Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuwadia tarehe 12 Rabiul-Awwal, siku ya kuzaliwa Mtume wa Rehma, Bwana wetu Muhammad Mustafa (saw), kwa mujibu wa riwaya ya Ahlus-Sunna, matukio ya kuvutia yalishuhudiwa katika jiji la kihistoria na kitamaduni la Lucknow nchini India. Katika siku hiyo, sehemu mbalimbali za mji huo zilipambwa kwa picha za Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei (Mola amuhifadhi), Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwenye picha hizo kulikuwa na maandishi yaliyoandikwa: “Ahlus-Sunna tumekubali kwamba Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ndiye kiongozi wetu.”
Kitendo hiki kilipata mwitikio mkubwa miongoni mwa wananchi na kilionekana kuwa ishara ya nafasi na umaarufu unaoongezeka kila siku wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu miongoni mwa Waislamu, hususan Ahlus-Sunna nchini India.
Matukio ya karibuni, hususan vita vya hivi majuzi kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na utawala wa Kizayuni, yamesababisha nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuimarika zaidi, si tu miongoni mwa Mashia, bali pia miongoni mwa Ahlus-Sunna na hata wasio Waislamu, msimamo wa Iran na makundi ya muqawama, hasa Hizbullah ya Lebanon, katika kusimama dhidi ya ubeberu wa Kizayuni na msaada wao wa kivitendo kwa watu wanyonge wa Palestina, umeibua pongezi na heshima kubwa kutoka kwa vijana wengi duniani.
Leo hii, iwe ni Shia au Sunni, na hata watu wengi huru wasio Waislamu, wanazungumza waziwazi kuhusu muqawama na viongozi wake, na wanachapisha tena picha na maneno ya Ayatullah Khamenei katika mitandao ya kijamii wakiashiria kumuunga mkono.
Uwekaji wa picha za Ayatullah Khamenei katika tarehe 12 Rabiul-Awwal na Ahlus-Sunna wa Lucknow, kwa hakika ni alama ya umoja na mshikamano katika kusimama dhidi ya dhulma na ubeberu wa kimataifa, hatua hii inaonyesha kuwa watu huru – bila kujali dini au madhehebu – wapo mstari wa mbele katika kupinga dhulma na kuwaunga mkono wanyonge, huku wakiunga mkono viongozi wa muqawama.
Baadhi ya vijana wa Ahlus-Sunna pia waliandika waziwazi katika mitandao ya kijamii: “Kiongozi wetu ni Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.” Waliashiria pia kuchukizwa kwao na nchi zinazojidai za Kiislamu kama Saudi Arabia na Uturuki ambazo zimenyamaza mbele ya jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni.
Inastahili kuelezwa kuwa mji wa Lucknow katika historia ya kisasa ya India umekuwa na kumbukumbu ya migogoro na tofauti za kidini kati ya Shia na Sunni, migogoro hiyo ilianza mwaka wa 1904 na hadi miaka michache iliyopita, katika nyakati kama vile maombolezo ya Muharram au siku ya 12 Rabiul-Awwal, migongano hiyo ilisababisha vifo na hasara kubwa za mali, lakini leo, mji huo huo uliokuwa wakati fulani uwanja wa migawanyiko, umegeuka kuwa nembo ya mshikamano na umoja katika kusimama dhidi ya dhulma na kuwaunga mkono wanyonge.
Maoni yako