Jumanne 24 Februari 2026 - 14:15
Chemli ya Ramadhani | Mafunzo Muhimu ya Haki za Wanawake katika Surat An-Nisaa

Hawza/ Juzuu ya nne ya Qur’ani Tukufu inajumuisha Surat Aal-Imran (kuanzia aya ya 93 hadi mwisho) na Sura An-Nisaa (aya ya 1–24). Surat An-Nisaa ina aya 176, imeteremshwa Madina, na inasisitiza ufuasi kamili wa hukumu za Mwenyezi Mungu na uadilifu wa kijamii.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika majira ya masika ya Qur’ani, jalada la “Chemli ya Ramadhani” pamoja na maelezo mafupi na yenye matumizi ya aya za Qur’ani Tukufu, yatakayotolewa na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ali Zarei, mwalimu wa Hawza na mtaalamu wa elimu za Qur’ani, litawasilishwa katika meza zenu za futari enyi wasomi.

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu; tupo katika juzuu ya nne ya Qur’ani Tukufu. Juzuu hii inajumuisha Sura Tukufu ya Aal-Imran kuanzia aya ya 93 hadi mwisho wa sura, na Sura Tukufu ya An-Nisaa kuanzia aya ya kwanza hadi aya ya 24.

Sura Tukufu ya An-Nisaa imeteremshwa Madina na ina aya 176. Mada kuu na ya msingi ya sura hii ni kwamba kufuata hukumu zote za Mwenyezi Mungu katika maisha ni sharti la  kumuabudu Mola kwa dhati.

Mwanadamu hawezi kusema: “Ninakubali hukumu zile zilizo na manufaa kwangu, na zile zilizo ngumu kwangu sizikubali.” Uchaji Mungu unapaswa kuwa katika pande zote na ujumuishwe katika masuala yote na hukumu zote za Kiungu, ili mtu ahesabiwe kuwa mja wa kweli wa Mwenyezi Mungu.

Katika sura hii yamejadiliwa masuala mbalimbali, miongoni mwao: Uumbaji wa mwanadamu na kuundwa kwa familia, Hukumu za kisheria na kiuchumi za familia kama vile kuoa wake wengi, wajibu wa kutoa mahari, mirathi na mgawanyo wake, Uharamu wa kuwaoa maharimu na uongozi wa mume, Masuala ya migogoro ya kifamilia na uasi (nushuz), uadilifu, imani na kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, Kuwasaidia mayatima na kuwalinda, Kudumisha undugu na umuhimu wa kumtii kiongozi, Kumtambua adui na wajibu wa watu miongoni mwao, Uadilifu katika amana pamoja na masuala mengine ya kijamii.

Hukumu na haki nyingi za wanawake zimeelezwa katika Sura Tukufu ya An-Nisaa. Kwa sababu hiyo, sura hii inajulikana kwa jina la Sura An-Nisaa. Katika baadhi ya tafsiri, sura hii imeitwa “Sura Kubwa ya Wanawake” na Sura At-Talaq kuitwa “Sura Ndogo ya Wanawake.”

Katika aya ya kwanza ya sura hii, Mwenyezi Mungu amekanusha aina yoyote ya ubaguzi wa kijinsia na amesema kwamba mwanamke na mwanaume wameumbwa kutokana na nafsi moja, na wote wawili ni sababu ya kuenea kwa kizazi cha binadamu. Mwenyezi Mungu hakuwatofautisha wawili hao kwenye ubora wa asili.

Ni muhimu tuisome sura hii, tuyazingatie maudhui yake, na tutende kwa mujibu wa amri na maelekezo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ili tufanikiwe.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha