Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Mujtaba Hussein Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa ujumbe kwa wasomi mahiri na washindi wa medali za kisayansi na michezo katika mashindano ya kimataifa. Katika ujumbe huo, amebainisha nafasi isiyoweza kufidiwa ya wasomi mahiri na vijana wenye vipaji walioleta heshima katika nyanja za sayansi na michezo, na kuchangia kudhihirisha matumaini, maendeleo na uchangamfu nchini. Ameitaja elimu isiyo na mipaka waliyonayo wasomi mahiri kuwa ndio ufunguo wa kuifanya Iran izidi kuwa imara, amesisitiza kwamba, kwa kuzingatia mkakati mkuu wa «Al-‘Ilmu Sultan» (Elimu ni Ufalme), maendeleo ya nchi yanahitaji msukumo wa kina na wa kasi katika nyanja ya sayansi. Aidha, ameeleza kwamba viongozi wanapaswa kuweka miundombinu na mazingira yanayowezesha hatua hiyo kubwa ya maendeleo ya kisayansi, huku wakitumia kwa kiwango cha juu uwezo wa mtu mmoja mmoja na hekima ya pamoja ya wasomi mahiri.
Mambo Makuu Yaliyoainishwa katika Ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Wasomi wa Sayansi na Michezo
1. Nguvu ya Iran inategemea uwezo wake wa kisayansi na kiteknolojia.
2. Umuhimu wa kuanzisha msukumo wa kina na wa kasi katika maendeleo ya sayansi.
3. Nafasi ya wasomi mahiri katika maendeleo na uimara wa nchi.
4. Kuwapongeza washindi wa medali za kielimu na michezo.
5. Kupanua dhana ya umahiri katika nyanja mbalimbali.
6. Umuhimu wa kuishukuru neema ya umahiri kwa vitendo.
7. Kutumia elimu kwa vitendo ili kutatua matatizo ya nchi.
8. Kuimarisha elimu za msingi na sayansi za kibinadamu.
9. Kuvunja mipaka ya maarifa ya kielimu na kutatua matatizo ambayo hayajapatiwa ufumbuzi.
10. Kusaidia ubunifu na uvumbuzi.
11. Kuimarisha kujitegemea katika sayansi na teknolojia.
12. Kuunganisha vyuo vikuu na sekta ya viwanda pamoja na masoko.
13. Kuendeleza kampuni zinazotegemea maarifa ya kisayansi na kiteknolojia pamoja na biashara changa.
14. Kuelekeza nguvu katika masuala ya kimkakati ya maji, udongo, chakula na nishati.
15. Kuendeleza akili unde na teknolojia za kisasa.
16. Kuwashirikisha wasomi mahiri katika uundaji wa sera na ufanyaji wa maamuzi.
17. Kukabiliana na juhudi za kuwakatisha tamaa na kuwadhoofisha wasomi mahiri.
18. Kuifanya Iran kuwa kitovu cha marejeo ya kisayansi na kiteknolojia duniani.
19. Kuifanya lugha ya Kiajemi kuwa miongoni mwa lugha zinazotumika kama marejeo katika elimu duniani.
20. Kuufanikisha ustaarabu mpya wa Kiislamu na Kiirani.
Maandishi kamili ya ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran, uliosomwa usiku huu katika hafla ya kuwaenzi washindi wa medali za kisayansi na michezo katika tukio lililopewa jina la «Washindi wa Medali Wanaoipenda Nchi Yao», na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Haj Ali Akbari, ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Siku hizi, kwa mujibu wa mojawapo ya kauli zilizopo, zinaambatana na siku za kumbukumbu ya kuuawa kishahidi bibi mtukufu na kiongozi wa wanawake wa Peponi, Hadhrat Siddiqah al-Tahirah Fatimah Zahra, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.
Inashangaza kwamba tarehe ya kuuwawa kishahidi Bibi huyo imeendelea kuwa haijulikani; kama ambavyo mahali patukufu ilipozikwa nuru hiyo ya Mwenyezi Mungu pamebaki kuwa siri. Vilevile, daraja lake la juu na utukufu wa nafasi yake havijulikani kikamilifu, na viko juu ya uwezo wa ufahamu wa mwanadamu.
