Jumanne 27 Oktoba 2026 - 12:00
Ayatullah Isa Qasim Atahadharisha Kuhusu Kuwekwa Vikwazo katika Utekelezaji wa Hukumu za Kisheria nchini Bahrain

Hawza/ Ayatullah Isa Qasim, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Bahrain, ametahadharisha kuhusu madhara hatari ya maamuzi yanayowekea vikwazo utekelezaji wa hukumu za Sheria ya Kiislamu nchini Bahrain, amesisitiza kuwa hatua hizo zinafanya utekelezaji wa wajibu wa kidini utegemee kibali rasmi cha serikali.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sheikh Isa Ahmad Qasim, kupitia taarifa yake, ameonya kuhusu matokeo ya maamuzi yaliyopitishwa nchini Bahrain ambayo yanaweka vikwazo katika utekelezaji wa hukumu za Sheria ya Kiislamu. Ameeleza kuwa maamuzi hayo ni sawa na kuweka utekelezaji wa wajibu wa kidini chini ya mamlaka ya “kibali rasmi”, na ameitaka mamlaka husika kuyafutilia mbali mara moja na bila utata wowote.

Ayatullah Sheikh Isa Qasim amefafanua kuwa; maamuzi hayo hayahusu tu kupanga na kudhibiti baadhi ya shughuli za kidini, bali yanavuka mipaka hiyo na kufikia hatua ya kuweka vikwazo katika kutekeleza wajibu wa kisheria. Hali hii inafanya utekelezaji wa wajibu huo utegemee idhini ya mamlaka tawala, jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni kuingilia haki ya dini na hukumu zake.

Taarifa hiyo imeeleza pia kuhusu sharti la kupata kibali cha awali chenye muda wa miaka miwili kwa ajili ya kutekeleza baadhi ya majukumu ya kidini, yakiwemo kuhubiri na kutoa mihadhara. Baada ya muda huo kumalizika, wahusika wanatakiwa tena kuwasilisha ombi la kupata kibali rasmi ili waendelee na shughuli hizo.

Ameeleza kuwa hatua hii haipaswi kuchukuliwa kama fursa au utambuzi wa hadhi ya watu wanaotekeleza majukumu hayo, bali ni jaribio la kuimarisha mamlaka ya taasisi rasmi ya kuwazuia kutekeleza majukumu yao baada ya muda uliowekwa kumalizika.

Ayatullah Qasim ameyaelezea maamuzi hayo kuwa yanapingana waziwazi na haki ya Mwenyezi Mungu, hukumu za dini tukufu ya Uislamu na Kitabu Kitukufu cha Qur’ani. Amesisitiza kuwa hatua za aina hii zinadhoofisha uhuru wa shughuli za kidini, pamoja na nafasi ya wanazuoni na shule za Kiislamu katika kutekeleza majukumu yao ya kisheria.

Akiendelea na taarifa yake, kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu nchini Bahrain ametaka maamuzi hayo yapitiwe na yafutwe waziwazi na mara moja iwapo yalitokana na kutofahamu matokeo yake. Ameonya kuwa kuendelea kuyatekeleza kwa msisitizo, baada ya ukweli na madhara yake makubwa kufichuka, kutasababisha matokeo hatari.

Ayatullah Qasim, mwishoni mwa taarifa yake, amesisitiza hatari ya kuweka wajibu wa kisheria chini ya maamuzi rasmi ya mamlaka. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutatua suala hili kwa namna ambayo utahakikisha heshima na mipaka ya hukumu za Sheria inalindwa, na kuzuia kuwekwa vikwazo katika mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyafaradhisha.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha