Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ni wachache ambao katika siku na wiki za hivi karibuni, katika wigo wa vyombo vya habari na katika anga la mitandao ya kijamii, hawajasikia jina “Jeffrey Epstein” au hawajasoma habari na makala kuhusu tajiri huyu fisadi wa Kimarekani na janga lililotokea katika kisiwa chake.
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi siku chache zilizopita alieleza kuhusu suala hili: “Kufichuka kwa ufisadi wa kushangaza katika kisa cha ‘kisiwa chenye sifa mbaya’ kunaonesha uhalisia wa ustaarabu na demokrasia huria ya Magharibi. Yote tuliyokuwa tukiyasikia kuhusu ufisadi wa viongozi wa Magharibi ni upande mmoja, lakini kisa cha kisiwa hiki ni upande mwingine. Bila shaka huu ni mfano tu wa wingi wa maovu yao; kama ambavyo suala hili halikuwa wazi lakini limefichuka, yapo mengi pia ambayo yatafichuka baadaye.”
Tunda baya la demokrasia huria ya Magharibi
Kwa mujibu wa Morteza Mofidnejad, vyombo vya habari vya Magharibi vinajaribu kukwepa mtazamo wa kimfumo na wa kimsingi kuhusu jalada hili na kulipunguza hadi kiwango cha tukio la kusikitisha tu. Mwandishi huyo wa habari aliongeza: Hata hivyo, mtazamo wa nje ya maandishi (wa kina na mpana) kuhusu jalada la Epstein unapaswa kuchukua nafasi ya mtazamo wa ndani ya maandishi na ulio na mipaka. Jalada la Jeffrey Epstein haliwezi kupunguzwa hadi kuwa kashfa ya maadili au upotovu wa mtu binafsi, kwa sababu kwa hakika ni mojawapo ya mifano iliyo wazi kabisa ya mkutano wa nguvu, utajiri, ufisadi na kinga ya kisiasa ndani ya muundo wa demokrasia huria ya Magharibi; muundo ambao kwa miaka mingi umejitambulisha kama kielelezo cha kimataifa kwa kaulimbiu za uwazi, utawala wa sheria na maadili ya kisiasa, lakini katika kukabiliana na jalada kama hili umeonekana ima kushindwa au kukosa nia.
Aidha alibainisha kuwa, Jeffrey Epstein hakuwa mtu wa pembeni, bali alikuwa na ufikiaji mpana kwa wasomi wa kisiasa, kifedha na kimedia wa Marekani na Ulaya. Uwepo wa mara kwa mara wa wanasiasa wa ngazi za juu, mabilionea, wanazuoni na watu wenye ushawishi karibu naye uliudhihirishia ulimwengu kwamba; kulikuwa na mtandao wa nguvu uliokuwa ukifanya kazi kwa miaka mingi katika eneo salama nje ya mkono wa sheria. Hapa ndipo swali la msingi linapaswa kuulizwa kwa uzito zaidi: imekuwaje kwa miaka mingi, pamoja na watu wengi waliohusika katika jalada hili, suala hili lilibaki kimya na halikufikia hatima yoyote?
Mofidnejad aliendelea kusema: Ukweli wa msingi ni kwamba; kwa miaka mingi, watu waliposema ustaarabu wa Magharibi unaelekea kudidimia, walikabiliwa na mashambulizi ya kifikra na kimaadili. Baadhi walijitahidi kwa nguvu zote kuthibitisha kuwa; ustaarabu wa Magharibi utaendelea kwa fahari katika nguvu zake; lakini muda umeonyesha kuwa ndani ya mti huu wa kale kumejaa wadudu na kuoza kwa kiasi kwamba uwezekano wa kubomoka kwake umeongezeka sana.
Athari haramu za siasa isiyo na maadili
Aliongeza kuwa: Kisiwa kile na matukio yaliyotokea kimyakimya na bila ufahamu wa wanadamu miongo miwili iliyopita, vina ujumbe wazi kwa ulimwengu mzima: siasa bila maadili, mapema au baadaye, hufika kwenye ukomo wa uhalali wake. Kufukia ukweli, kuwaondoa watu na kusimamia mgogoro kwa njia ya kimedia, huenda kukawa na manufaa ya muda mfupi, lakini kwa muda mrefu huichosha na kuharibu imani ya umma. Ijapokuwa imesemwa kuwa mmiliki wa kisiwa hicho amefariki miaka kadhaa iliyopita, jalada lake limefunguliwa upya hivi karibuni na limekuwa alama ya kuhoji misingi ya nadharia ya Magharibi ya kisasa.
