Jumatatu 3 Machi 2025 - 12:21
Mwenyezi Mungu Ndiye Mmiliki wa Siku ya Malipo

Hawza / Mwenyezi Mungu kama ambavyo Yeye Ndiye Mmiliki wa Ulimwengu mzima, vile vile Yeye Ndiye Mwenye kumiliki Siku ya Kiyama, ambayo ndio Siku ya Malipo na Siku hiyo watu wote watalipwa kulingana na matendo yao.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Darsa la Tafsiri ya Qur'an Tukufu linaloendeshwa na Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania, Maualana Sheikh Hemed Jalala, katika viwanja vya Masjid Al-Ghadir, Dar-es-Salam, Tanzania, limefunguliwa rasmi kwa kuanza na Tafsiri ya Surat al-Fatiha.

Maualana Sheikh Hemed Jalala akitafsiri na kubainisha Aya Tukufu za Surah hii amesema: Kwa hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t), amebainisha na kuweka wazi juu ya (Umiliki) Ufalme Wake katika Ulimwengu huu, ya kwamba Yeye Ndiye Mmiliki wa Ulimwengu huu na Walimwengu wote, na bali na vyote vilivyomo ndani yake, pale aliposema: “(ٱلْحَمْدُ لله رَبِّ ٱلْعَالَمِینَ) Sifa njema (Himidi) zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa Walimwengu wote". Kwa mantiki hiyo viumbe vyote vinatakiwa kusilimu (kusalimu amri) na kunyenyekea kwa Mola wa Walimwengu wote.

Umiliki na Ufalme wa Mwenyezi Mungu hauishii katika Ulimwengu huu tu, na ndio maana Mwenyezi Mungu baada ya kuelezea na kubainisha juu ya Ufalme (Umiliki) Wake wa Ulimwengu wote, vile vile anaelezea juu ya Umiliki na Ufalme Wake huko Akhera kwa kusema: “ (مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ) Mmiliki wa Siku ya malipo".

Maulana Sheikh Hemed Jalala, akitafsiri na kufafanua Aya hiyo Tukufu amesema kuwa: Dini: Ni neno lenye maana mbalimbali. Linakuja kwa maana ya: Malipo, hesabu, utii, ada (desturi), kutawala na kumiliki. Na makusudio ya neno Dini hapa (katika Aya hii) ni Siku ya Kiyama ambaye Mmiliki wa Siku hiyo ni Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t). Siku hiyo ndio Siku ya Malipo. Kwa maana watu wote watalipwa Siku hiyo kulingana na matendo yao.

Aya hii Tukufu ni dalili na ni uthibitisho wa uwepo wa Siku ya Kiyama (kwamba watu wote watafufuliwa Siku hiyo ili wakalipwe kwa mujibu wa matendo yao walivyotenda hapa Duniani). Hivyo Aya hii inawashawishi waja wa Mwenyezi Mungu na kuwatia moyo (hasa waja wema watakaozingatia na kufuata amri na maelekezo ya Mwenyezi Mungu), lakini pia inatoa kitisho (kwa wale watakaokengeuka na kwenda kinyume na maelekezo ya Mwenyezi Mungu kwamba watambue kuwa ipo siku ya kiyama ambapo katika siku hiyo watahesabiwa matendo yao na kulipwa kwa matendo yao). Kwa mantiki hiyo, Mukalaf (mwenye kutii na kutekeleza Sheria za Mwenyezi Mungu) akifikiria kuwa ipo Siku ya Kiyama na Mwenyezi Mungu Ndiye Mmiliki wa Siku hiyo, ni lazima atakuwa na matumaini, na atakuwa na khofu.

Aidha, katika mlolongo wa Darsa hili amebainisha kuwa: Muislamu anaposimama katika Swala akasoma Surah Al-Fatiha, huwa anamwambia Mwenyezi Mungu kupitia Surah hii kuwa anajiepusha na aina yoyote ile ya Shirki, na anampwekesha na kumuabudu Mwenyezi Mungu (s.w.t) ambaye Ndiye Mwenye Kustahiki kuabudiwa kwa Haki.

Inafaa kuashiria hapa kuwa: Darsa hili la Tafsiri ya Qur'an, hujiri kila Mwaka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, katika viunga vya Masjid al-Ghadir, iliyopo Kigogo Post, Dar-es-salam, Tanzania, likiendeshwa na Maulana Sheikh Hemed Jalala kwa muda wa Mwezi Mzima Mtukufu wa Ramadhan, ambapo Waumini mbalimbali wa Shia na Sunni huhudhuria katika Darsa hili la wazi la Tafsiri ya Qur'an Tukufu, na kufaidika na ilmu, maarifa na maana pana zilizomo katika Aya Tukufu za Qur'an.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha