Jumatatu 7 Aprili 2025 - 13:33
Mus’haf wa karne nne wavutia umma Kaskazini mwa Iraq

Katika kijiji kidogo cha Gelezerde, pembezoni mwa mji wa Sulaymaniyah, kaskazini mwa Iraq, kuna nakala ya Qur’ani Tukufu (Mus’haf) ambayo haiwezi kupuuzwa – sio tu kwa uzuri wake wa kale, bali kwa thamani yake ya kiroho, kihistoria na kitamaduni.

Shirika la Habari la Hawza - Kulingana na IQNA, nakala hii ya Qur’ani, iliyoandikwa kwa mkono zaidi ya miaka 400 iliyopita, sasa ni kivutio kikuu katika jamii hiyo na heshima kubwa kwa Waislamu wa eneo hilo.

Mus’haf huu unahifadhiwa kwa uangalifu ndani ya sanduku la kioo, na huonyeshwa kwa hadhara wakati wa sherehe za Kiislamu kama sehemu ya kuenzi turathi. Wakazi wa eneo hilo wanautambua Mus'haf huo kwa jina la “Qur’ani ya Gelezerde” na kuutazama kama kitu kitakatifu, ambacho hutumika kuapisha watu katika viapo vya ukweli na uaminifu.

Mus’haf huu umebeba muhuri wa Sheikh Hasan Gelezerde, mwanazuoni wa elimu ya Kiislamu aliyeheshimika sana katika enzi zake. Hakuishia tu kuwa sehemu ya historia ya mus’haf huu, bali pia alihusika katika kuuhifadhi na kuukarabati. Kupitia muhuri wake, alithibitisha uhalali na uzito wa maandiko hayo.

Katika mojawapo ya kurasa zake, kuna ujumbe wa kugusa moyo kutoka kwa mama wa Sheikh Hasan Gelezerde aliyeandika:

"Kama kuna kosa katika maandishi haya, nisameheni. Mkono mmoja ulikuwa ukiandika, mwingine ukimbembeleza Hasan kwenye chekeche."

Ujumbe huu si tu unadhihirisha mapenzi kwa elimu ya Qur’ani, bali pia uzalendo wa Kiislamu wa kifamilia – ambapo Qur’ani ilikuwa katikati ya malezi na maisha ya kila siku.

Mus’haf huu umeandikwa kwa hati ya thuluth – mojawapo ya aina za maandiko ya Kiarabu yenye ugumu na uzuri wa kipekee, iliyotumika kwa karne nyingi katika kuandika nakala za Qur’ani na mapambo ya misikiti. Vipimo vyake ni sentimita 24 kwa 40, na kina chake ni sentimita 9.

Mwaka 2015, Mus’haf huu ulifanyiwa ukarabati mkubwa na kuendelea kuwa katika hali nzuri, japokuwa sehemu chache zimeathiriwa na maji. Nakala hiyo iliwahi kutumwa katika Chuo Kikuu mashuhuri cha Al-Azhar nchini Misri, ambako ilitunukiwa tuzo maalum kutokana na umuhimu wake wa kipekee.

Profesa Adnan Hevremani, mhadhiri katika Kitivo cha Sayansi za Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Sulaymaniyah, anasema:

“Watu wanapotoa viapo, huapa juu ya Qur’ani ya Gelezerde." Anaongeza kuwa: “Nakala hii inarudi nyuma takriban miaka 400 na imebeba muhuri wa Sheikh Hasan Gelezerde – Mwenyezi Mungu amrehemu.”

“Turathi hii haiwezi kulinganishwa na mali ya aina yoyote,” amesisitiza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha