Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Arafi, Mkurugenzi wa hawza, katika ujumbe wake ametoa pongezi kwa kuchaguliwa Papa Leon wa kumi na nne kuwa kiongozi wa Katoliki duniani, matini ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Papa Leon wa kumi na nne
Kiongozi Mkuu wa Katoliki Duniani
Kwa salamu na heshima,
Nachukua fursa hii kukupongeza kwa kuchaguliwa kwako katika cheo hiki cha juu cha uongozi wa Kanisa Katoliki. Jukumu hili zito ni fursa adhimu ya kuendeleza juhudi za thamani katika uwanja wa maisha ya kiroho, haki ya kijamii, msingi wa familia, ukaribu kati ya dini za mbinguni, na kupambana na dhulma na ufisadi duniani.
Kadhalika, katika fursa hii, nakupa pole wewe na jamii ya Kikristo duniani kwa kuondokewa na Papa Francis ambaye alitumia maisha yake katika kuhudumia maadili, amani na maisha ya kiroho. Natumai kuwa njia yake iliyojaa nuru na kujitolea kwake kwa uhai wa kiroho itaendelea kuendelezwa.
Misingi ya pamoja kati ya Uislamu na Ukristo, ikiwemo kusisitiza maisha ya kiroho, hadhi ya juu ya familia, haki ya kijamii, kupambana na ufisadi na dhulma, na kumuabudu Mungu mmoja, daima imekuwa misingi ya mazungumzo na ushirikiano wa kujenga kati ya dini na mataifa. Natumai kuwa katika kipindi hiki kipya, ushirikiano huu utaimarika zaidi na kuwa daraja la amani, maelewano na mshikamano wa kitamaduni na kidini duniani.
Pamoja na kukuombea mafanikio na taufiki ya Mwenyezi Mungu, natumai kuwa ushirikiano wa kielimu, kitamaduni na wa kiroho kati ya hawza ya Iran na Vatikani utaendelea kupanuka, na tutafikia mafanikio ya thamani katika njia ya kuimarisha maadili ya kimungu na kibinadamu.
Kwa heshima na dua njema,
Alireza Arafi
Rais wa hawza
Qom – Iran
Maoni yako