Alikuwa mtu wa kipekee katika ibada, utiifu na kumtumikia Mwenyezi Mungu; mfano bora katika kuambatana kwa namna ya pekee na ya pande zote na Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu; na katika kumtetea kwa moyo wote Wilayah ya Amirul-Muuminina, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao na familia zao.
Alikuwa pia mfano bora katika kujifunza na kufundisha maarifa, kutambua wakati unaofaa na kusimama kuitetea haki, kusimama imara na kubainisha ukweli. Aidha, alikuwa kielelezo cha daraja la kwanza katika subira, kujitolea, kutoa muhanga, kuwahudumia wengine bila kutarajia malipo na kuhurumiana katika jamii.
Alikuwa mfano bora katika maisha ya ndoa, mama, malezi ya watoto na kulea kizazi cha Maimamu watoharifu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao, ambao ni viongozi wa wanadamu. Vilevile, alikuwa mfano katika juhudi, bidii, mapambano, usafi, unadhifu, uchamungu, nuru na hali ya kiroho. Kwa neno moja, alikuwa kielelezo kwa wanawake na wanaume wote wenye imani.
Miongoni mwa fadhila zinazong'ara za jamii inayofuata mwenendo wa Fatimah ni kwamba huweka wazi mwongozo wa njia ya harakati kubwa za kijamii, kushiriki katika medani na nyanja za mapambano na jihadi, harakati za wananchi, na hata azma ya maendeleo katika nyanja za kielimu na utoaji wa huduma kwa unyenyekevu bila kutarajia malipo. Huu ni mwongozo kwa taifa la Iran ambalo ni la kimapinduzi na la Kiislamu.
Katika kipindi hiki, nchi yetu pendwa ya Iran inadhihirisha zaidi azma na matumaini. Nafasi ya wasomi mahiri na vijana wa Iran wenye vipaji na uwezo katika kuimarisha matumaini hayo, kuleta maendeleo na kuingia katika njia ya mustakabali wake wenye nuru, haiwezi kufidiwa.
Hata hivyo, eneo la umahiri halijafungika katika nyanja za sayansi na teknolojia, michezo au aina mbalimbali za ujuzi. Kila aina ya ubora unaokubalika na wenye manufaa inaweza kumwezesha mtu kutimiza sifa ya umahiri.
Siku hizi tunashuhudia kudhihirika umahiri wa watu bora miongoni mwa wananchi wa nchi hii, ambao wanajitahidi kwa moyo wote kuinua bendera takatifu ya nchi yao, huku wakiangalia upeo mpana zaidi. Hawa ni wasomi mahiri katika utambuzi wa mambo na jihadi.
Tunawaona watu kama Riz‘ali Khajawi na Ali Landi kuwa ni miongoni mwa watu mahiri ambao majina yao yanapaswa kuandikwa kwenye milango ya majengo ya kitamaduni. Miongoni mwa mifano hiyo bora kwenye jamii pia wamo mashahidi na watu waliojitolea nafsi zao, ambao kwa kutoa maisha na afya zao wamekuwa na athari kubwa mno katika hatima ya Iran na taifa lake pendwa. Watu hao walipokea medali ya utumishi kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mmoja wa Pekee.
Kwanza, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wananchi wote wapendwa wa nchi yetu na kila mmoja miongoni mwa walioleta heshima kwa kushinda tuzo na medali mbalimbali za kisayansi katika mashindano ya Olimpiki ya Kimataifa ya Astronomia na Astrofizikia, Hisabati, Elimu za Dunia, Jiografia, Fizikia, Kemia, Baiolojia, Kompyuta na Akili Unde, pamoja na Sayansi za Kibinadamu. Vilevile, nawapongeza kwa mafanikio mbalimbali ya hivi karibuni katika michezo.
Ninatoa pia pongezi na kutambua juhudi na azma ya wale wanaoongoza msafara wa heshima na matumaini, pamoja na wabeba bendera ya maendeleo ya nchi, katika makundi yote ya watu wenye vipaji na umahiri, kuanzia vijana wadogo na wakubwa hadi makocha, walimu, maprofesa na wasomi wenye hekima.
