Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa tafiti za Mahdawiyya chini ya anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora”, umekusudiwa kueneza mafundisho na elimu inazohusiana na Imam al-Mahdi (aj).
Aya ya Nne:
«وَلِکُلٍّ وِجْهَةٌ هُوَ مُوَلّیها فَاسْتَبِقُوا الْخَیراتِ أَینَ ما تَکُونُوا یأْتِ بِکُمُ اللّهُ جَمیعًا إِنَّ اللّهَ عَلی کُلِّ شَیءٍ قَدیرٌ»Kila kundi lina Qibla ambacho Mwenyezi Mungu amewapangia kuelekea; basi msibishane sana juu ya Qibla, bali shindaneni katika mambo mema. Popote mlipo, Mwenyezi Mungu atawakusanya nyote (kwa ajili ya malipo na dhambi kutokana na amali nzuri na mbaya); hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila jambo.
(Surat al-Baqara, 2:148)
Katika riwaya nyingi za Ahlulbayt (as), kauli hii: «أَینَ ما تَکُونُوا یأْتِ بِکُمُ اللّهُ جَمیعًا», imetafsiriwa kumaanisha kukusanyika kwa wafuasi wa Imam al-Mahdi (aj) wakati atakapo dhihiri.
Imam al-Baqir (as) amesema kuhusu aya hii:
«یعْنِی أَصْحَابَ الْقَائِمِ الثَّلَاثَ مِائَةِ وَ الْبِضْعَةَ عَشَرَ رَجُلاً قَالَ وَ هُمْ وَ اللَّهِ الاُمَّةُ الْمَعْدُودَةُ قَالَ یجْتَمِعُونَ وَ اللَّهِ فِی سَاعَةٍ وَاحِدَةٍ قَزَعٌ کَقَزَعِ الْخَرِیفِ.»
“Yamaanisha wafuasi wa al-Qā’im (aj) ambao ni watu mia tatu na kumi na tatu. Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Hao ndio ‘umma uliyohesabiwa’ (الأمة المعدودة). Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Watakusanyika wote kwa saa moja tu, kama vipande vya mawingu ya vuli vinavyokusanywa na upepo.”
(Al-Kāfī, Juzuu ya 8, uk. 313)
Imam al-Ridhā (as) naye amesema:
«وَ ذَلِکَ وَ اللَّهِ أَنْ لَوْ قَدْ قَامَ قَائِمُنَا یجْمَعُ اللَّهُ إِلَیهِ شِیعَتَنَا مِنْ جَمِیعِ الْبُلْدَانِ.»
“Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Atakaposimama Qā’im wetu (aj), Mwenyezi Mungu atawakusanya Shia wetu kutoka katika miji yote ulimwenguni wawe pamoja naye.”
(Bihār al-Anwār, Juzuu ya 52, uk. 291)
Tafsiri hii ni ya aina ya maana za batini za Qur’ani, kwani kwa mujibu wa riwaya, baadhi ya aya za Qur’ani hubeba maana kadhaa — moja ni ya dhahiri kwa watu wote, na nyingine ni ya ndani (batini) ambayo hujulikana tu kwa Mtume (saww), Maimamu (as) na wale aliowachagua Mwenyezi Mungu.
Kutokana na mtazamo wa riwaya hizi, Mwenyezi Mungu ambaye ana uwezo wa kuzikusanya chembechembe za udongo wa wanadamu siku ya Kiyama kutoka pembe zote za dunia, bila shaka anaweza pia kuwakusanya wafuasi wa Imam Mahdi (aj) kwa siku moja na saa moja, ili kuasisi dola ya haki ya kimataifa na kuondosha dhulma na ukandamizaji duniani.
Aya ya Tano
«بَقِیتُ اللّهِ خَیرٌ لَکُمْ إِنْ کُنْتُمْ مُؤْمِنینَ وَما أَنَا عَلَیکُمْ بِحَفیظٍ»“Kile ambacho kimebaki kutoka kwa Mwenyezi Mungu (mali halali na neema zake) ni bora kwenu ikiwa nyinyi ni waumini; nami si mlinzi wenu.”
(Surat Hūd, 11:86)
Katika riwaya mbalimbali, neno “Baqiyyatullāh” (بقیة الله) limetafsiriwa kumaanisha Imam al-Mahdi (aj) au baadhi ya Maimamu wengine (as).
Imam al-Baqir (as) amesema:
«وَأَوَّلُ مَا ینْطِقُ بِهِ هَذِهِ الْآیةُ «بَقِیتُ اللَّهِ خَیرٌ لَکُمْ إِنْ کُنْتُمْ مُؤْمِنِینَ» ثُمَّ یقُولُ: أَنَا بَقِیةُ اللَّهِ فِی أَرْضِه.»
“Maneno ya kwanza atakayoyasema (Imam Mahdi) baada ya kudhihiri kwake ni aya hii: «بَقِیتُ اللّهِ خَیرٌ لَکُمْ إِنْ کُنْتُمْ مُؤْمِنینَ». Kisha atasema: ‘Mimi ndiye Baqiyyatullāh katika ardhi Yake.’”
(Kamal al-Dīn wa Tamām al-Ni‘mah, Juzuu ya 1, uk. 330)
Ni kweli kwamba katika muktadha wa aya hii, waliokusudiwa ni kaumu ya Nabii Shu‘ayb (a.s.), na “Baqiyyatullāh” imefasiriwa kuwa faida halali iliyobaki au thawabu za Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo, kila kiumbe chenye manufaa kilichobakia duniani kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya uongofu na ustawi wa wanadamu, kinaweza kuitwa “Baqiyyatullāh.”
Kwa msingi huu, manabii wote wa Mwenyezi Mungu na viongozi watukufu ni miongoni mwa Baqiyyatullāh.
Na kwa kuwa Imam Mahdi (aj) ndiye kiongozi wa mwisho na mkubwa zaidi baada ya Utume wa Mtume Muhammad (saww), basi yeye ndiye mfano ulio wazi zaidi wa “Baqiyyatullāh” na mwenye kustahili zaidi jina hilo — hasa kwa sababu ndiye aliyebakia kati ya Mitume na Maimamu kama mrithi wa mwisho wa uongozi wa kimungu.
Aya ya Sita
«هُوَ الَّذی أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدی وَدینِ الْحَقّ لِیظْهِرَهُ عَلَی الدِّینِ کُلِّهِ وَلَوْ کَرِهَ الْمُشْرِکُونَ.»“Yeye ndiye aliyemtuma Mtume Wake kwa uwongofu na dini ya haki, ili aidhihirishe juu ya dini zote, ijapokuwa washirikina watachukia.”
(Surat al-Tawbah, 9:33)
Aya hii, kama ilivyobainishwa katika riwaya nyingi, ni miongoni mwa aya zinazohusishwa na ushindi wa mwisho wa haki juu ya batili na kutimia kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kupitia kudhihiri kwa Imam al-Mahdi (aj), ambaye atauonesha Uislamu katika utukufu wake kamili, na kuufanya uenee juu ya dini zote duniani.
Baadhi ya wafasiri wamechukulia ushindi unaotajwa katika aya hii kuwa ni ushindi wa eneo maalumu, uliofikiwa katika zama za Mtume Muhammad (saww) au katika vipindi vilivyofuata baada yake. Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa aya hii haina kizuizi chochote wala sharti lolote, na imekuja kwa maana ya jumla kabisa, hakuna sababu ya kuipunguza maana yake.
Kwa hivyo, tafsiri sahihi ni kwamba aya hii inamaanisha ushindi wa kina na wa kimataifa wa Uislamu juu ya dini zote, yaani, hatimaye Uislamu utatawala uso mzima wa dunia na kuenea kila pembe ya ardhi.
Hakuna shaka kuwa jambo hili kwa sasa halijatekelezwa kikamilifu, lakini ahadi hii thabiti ya Mwenyezi Mungu ipo katika hatua za utekelezaji wake. Kwa mujibu wa riwaya nyingi, ukamilifu wa mpango huu utafikiwa wakati Imam Mahdi (aj) atakapo dhihiri, naye ataitekeleza program ya kuusambaza Uislamu ulimwenguni kote.
Shaykh as-Saduq (ra) amenukuu kutoka kwa Imam As-Swadiq (a.s.) katika tafsiri ya aya hii akisema:
«وَ اللَّهِ مَا نَزَلَ تَأْوِیلُهَا بَعْدُ وَ لَا ینْزِلُ تَأْوِیلُهَا حَتَّی یخْرُجَ الْقَائِمُ عجل الله تعالی فرجه الشریف فَإِذَا خَرَجَ الْقَائِمُ لَمْ یبْقَ كَافِرٌ بِاللَّهِ الْعَظِیمِ وَ لَا مُشْرِكٌ بِالْإِمَامِ إِلَّا كَرِهَ خُرُوجَهُ حَتَّی لَوْ كَانَ كَافِرٌ أَوْ مُشْرِكٌ فِی بَطْنِ صَخْرَةٍ لَقَالَتْ یا مُؤْمِنُ فِی بَطْنِی كَافِرٌ فَاكْسِرْنِی وَ اقْتُلْهُ.»
“Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Taawili kamili ya aya hii bado haijateremka, wala haitateremka, mpaka al-Qā’im (aj) atakapo dhihiri. Atakapodhihiri, hapatosalia mkanushaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, wala mwenye kumshirikiaha na anayemkataa Imam, ila atachukizwa na kudhihiri kwake. Hata kama kafiri au mshirikishaji huyo atakuwa amejificha ndani ya kipande cha jiwe, basi jiwe hilo litasema: ‘Ewe muumini! Ndani yangu yupo kafiri; nivunje na muuue!’”
(Kamal ad-Din wa Tamam an-Ni‘mah, Juzuu ya 2, uk. 670)
Baadhi ya wanazuoni wa Kishia wametaja kuwa idadi ya aya za Qur’ani zinazohusiana na mada ya Mahdawiyyat ni zaidi ya 120 aya, na zimeelezewa kwa kina katika vitabu mahsusi vya mada hiyo. Kwa hivyo, hapa tunatosheka na maelezo haya kwa muhtasari.
Utafiti huu unaendelea....
Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Darsnāmeh-ye Mahdawiyyat” kilichoandikwa na Khodā-Morād Salīmiyān, huku ikifanyiwa mabadiliko
Maoni yako