Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hussein Mokhtari, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Vatican, alikutana na Mtukufu Ayatullah Nuri Hamedani.
Mtukufu Ayatullah Nuri Hamedani katika mkutano huo alieleza kuwa: Kuimarisha uhusiano kati ya wafuasi wa dini na kutumia uwezo wa pamoja katika kuanzisha na kuimarisha hari ya kiroho katika jamii za kidini, hasa kizazi cha vijana, ni jambo lenye athari na thamani kubwa. Dunia ya leo inahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote mazungumzo ya kweli kati ya dini na tamaduni.
Akiashiria kumvunjia heshima Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mtukufu Ayatullah al-Udhma Khamenei, na mmoja wa wawakilishi katika Bunge la Ulaya, alisema: Kumvunjia heshima kiongozi wa kidini wa mamilioni ya watu si tu kumshambulia mtu mmoja au hata taasisi ya kidini, bali kwa hakika ni aina ya kuvunja misingi ya maadili katika anga ya kijamii. Katika mazingira kama hayo, lugha badala ya kuwa chombo cha mazungumzo na maelewano hugeuka kuwa silaha ya uharibifu. Maneno ambayo yanapaswa kuwa daraja baina ya nyoyo, hugeuka kuwa ukuta.
Marji' huyu wa taqlidi aliongeza: Matokeo yake ni kwamba; jamii badala ya kuwa na wingi wenye mshikamano, huingia katika wingi wenye uhasama. Hapo ndipo matusi kutoka kuwa tabia ya mtu mmoja hugeuka kuwa mgogoro wa kijamii na hata wa kiustaarabu. Kwa mtazamo huu, kutetea heshima ya viongozi wa dini si tu kuitetea itikadi fulani maalumu, bali ni kutetea msingi wa kuishi pamoja kwa amani.
Mtukufu Ayatullah Nuri Hamedani aliongeza kuwa: Kulinda heshima si dalili ya udhaifu, bali ni alama ya ukomavu wa kitamaduni na kimaadili kwa taifa. Jamii inayoupamba ulimi wake kwa adabu, hata katika hali ya kutofautiana, itahifadhi nuru ya ubinadamu; na huo ndio mtaji ambao hakuna nguvu ya kisiasa au kiuchumi inayoweza kuchukua nafasi yake.
Katika muendelezo wa kikao hicho, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mokhtari aliwasilisha ripoti zinazohusu shughuli za Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vatican.
Akiweka wazi kwamba mikutano mbalimbali imefanyika kwa ushiriki wa wanazuoni wa kidini kutoka Iran na Vatican kwa mhimili wa uwezo wa pamoja kati ya Uislamu na Ukristo, aliomba kuwepo kwa juhudi zaidi kutoka kwenye hawza za kielimu na vyuo vikuu katika kuongeza uhusiano wa kidini baina ya dini tofauti.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mokhtari pia alirejea safari ya wawakilishi watatu wa Kikristo wa Bunge la Ushauri la Kiislamu kwenda Vatican, na akasema: Kwa mnasaba wa siku za kheri za muongo wa Fajr, wawakilishi watatu wa kidini katika Bunge la Ushauri la Kiislamu walisafiri kwa ajili ya kushiriki katika hafla ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, iliyofanyika kwa uwepo wa mabalozi wa nchi mbalimbali wanaoishi Vatican.
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu hukk Vatican aliongeza kuwa: Wawakilishi hao wa Kikristo, pamoja na kukutana na maafisa wa Vatican na kushiriki katika mkutano wa waandishi wa habari wa mashirika mashuhuri ya Italia na Vatican, waliwafafanulia hali halisi za ndani ya nchi na wakakanusha habari na ripoti za uongo za maadui wa mfumo, na wakasisitiza kuwepo kwa uhuru wa aina mbalimbali, ikiwemo uhuru wa dini na madhehebu.
Aidha, kuhusu kumvunjia heshima Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na mwakilishi wa Italia katika Bunge la Ulaya, alisema: Ikiwa wanasiasa kweli wanajiona kuwa wawakilishi wa ustaarabu, basi ishara ya kwanza ya ustaarabu wao inapaswa kuwa ni ustaarabu wa maneno na heshima.
Kuwaheshimu viongozi wa kidini wa wengine si fadhila, bali ni wajibu wa kimaadili na sharti la kuishi pamoja kimataifa.
Maoni yako