Motisha na matumaini ya wasomi mahiri ya kuleta mabadiliko nchini ni mwenge unaowaka kwa mwangaza mkubwa, ambao nimekuwa nikishuhudia kwa mbali na karibu katika kipindi cha miaka mingi iliyopita.
Kuona harakati kubwa ya wasomi mahiri na mkondo wa kisayansi nchini, wenye kuleta matumaini, pamoja na kudhihirika kwa harakati hizo kupitia ushindi unaojirudia mara kwa mara na kila mwaka katika taaluma za sayansi, mashindano ya Olimpiki ya kitaaluma na michezo, ni jambo linaloleta heshima na fahari kwa taifa lote la Iran.
Nafasi za juu zilizopatikana na wanamichezo wetu wenye bidii katika michezo mbalimbali katika siku na miezi ya hivi karibuni, pamoja na kuweka rekodi mpya, zinaonesha juhudi, bidii, azma na imani yao.
Wanamichezo hao, ambao kwa nguvu za miili yao, uimara wa roho zao, maadili yao mema, imani yao na juhudi zao zinazoendelea, wanaongeza uwezo na nguvu ya Iran yetu pendwa mbele ya macho ya mataifa yote. Kwa kufanya hivyo, wanadhihirisha mbele ya dunia nzima kwamba taifa shupavu la Iran linaendelea kuwa hai na lenye nguvu.
Wanawake wanamichezo ambao huifanya ishara yenye fahari ya mavazi ya mwanamke wa Kiirani kung'ara duniani; washindi wa medali za michezo wanaoleta furaha na shangwe katika nyoyo za wananchi wa Iran na kuipa heshima bendera yenye fahari ya Iran; wote hao, kila mmoja kwa kiwango chake, wanashiriki na kuwa na mchango katika kuipa maana dhana ya Iran imara.
Kwa kuwa siku hizi ni kipindi cha uchangamfu na kuielekeza fikra katika elimu na utafiti kwenye vyuo vikuu, vyuo vya elimu ya dini na shule, naona inafaa nitoe maelezo mafupi kuhusu jambo hili kwa wanaopenda elimu, wasomi mahiri wa taifa na watu wenye hekima wa Iran yetu pendwa.
Umahiri ni neema na kipawa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Msingi wake mkuu ni kipaji na uwezo wa kiakili, ambavyo taifa la Iran, hasa vijana wa nchi yetu, wamejaliwa kwa wingi kuwa navyo kama neema na utajiri mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Sharti la busara na kumtumikia Mwenyezi Mungu, ni kwamba mwanadamu atimize ipasavyo wajibu wa kushukuru neema za Mwenyezi Mungu. Ikiwa shukrani hiyo itatekelezwa katika ngazi zake zote za moyoni, kwa ulimi na kwa vitendo, basi njia ya kufikia ukamilifu wa neema hiyo itafunguliwa.
Kutambua na kuthamini neema ya umahiri kunapaswa kuanza na mtu mwenyewe mwenye kipaji, kisha kuendelea katika mazingira yanayomzunguka, kuanzia kwa wazazi, familia, walimu na maprofesa hadi mazingira ya shule, chuo kikuu na mfumo mzima wa nchi. Lengo ni kukuza na kuongeza uwezo huo, kisha kuutumia kwa usahihi.
Kwa msingi huo, mtu mwenye kipaji ana jukumu zito zaidi katika kuishukuru neema hii kwa vitendo. Inafaa kwake, pamoja na kuimarisha uwezo wake na kukuza kipaji chake, kukitumia kipaji hicho kwa namna bora zaidi katika kutatua matatizo ya nchi na jamii.
Mtu mwenye kipaji si yule ambaye, kwa sababu tu ana akili na uwezo mkubwa wa kufikiri, anajiona kuwa kiumbe wa pekee aliyejitenga na wengine na kufikiria tu matamanio yake binafsi ya muda mfupi. Bali, mtu mwenye kipaji ni yule anayejali kukuza uwezo wake, anayejitambua kuwa sehemu yenye mchango katika jamii, na anayetumia kipaji na uwezo wake kwa ajili ya maendeleo yake binafsi na ya jamii yake kwa pamoja.
