Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah al-Udhma Abdullah Jawadi Amoli, leo asubuhi kabla ya adhuhuri katika hafla ya ufunguzi wa kongamano la kimataifa la kumbukumbu ya miaka mia moja tangia kuanzishwa upya Hawza ya Qom, na kwa ajili ya kumuenzi marehemu Ayatollah al-Udhma Haj Sheikh Abdulkarim Hairi mjini Qom, alisema:
Amirul-Mu’minin Ali (a.s) katika Nahjul-Balagha amesema: Kitabu ambacho hakina kifani ni Qur’ani, na wanaolifahamu vyema Qur’ani ni Ahlul-Bayt (a.s). Kilele cha wilaya ni Ali (a.s) na watoto wake, kama ambavyo kilele cha daraja za maarifa ni Ali (a.s) na watoto wa Ali (a.s). Na hata kama Peponi ina daraja mbalimbali, daraja za juu kabisa ni kwa ajili ya hawa maimamu watoharifu (a.s).
Akaongeza kusema kuwa: Qur’ani Tukufu ni kitabu ambacho Ahlul-Bayt (a.s) ndio wafasiri wake. Wala Qur’ani haina kifani wala Ali (a.s) na watoto wake hawana kifani. Katika khutba ya pili ya Nahjul-Balagha amesema kuwa Qur’ani haina kifani, wala Ahlul-Bayt (a.s) hawana kifani.
Mtu mtukufu huyu pia alisema: Qur’ani ni kitabu cha akili na elimu. Imamu Ridha (a.s) amesema kuwa hoja ya Mwenyezi Mungu juu ya watu ni akili. Katika utangulizi wa kitabu cha al-Kāfī, imeelezwa kuwa siri ya kuanza kitabu hicho kwa sura ya “akili na ujinga” ni kwamba mhimili mkuu wa kitamaduni wa Uislamu ni akili. Ikiwa akili itakuwepo, basi Qur’ani itaweza kuhifadhiwa na Ahlul-Bayt wataeleweka na kuhifadhiwa pia, pamoja na kwamba akili hiyo huijenga Hawza ya miaka elfu moja ya Najaf na Qom. Hakika kabisa, ikiwa mwanadamu hana akili, hawezi kuanzisha Hawza.
Akiashiria kwamba marehemu Ayatollah al-Udhma Hairi ndiye aliyefufua Hawza katika karne ya kumi na nne Hijria, alisema: Maulamaa wakubwa kama Ayatollah Buroojerdi, Hujjat na Imam Khomeini walikuja kwenye Hawza hii kwa sababu walikuwa wamejaza mikono yao elimu ya Qur’ani na maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s). Kwa mikono hiyo iliyojaa maarifa ndipo nafasi hii ya juu na tukufu ilipoweza kuundwa.
Ayatollah Jawadi Amoli aliongeza kusema kwamba: Siri, sifa na tabia adhimu ya marehemu Ayatollah Haeri Yazdi, ambaye aliweza kuhuisha Qur’ani, elimu za kiakili, fiqhi na usūl kuliko wakati wowote uliopita, ni jambo linalopaswa kuchunguzwa.
Mtu mtukufu huyu pia alisema: Siku ambazo Hawza ya Qom iliasisiwa zilikuwa ni siku za ukandamizaji. Imam Khomeini katika kuelezea ugumu wa zama hizo alisema: "Siku tunatoka Qom, usiku tunarudi.” Katika mazingira kama haya ndipo Hawza ya kielimu ya Qom iliasisiwa.
Yeye (Ayatollah Jawadi Amuli) aliongeza kusema: Katiba ya Uislamu haituruhusu tufikiri kama bwawa la maji, yaani kukusanya elimu na kuifanya kuwa hazina tu ya maandishi au ya ndani ya moyo. Tunapaswa kuwa kama chemchemi. Imamu Swādiq (a.s) ndiye aliyeweka katiba hii kwa ajili ya Mashia. Yeye anaeleza kwamba haifai mtu kusema zaidi ya kiwango cha elimu alicho nacho au kudai nafasi asiyoifikia.
