Mu’ayyad alibainisha kuwa miongoni mwa changamoto kuu zinazoikabili taasisi hiyo, mbali na athari za vita na mzingiro ambazo zimeathiri huduma za msingi, ni udhaifu wa ufadhili wa kifedha na upungufu wa fursa za kupata mitaji kwa ajili ya miradi midogo.

Hata hivyo, licha ya changamoto hizo, taasisi hiyo inaendelea mbele kwa rasilimali chache lakini kwa dhamira thabiti. Katika mipango yake ya baadaye, taasisi hiyo ya hisani inapanga kufungua vituo vipya vya mafunzo katika mikoa mbalimbali na kupanua nyanja za elimu ili kujumuisha masomo ya masoko ya kielektroniki (digital marketing), usimamizi wa fedha, na ufungashaji wa bidhaa. Pia inatarajia kuanzisha maabara mpya na kuimarisha ushirikiano na taasisi za kusaidia miradi kwa lengo la kudumisha uendelevu wa miradi yake.

Vikwazo vya kiuchumi na fursa mpya kwa wanawake wa Yemen

Al-Mu’ayyad alisema kuwa, katika mazingira ya vikwazo vya kiuchumi, kampeni ya wananchi ya kususia bidhaa za Marekani na Israel ni fursa muhimu kwa wanawake wa Yemen. Fursa hiyo inawawezesha kuendeleza uzalishaji wa ndani na kutengeneza bidhaa zinazoweza kushindana sokoni. Alisisitiza kuwa kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu wa kuunga mkono bidhaa za kitaifa ni jambo linaloweka msingi wa kufikia kujitegemea na kuimarisha uchumi wa taifa.

Ujumbe wa matumaini kwa wanawake wa Yemen

Al-Mu’ayyad alihitimisha hotuba yake kwa ujumbe wa kutia moyo, akisema: “Tunamwaambia kila mwanamke wa Kiyemeni: msikubali kushindwa na hali zilizopo, kwa kuwa kila changamoto inaweza kubadilishwa kuwa mafanikio. Taasisi ya Khayrat al-‘Atā’ inasimama pamoja nanyi kwa elimu na msaada, ili muwe wanawake wazalishaji mnaoshiriki kwa heshima katika kuijenga nchi yenu.”

Kwa hivyo, Taasisi ya Maendeleo ya Khayrat al-‘Atā’ inatoa mfano wa kujivunia kutoka Yemen katika nyanja za kuwawezesha wanawake kiuchumi, ikisisitiza kuwa wanawake wa Yemen wana uwezo wa kubadilisha uvumilivu na subira yao kuwa tija, na mateso yao kuwa baraka endelevu.

Wanawake wa Yemen hawawezi kupuuzwa

Wanawake wa Yemen ni nguvu ya kweli ya kijamii na kiuchumi inayopaswa kuhesabiwa. Wameonyesha wazi kuwa hawako tu kama waathirika wa vita, bali ni nguvu hai ya mabadiliko ambayo haiwezi kupuuzwa. Wanawake wengi wa Yemen, kutokana na mchango wao katika kazi za kibinadamu, haki za binadamu na maendeleo ya kijamii, wamepata tuzo na heshima mbalimbali — ushahidi tosha kuwa licha ya mazingira magumu wanayokabiliana nayo, wanawake wa Yemen wana uwezo wa kuleta mabadiliko halisi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha