Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, mnamo tarehe 6 Juni “Lucas Luna” maarufu kama “Sagaz”, ambaye ni miongoni mwa wasaidizi wa kisiasa wa “Santiago Caputo”, alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii X akidai kutokea kwa shambulio la kigaidi siku ya Iddul-Adh’ha iliyopita, na akaandika: “Hatujachukia Uislamu vya kutosha.” Dai hili ambalo mara kadhaa lilikataliwa na vyombo vya habari, liliibua wimbi la mwitikio, Kituo cha Kiislamu cha Jamhuri ya Argentina (CIRA) katika tamko rasmi kilitaja kauli hiyo kuwa ni mfano wa wazi wa chuki dhidi ya Uislamu na kikaipinga vikali.
Katika muktadha huo, “Martin Saadeh” katibu mtendaji wa Kituo cha Kiislamu cha Argentina na “Sheikh Muhammad Ahmad Jalal Muhammad” imamu wa Msikiti Al-Ahmad katika eneo la San Cristobal, katika mazungumzo na mwandishi wetu walisisitiza kuwa chuki dhidi ya Uislamu si jambo la pembeni tena, bali limekuwa mkondo wa kutia wasiwasi nchini, Saadeh alisema: “Tangia miaka miwili iliyopita hadi sasa, kumekuwa na matukio mengi ya ubaguzi na vitisho dhidi ya Waislamu; kuanzia dhihaka na kejwli za kudhalilisha, hadi vitisho vya moja kwa moja dhidi ya jamii nzima ya Kiislamu.”
Akaongeza kusema: “Jambo hili halijabakia katika maneno pekee, leo tunashuhudia ukaguzi wa kibaguzi, upekuzi wa mawasiliano ya simu na ukosefu wa usalama wa kutosha misikitini, kwa masikitiko, upendeleo wa kigezo cha pande mbili katika mfumo wa mahakama pia unaonekana wazi; mtu mmoja alikaa mahabusu kwa miezi kadhaa kwa sababu ya kutoa kauli kuhusu Israel, ilhali wale wanaoita wazi wazi kuangamizwa kwa Waislamu wanabaki bila kufikishwa mbele ya sheria.”
Kwa upande mwingine, Sheikh Jalal akieleza kuhusu ukosefu wa uhusiano thabiti kati ya serikali na jamii ya Waislamu alisema: “Jamii ya Kiislamu imekuwepo Argentina kwa zaidi ya miaka 150 na kituo chetu cha Kiislamu kina historia ya zaidi ya karne moja, lakini inapokuja mijadala kuhusu Uislamu kwenye vyombo vya habari, mara chache sana viongozi halisi wa Waislamu hualikwa; badala yake, minbar hutolewa kwa watu wasio na uhusiano wowote na sisi.”
Kwa mujibu wa Saadeh, mfano mwingine wa ubaguzi huu ulijitokeza katika uwanja wa kitamaduni; pale ambapo kipindi cha televisheni “Al-Qalam” ambacho kilikuwa kikirushwa kwa miaka mingi kupitia televisheni ya taifa, mwishoni mwa mwaka 2024 kilisitishwa bila maelezo yoyote, Alibainisha kuwa: “Kipindi hiki hakikuwa na gharama yoyote na kilikuwa kikitayarishwa kikamilifu na sisi, lakini ghafla tu, wakati mgogoro wa Palestina ulipokuwa ukiongezeka, kiliondolewa hewani.”
Sheikh Jalal akiwahimiza wananchi kuhudhuria misikitini alisisitiza: “Uislamu si kile kinachoonyeshwa kwenye video za uchochezi wa chuki, milango ya misikiti yetu ipo wazi kila wakati; hapa watu wanaweza kuona, kuuliza na kusikiliza, tunafanya kazi za misaada, tunawapelekea chakula wahitaji na tunashirikiana na shule, Uislamu ni kile kinachoonekana katika maisha ya kila siku pamoja na watu.”
Aidha, alitaja mazungumzo ya kidini baina ya dini tofauti kuwa ni miongoni mwa maeneo ya kutia matumaini, akaongeza: “Mahusiano yetu na jamii zingine za kidini nchini Argentina ni mazuri, tatizo si baina ya dini, bali ni ujinga na matumizi mabaya ya baadhi ya mitiririko ya kisiasa na vyombo vya habari vinavyonufaika na uchochezi wa chuki.”
Saadeh naye mwishoni alibainisha: “Iwapo kutoa huduma kwa watu, kusambaza chakula na kujitahidi kwa ajili ya amani kutaitwa kurudi nyuma, basi maana ya maendeleo imepinduliwa, amani haiwezi kujengwa kwa maneno ya mdomo, bali lazima kila siku ijengwe kwa vitendo.”
Maoni yako