Hdhrat Ayatollah Jawadi Amuli aliendelea kusema: Imamu Swādiq (a.s) hatutaka sisi tuwe ni watu wa kuhifadhi elimu pekee. Kuwa kama bwawa kunaweza kutatua tatizo la bustani moja tu, lakini kuwa chemchemi kunaweza kutatua tatizo la nchi nzima. Hivyo basi, Imamu Swādiq (a.s) anasisitiza sana umuhimu wa ijtihadi na ubunifu.
Yeye alikumbusha kuwa: Ujumbe wa Qur'ani ni kwamba, Qur'ani kila mara ina ujumbe mpya, na hakuna sehemu nyingine ambapo mtu anaweza kujifunza maneno ya Qur'ani isipokuwa ndani ya Qur'ani yenyewe. Hata leo tunapaswa kusema jambo hili katika jamii ya Kiislamu, kwamba tunapaswa kujifunza kutoka Qur'ani, na tuzame ndani yake kama vile wapiga mbizi, ili tufaidike na bahari hii iliyojaa neema.
Mwanzauoni huyo pia aliongeza kusema: Ikiwa mwanadamu atakuwa na uwezo, na ikiwa akili na mapokezi vitakwenda sambamba, na tukafikiri kama marehemu Sheikh Kulaini, basi kila siku tunaweza kupata ujumbe mpya kwa ajili ya dunia ya leo na kuuweka mbele ya watu.
Ayatollah Jawadi Amuli alisisitiza: Ikiwa akili na elimu za kiakili zitakuwepo Hawza, hakika tutapata mafanikio makubwa. Lakini kama hakutakuwa na akili na hoja za kiakili, basi tutaelemewa na mashaka. Watoto wa Ayatollah al-Udhma Hairi walikuwa wanazuoni wa fiqhi na falsafa. Walijitahidi kuendeleza elimu za kiakili Hawza. Jambo la muhimu ni kwamba tufahamu kuwa tukibakia katika elimu za mapokezi tu, na tukaiteremsha chemchemi kuwa bwawa, basi bila shaka tutapata hasara.
Yeye aliongeza: Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa marehemu Ayatollah Hairi amana hii, naye akawa mtiifu kwa Mwenyezi Mungu. Kufikia daraja ya kuwa "Aminullah" (mtiifu wa Mungu) ni daraja ya juu sana. Mtu akiwa na nafasi ya uongozi anaitwa amiri, lakini anapokuwa mlinzi wa amana anaitwa "Aminullah".
Ulamaa huyo alisema: Wapo wengi waliokuwa "Umanaur-Rahman" – yaani walinzi wa rehema ya Mwenyezi Mungu. Watu wa aina hii, watu wa Kiungu ambao hawajui chochote isipokuwa tauhidi, ni waaminifu. Mtu hawezi kuwa mlinzi wa dini ya Mwenyezi Mungu mpaka awe amin wa Mwenyezi Mungu. Na kwa hivyo, hatofanya chochote kitakachowafanya watu waikimbie dini au waichukulie kinyume na uhalisia wake.
Ayatollah Jawadi Amuli pia alisema: Tunapoingia katika haramu za Ahlul-Bayt (a.s), tunapaswa kuwa na malengo makubwa. Daima tunapaswa, tukiwa katika haramu za Ahlul-Bayt (a.s) na Imamu Ridha (a.s), kumuomba Mwenyezi Mungu elimu kupitia kwa Imaam wa nane (a.s). Tunapaswa kuwa na uwezo wa kupokea elimu hizi na, kwa juhudi kama zile za marehemu Sheikh Abdulkarim Hairi, tuzieneze.
Yeye aliongeza: Daraja ya amana ni kama daraja ya ukhalifa na uongozi – kwamba mtu akiipata, huwa "Aminullah". Na daraja hii nayo ina viwango mbalimbali. Mtu akiwa "Aminullah", basi Mwenyezi Mungu humkabidhi Hawza, na katika historia ya Hawza tumeshuhudia uwepo wa wanazuoni wakubwa na marejeo ya dini.
Ayatollah Jawadi Amuli alisisitiza: Qur'ani Tukufu na Ahlul-Bayt (a.s) ndivyo vilivyoweka msingi huu ili tusipotee. Hivyo basi, tunapaswa kujitahidi kunufaika na Qur'ani na kizazi kitakatifu cha Mtume (a.s) ili tufikie uongofu na ufanisi.
Maoni yako