Msomi mahiri wa Kiirani ameonesha kwamba inawezekana kuigeuza elimu na kipaji kuwa nyenzo ya kutatua matatizo halisi ya wananchi na nchi. Kuanzia katika nyanja za seli shina, teknolojia ya nano na teknolojia za kibayolojia, hadi teknolojia za kisasa za anga na safari za angani, viwanda, madini, tiba, kilimo, nishati ya nyuklia, nishati kwa ujumla na miundombinu, wasomi mahiri wamekuwa wakijitahidi kutumia sayansi na elimu yao kwa vitendo. Sote tunashuhudia matokeo na mifano ya harakati hii ya maendeleo katika maisha halisi.
Uzalishaji wa umeme kwa kutumia mitambo ya turbine iliyotengenezwa nchini Iran katika vituo vya kuzalisha umeme; matumizi ya teknolojia inayotegemea maarifa ya kisayansi katika mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji katika visiwa vya kusini; ndege zisizo na rubani za kilimo zinazoruka juu ya mashamba, bustani na mashamba ya mpunga ya kaskazini kwa ajili ya kuboresha shughuli za kilimo na matumizi ya maji na udongo; kuzaliwa watoto katika familia zilizokuwa na changamoto ya kutopata watoto kupitia teknolojia za kisasa za Taasisi ya Royan; kugundua na kutibu magonjwa magumu kutibika kwa kutumia dawa zenye mionzi; kufuatilia ardhi, maji na mazao kwa kutumia satelaiti za uchunguzi; pamoja na kuongeza tija na usalama wa chakula kupitia ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia.
Hii ni mifano michache tu inayoweza kutajwa kutoka katika mkusanyiko huu mkubwa wenye manufaa mengi. Mifano mingine mingi, hasa katika nyanja za kiulinzi na kijeshi, imekuwa ikiishangaza dunia mara nyingi unapofika wakati wake, na hali hiyo itaendelea pia katika siku zijazo.
Iran imara inajengwa juu ya nguvu za kisayansi na kiteknolojia. Hili ni mojawapo ya mambo muhimu zaidi yanayoipa Iran nafasi ya kushiriki na kuathiri mlingano wa nguvu na mfumo mpya wa dunia.
Kwa hiyo, ufunguo wa kuifanya Iran izidi kuwa imara ni kwa wasomi mahiri kuvunja mipaka ya maarifa yaliyopo na kupata ufumbuzi wa matatizo ya kisayansi ya nchi. Uovu na uhalifu unaofanywa na maadui dhidi ya Iran kwa kuwalenga wanasayansi na wasomi wake mahiri unaonesha wazi nafasi yenye ushawishi ya wasomi hao katika kuimarisha nchi.
Adui anayewaua kwa kutumia ugaidi wanasayansi mashuhuri na wasomi wenye mchango mkubwa katika jamii yetu, katika vita vya pili na vya tatu vilivyolazimishwa dhidi yetu, na hata miaka mingi kabla ya hapo, katika mazingira yao ya kitaaluma na maisha yao ya kawaida, hawezi kuvumilia kuona Iran ikipiga hatua za maendeleo na kuimarika.
Adui huyo hutumia nyenzo na mbinu zake zote kuwadhoofisha wasomi mahiri wa Iran yetu pendwa. Mbinu hizo ni pamoja na kuwakatisha tamaa na kuwafanya wapoteze matumaini, kuteka fikra na roho zao, kuwameza ndani ya mfumo wa ukoloni mamboleo na kuwageuza kuwa kama vipuri vya mashine ya uporaji na mfumo wa kiuchumi unaotawaliwa na mitaji ya Magharibi.
Adui huyo amesahau kwamba kila tone la damu ya shahidi miongoni mwa wasomi mahiri, wanasayansi, maprofesa, wanafunzi wa vyuo vikuu na wanafunzi wa shule wa taifa hili limekuwa na linaendelea kuchochea tufani ya azma na maendeleo.
