Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kikao hiki kiliandaliwa na Kituo cha Utafiti na Elimu cha Mashia nchini Myanmar katika Msikiti Mkuu wa Mago, mji wa Yangon. Tukio hilo, lililohudhuriwa na wanazuoni, watafiti na wapenda elimu za Kiislamu, lilikuwa fursa muhimu kwa ajili ya kuchunguza fikra na mitazamo ya viongozi wakuu wa Kishia na athari zao za kielimu na kijamii.
Katika kikao hicho, Hujjatul-Islam Sayyid Muhammad Yusuf Mahdi, naibu mkurugenzi wa idara ya utafiti katika kituo hicho, alitoa uchambuzi wa kina kuhusiana na fikra na mitazamo ya kipekee ya wanazuoni na viongozi mashuhuri wa Kishia. Aidha, alizungumzia mitazamo yao kuhusiana na ustaarabu wa Magharibi, pamoja na mikakati yao ya kijamii na kisiasa, akieleza pia mchango wao katika kuiongoza jamii ya Kishia na kukabiliana na changamoto za zama hizi.
Hujjatul-Islam Sayyid Nasir Husein, mhubiri wa Myanmar, katika hotuba yake alijikita katika kuelezea na kuchambua maisha, mchango wa kielimu na juhudi za kimapinduzi za Ayatullah Sayyid Abul-Qasim al-Khu’i (r.a.), Imam Khomeini (r.a.), na Shahid Nimr. Alibainisha nafasi muhimu ya viongozi hao kwenye kuwaongoza wafuasi wa Kishia na kusimama imara dhidi ya dhulma na ukandamizaji.
Hujjatul-Islam Sayyid Ja‘far Ja‘fari, imamu wa Ijumaa wa Msikiti Mkuu wa Mago, alizungumzia maisha na shughuli za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei na Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Sistani, akieleza nafasi zao za kidini, kijamii na kiuongozi ndani ya Umma wa Kiislamu.
Aidha, Zaynab Madinabik, mkuu wa idara ya malezi katika Kituo cha Utafiti na Elimu ya Mashia cha Myanmar, aligusia nafasi ya Waislamu wa Kishia—hasa wanawake—ndani ya Umma wa Kiislamu, akifafanua mchango wao wa kielimu, wa kidini na wa kujitolea. Alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika ukuaji na maendeleo ya jamii ya kidini.
Mwisho wa kikao, Hujjatul-Islam Sayyid Muharram Husein aliwashukuru waandaaji na washiriki wote, kisha kikao kikahitimishwa kwa dua na ibada ya pamoja.
Kikao hiki kilipokelewa kwa mwitikio mkubwa kutoka kwa washiriki, ikiwa kama fursa muhimu ya kujifunza zaidi kuhusiana na fikra pamoja na maisha ya viongozi wa kidini wa Kishia, na pia kwa ajili ya kurithisha vizazi vipya tajriba na mafundisho ya viongozi hao wakubwa.
Maoni yako