Jumanne 24 Februari 2026 - 17:15
Ni vipi utaingia katika Mwezi wa Ramadhani ukiwa na nafsi iliyotakasika

Hawza/ Mwanadamu anapaswa kuyaona matendo yake kuwa yako mbele ya Mwenyezi Mungu, ajiepushe na kusengenya na kutuhumu, aingie katika Mwezi wa Ramadhani akiwa na moyo safi, adiriki makosa ya zamani na atubie, na kwa utakaso wa nafsi pamoja na kutekeleza wajibu wake, ajihusishe na Mtume wa Mwenyezi Mungu na Qur’ani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ruhollah Khomeini (r.a) katika siku za uhamisho wake huko Najaf, akizungumza mbele ya wanazuoni na wanafunzi wa elimu za dini, alisisitiza kwamba; kila tendo linalotoka kwa mwanadamu liko mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akasema:

“InshaAllah mtaingia katika Mwezi Mtukufu mkiwa na nafsi zilizo salama; na katika mwezi huu mjione kuwa mpo katika dhifa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mumuone Yeye kuwa ndiye mwenye kuwakaribisha, na mjue kuwa Yeye yupo na anashuhudia.

Iwapo — Mungu aepushe mbali — mtataka kumdhalilisha mtu, tambueni kwamba mko mbele ya Mwenyezi Mungu mnamdhalilisha mja Wake. Ikiwa mmesengenya muumini, jueni kwamba mmesengenya mbele ya Mwenyezi Mungu. Matendo yenu — kwa mujibu wa riwaya — huwasilishwa mbele ya Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake).

Iwapo matendo yenu yatawasilishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu akaona kuwa mmekuwa wakosaji, atahuzunika kwa kiasi gani?! Msifanye Mtume wa Mwenyezi Mungu ahuzunike; msiichafue moyo wake mtukufu. Iwapo siku moja ukurasa wa matendo yangu na yenu utapelekwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na akaona umejaa usengenyaji, tuhuma, matusi na mengineyo; na kwa upande wa moyo, ambao yeye anaujua, ukaona umeelemea kabisa katika dunia; na kwa upande wa maadili, umejaa maovu kama chuki, husuda, kinyongo na mtazamo mbaya kwa watu — basi akiona hali kama hiyo, huenda akahisi aibu mbele ya malaika wa Mwenyezi Mungu na mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba mtu huyu ni katika wafuasi wako, ni katika Mashia wako, ni katika umma wako.

Mwanadamu, ikiwa mtu anayehusiana naye — tuchukulie ni ndugu yake, mwanawe, jamaa yake au hata mtumishi wake — akifanya jambo baya, huona aibu mbele ya watu. Ninyi nyote mmehusiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kwa kuja kwenu katika hawza hizi, mmejihusisha na fiqhi ya Uislamu.

Mmejihusisha na Mtume wa Mwenyezi Mungu na Qur’ani ya Mwenyezi Mungu. Huenda Mtume wa Mwenyezi Mungu akaathirika iwapo mtafanya jambo baya. Huenda — Mungu aepushe mbali — badala ya kuwaombea dua, akatulaani.

InshaAllah katika Mwezi wa Ramadhani mlipie; ikiwa jambo fulani baya limetokea kutoka kwenu, lidirikini. Iwapo mmefanya dhambi — Mungu aepushe mbali — kabla ya kuingia Ramadhani, tubuni na mrudi kutoka katika dhambi hiyo. Jueni kwamba maangamizi ni mengi; jueni kwamba kuna njia nyingi tunazopaswa kupita; hatari ni nyingi mbele yetu. InshaAllah mtaingia katika Mwezi wa Ramadhani mkiwa na nafsi salama na safi; na ndani ya Ramadhani pia tekelezeni wajibu wake.

Mwenyezi Mungu, InshaAllah, awape nyote tawfiq.”

(Sahifa-ye Imam, Juzuu ya 2, uk. 390–391)

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha