Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, nchi kumi na nne pamoja na mashirika matatu ya kikanda siku ya Jumapili zililaani kauli za Mike Huckabee, balozi wa Marekani nchini Israel, ambaye alisema: “Ni jambo linalokubalika kwa Israel kudhibiti ardhi zinazomilikiwa na nchi za Kiarabu, ikiwa ni pamoja na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.” Kufuatia kauli hizi za kiutawala na za msimamo mkali, wimbi kubwa la hasira lilizuka katika mitandao ya kijamii dhidi ya matamshi ya balozi huyo wa Marekani, matamshi yanayoonesha mpango hatari wa Israel na Marekani dhidi ya Umma wa Kiarabu na Kiislamu.
Katika muktadha huo, “Mohammad Nasser Hatrosh”, mwandishi wa Kiyemeni, aliandika katika makala yake kwenye gazeti la Al-Samira: Kauli za Michael Huckabee, balozi wa Marekani katika utawala wa Kizayuni, zimezua hasira kubwa katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, kwa sababu matamshi hayo yaligusia uhalisia wa tamaa za Kizayuni katika eneo hili.
Mohammad Al-Farah, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah, katika uchambuzi wake wa kisiasa wa taarifa hiyo alieleza kuwa, kauli hizo si “kuteleza kwa ulimi” tu, bali zinaashiria kipaumbele cha wazi cha kuangusha tawala kubwa za Kiarabu, hususan Saudi Arabia na Misri.
Al-Farah, akisisitiza kuwa, mradi wa Kizayuni unalenga kugawanya eneo hili, alionya kwamba, iwapo nchi hizi hazitapitia upya mikakati yao ya uhasama dhidi ya Yemen, zamu ya kila mmoja itafika. Aliielezea Yemen kuwa “ngome” ya eneo hili na akalinganisha ulazima wa kuisaidia na hali ya “ndugu wa Yusuf” kwa ndugu yao baada ya kumtupa kisimani.
Yahya Nafi’, mwanaharakati wa Kipalestina, alichambua haiba ya balozi wa Marekani nchini Israel na kueleza kuwa, hatari yake inatokana na uhusiano wake na harakati pana ya “Uzayuni wa Kikristo” nchini Marekani, ambayo kwa msingi wa tafsiri za Biblia inaamini kuwa Israel ina haki juu ya ardhi hii. Pia alionya kuwa serikali ya Trump huenda ikaandaa mazingira bora ya kugeuza ndoto hizi za “kimetafizikia” kuwa uhalisia wa kijiografia unaoonekana na unaolitishia eneo hili.
Tangazo hatari na la wazi zaidi la kuangamiza Waarabu
Kauli za balozi wa Marekani zinaonesha nia halisi ya Washington, inayotafuta kuuhudumia utawala huu wa muda na kupanua ushawishi wake katika eneo hili. Ahmed Atwan, mwanahabari wa Misri, alizielezea kauli hizi kuwa “tangazo hatari na la wazi zaidi la kuangamiza Waarabu” kwa manufaa ya upanuzi wa Kizayuni.
Atwan alirejelea hoja za Tucker Carlson, mtangazaji wa Marekani, ambaye alifichua udhaifu wa mantiki ya kihistoria ya Huckabee na akaweka shaka juu ya uhalali wa madai ya Benjamin Netanyahu (aliyezaliwa katika familia yenye asili ya Ulaya ya Mashariki) kuhusu ardhi ambayo hana mizizi iliyothibitishwa humo, na hivyo kuiweka simulizi ya Kizayuni katika mgogoro wa kimaadili na kiakili.
Kauli hizi zinakuja sambamba na hali ya ulegevu na utiifu usio wa kawaida wa Waarabu na Waislamu, kama alivyothibitisha Abdulrahman Al-Ahnoumi, mwanaharakati wa vyombo vya habari, aliyesema: “Taarifa za kulaani za Waarabu hazina tena athari.” Al-Ahnoumi alikosoa misimamo rasmi ya Kiarabu iliyokuwa dhaifu, ambayo ilitosheka tu kwa kuomba “ufafanuzi” wa kauli zilizo wazi kabisa za Huckabee. Alisisitiza kuwa tangazo hili la haki “takatifu” ya kuteka Mashariki ya Kati si la kwanza, lakini ndilo la jeuri zaidi, na linaonesha pengo kubwa kati ya ukubwa wa tishio na udhaifu wa majibu rasmi.
Waislamu waamke kutoka katika usingizi mzito
Wakati ufrimasoni wa Kizayuni wa kimataifa unatafuta kuendeleza uhalalishaji wa uhusiano na utawala wa Kizayuni chini ya kivuli cha makubaliano ya amani, kauli za balozi wa Marekani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu zinaweka wazi motisha halisi ya mzozo kati ya Waarabu na Wazayuni, ambapo anathibitisha kuwa inatokana na mafundisho ya kiitikadi tu. Hili linawataka Waislamu kuamka kutoka kwenye usingizi wao mzito na kuungana ili kukabiliana na hatari halisi inayolitishia eneo zima bila ubaguzi.
Katika muktadha huu, Ahmed Salman, mwanaharakati wa Iraq, aliangazia mkanganyiko wa wazi: wakati maadui wanapotekeleza uvamizi wa ardhi zetu kwa visingizio vya kidini vya maelfu ya miaka (kutoka Nile hadi Furati), sisi tunapotaja mashujaa wa Karbala au Khaybar, tunatuhumiwa kuishi katika historia ya zamani. Anaamini kuwa Huckabee ametoa mwanga wa kijani wa kuteka kila kitu na kupuuza sheria zote za kimataifa.
Mkabala usioepukika na kuporomoka kwa dau la kisiasa
Kauli za Mike Huckabee zimeuweka ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu mbele ya changamoto ya kihistoria isiyo na kifani; diplomasia iliyokuwa imejificha nyuma ya kauli mbiu za “amani” na “suluhisho la mataifa mawili” imeporomoka kabisa na nafasi yake imechukuliwa na hotuba inayotegemea umiliki na umilikishaji kwa misingi ya “maandiko ya kidini” yaliyopotoshwa.
Kuunganisha hatima ya eneo zima na tamaa za Kizayuni kutoka Nile hadi Furati kunatupeleka kwenye uhakika wa mwisho wa enzi ya ujanja wa kisiasa, na kuufanya uelewa wa umma na hatua za kivitendo kuwa chaguo pekee la kuendelea kuishi.
Radi amali kutoka Yemen, Palestina, Misri na Iraq inaonesha kuwa, wananchi wa Kiarabu wanafahamu kikamilifu kuwa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni ni mapambano ya “uwepo” na “utambulisho.”
Hivyo basi, kuendelea kutegemea “dhamana za Marekani” kunahesabika kuwa ni kujiua kisiasa, kwa sababu mpango huu si siri tena, bali umegeuka kuwa “ratiba ya kazi” ya wazi ya balozi anayechukulia uporaji wa ardhi za mababu kuwa ni utekelezaji wa irada ya kimungu; na hivyo kuulazimisha Umma kubadili msimamo kutoka hali ya kujihami kwenda katika hali ya kuzuia kwa mkakati wa kina.
Maoni yako