Mkanganyiko wa vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu jalada la Epstein
Dkt. Ma’soumeh Nasiri, mhadhiri na mtafiti wa elimu ya vyombo vya habari, huku akisisitiza kwamba, suala la Epstein linahitaji kuchambuliwa kwa mtazamo wa kimedia kwa kina na uchunguzi makini, alisema: Katika ulimwengu ambamo hata matukio madogo yanaweza kuwa vichwa vikubwa vya habari, kwa hakika inafaa kuuliza swali la msingi: imekuwaje jalada lenye ukubwa huu limefunikwa chini ya kivuli cha usiri na udhibiti wa vyombo vya habari?
Aliongeza kuwa: Licha ya kuchapishwa baadhi ya taarifa zinazohusiana na jalada hili, bado inaonekana kuwa uwazi wa kimedia na mtiririko huru wa habari ambao Magharibi daima imejinasibu nao hauonekani kikamilifu. Aidha, uchapishaji wa taarifa hizi unaonekana kuwa matokeo ya mvutano wa kisiasa na kiusalama kati ya nchi kadhaa, ambao kwa sasa unatumika kusimamia maoni ya umma.
Alisema: Hoja kuu ni kwamba, mfumo wa Magharibi ambao kwa miaka mingi umezungumzia haki za binadamu na mtiririko huru wa habari, umewezaje kuficha suala muhimu kama hili chini ya tabaka za udhibiti na udikteta wa maudhui na majukwaa? Tukio hili linapaswa kumfanya msomaji kutafakari: je, ni mfumo wa utawala wa kimedia unaoamua nini tuone, lini tuone na kwa mtazamo upi?
Wakati viongozi wa Magharibi wanapohusishwa na jinai
Nasiri alibainisha kuwa: Kinachovutia ni kwamba, katika ulimwengu wa sasa, masuala mengi yasiyo na umuhimu hupewa uzito wa bandia, huku masuala nyeti kama jalada hili au suala la Ghaza na matukio mengine yanayokwenda kinyume na maslahi ya mfumo wa utawala yakibaki katika pazia la usiri na kupuuzwa.
Aidha alisema pia: Kwa mtazamo wa vyombo vya habari, jalada hili halipaswi kuhusishwa tu kwenye masuala ya haki za binadamu na unyanyasaji wa watoto, japokuwa hayo pia ni muhimu sana. Ikiwa tukio kama hili lingetokea katika nchi ya Kiislamu, vyombo vya habari vya Magharibi vingelifanya kuwa kashfa ya kimataifa; lakini sasa kwa kuwa viongozi wa Magharibi wanahusika, hakuna hisia ya aibu wala uchunguzi makini kutoka kwa vyombo vikuu vya habari.
Suala linalozidi unyanyasaji wa kijinsia
Mhadhiri huyo aliendelea kusema: Tabaka la kina zaidi la kisa hiki linazidi suala la unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, kwa sababu hoja kuu ni uwepo wa ibada za kishetani na juhudi za kuunda aina ya dini mpya katika kisiwa hicho. Kwa hiyo, dini zote za mbinguni zinapaswa kuonesha mwitikio wa pamoja na wa dhati katika kiwango cha kimataifa dhidi ya jambo hili.
Alisema pia: Hapa, mapambano kati ya haki na batili, usafi na uchafu, Mungu na shetani, yamejitokeza kwa uwazi mkubwa. Msomaji makini anapaswa kuuliza: imekuwaje mada yenye ukubwa huu, pamoja na ripoti za maelfu ya watoto kuwa wahanga, inapotea katika anga la vyombo vya habari duniani na hakuna anayezungumzia? Mikono inayoamua nini kionekane na nini kifichwe ni ile ile inayotokana na mitazamo ya kishetani. Lazima pia ichunguzwe nafasi ya Hollywood, muziki na tasnia nyingine za kitamaduni za Magharibi katika kueneza mitazamo hii ya kishetani.
Nasiri alihitimisha kwa kusema: Kwa mtazamo wa elimu ya vyombo vya habari, tunakabiliwa na anga jipya; anga ambalo halitazami tu maudhui ya juu juu, bali pia huchunguza chanzo cha ujumbe, itikadi ya mtumaji na uhusiano wake na mikondo hii iliyofichika. Hivyo basi, katika elimu na uchambuzi wa vyombo vya habari, tabaka hizi za ndani zinapaswa kutambuliwa kwa makini na kujadiliwa kwa uwazi.
Maoni yako