Taifa la Iran linakumbuka historia yake ya ustaarabu wa kale, mafanikio yake mbalimbali katika sayansi na ufundi, pamoja na kuwa na watu mashuhuri na wanasayansi waliotambulika duniani. Wakati huohuo, linakumbuka pia karne mbili za hali mbaya ya kubaki nyuma na kushindwa kuchukua hatua katika historia yake wakati wa tawala za Qajar na Pahlavi.
Taifa hili linatambua thamani na umuhimu wa mkakati mkuu wenye ushindi wa «Al-‘Ilmu Sultan» (Elimu ni Ufalme), pamoja na matokeo yake katika kukataa kutawaliwa kisayansi na nchi za Magharibi. Linatambua pia ukuaji wa haraka wa kisayansi na kiutafiti wa wasomi wake mahiri katika miongo mitatu iliyopita, ambapo sehemu kubwa ya mafanikio hayo inatokana na mipango maalumu na mwongozo wa Kiongozi Mkuu na Shahidi wetu mtukufu, Mwenyezi Mungu autakase moyo wake.
Ikiwa kabla ya kipindi hiki cha sasa na vita vya tatu vilivyolazimishwa dhidi yetu, kuanzishwa msukumo mpya wa kisayansi kulikuwa pendekezo muhimu na la lazima kwa wasomi mahiri, uzoefu wa vita viwili vya hivi karibuni umemthibitishia kila mtu kwamba msukumo huu mpya wa kisayansi unapaswa kuwa wa kina na wa kasi zaidi.
Ili kufikia lengo hili, pamoja na viongozi wa taasisi na vituo vya sayansi, utafiti na teknolojia, kila mmoja wa wasomi mahiri na watu wenye hekima wa Iran yetu pendwa anapaswa kujitolea kutekeleza jukumu lake kuu la kujenga mustakabali wenye utukufu wa Iran ya Kiislamu, pamoja na kuendeleza na kuijenga nchi hiyo.
Katika kutekeleza jukumu hilo, wanapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:
Kwanza: Lazima kuwe na mipango madhubuti, ya vitendo na iliyoandaliwa kwa usahihi kwa ajili ya kukuza elimu za msingi na sayansi za kibinadamu nchini. Ukuaji na maendeleo ya elimu za msingi, kama vile fizikia, kemia, sayansi za viumbe na hisabati, ambazo ndizo msingi mkuu wa elimu nyingine na teknolojia zinazotumika kwa vitendo, ni kichocheo cha maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya nchi. Kila taifa lililopiga hatua za maendeleo limefikia hapo kupitia elimu za msingi, nchi isiyokuza elimu hizi itaendelea kubaki nyuma daima.
Pili: Kuelekeza nguvu katika kutafuta ukweli ambao bado haujagunduliwa, kuvunja mipaka ya maarifa katika elimu za msingi na kuendelea kushindana katika kutatua matatizo maarufu ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi katika elimu hizo, hasa hisabati, kunapaswa kuzingatiwa daima kama lengo na mahali pa kufikia.
Tatu: Jambo kuu katika msukumo wa maendeleo ya elimu ni ubunifu na uvumbuzi. Kutoa nafasi kwa ubunifu na fikra bunifu zenye mwelekeo chanya, ambazo ni miongoni mwa nguzo kuu za ukuaji na upanuzi katika elimu zote au nyingi, ni jambo muhimu sana.
Vilevile, kunahitajika ujasiri wa kisayansi wa kubuni, kuunda na kuvumbua, pamoja na kuongeza kujiamini kwa mtu binafsi na taifa ili kujaribu njia mpya ambazo hazijawahi kutumika. Kuweka motisha zinazokubalika na zinazovutia kwa kila mtu anayeweza kuwasilisha ubunifu wenye manufaa kutasaidia kuandaa mazingira yanayowezesha jambo hili.
Nne: Kujitegemea katika kutatua matatizo ya kisayansi, kuweka miundombinu na kuondoa vikwazo vikuu vya kiteknolojia vinavyozuia shughuli na utendaji katika maeneo yaliyo nje ya mipaka ya nchi, kutaunda mchanganyiko wa uimara wa uwezo wa ndani na kufungua upeo wa shughuli katika kiwango cha kimataifa.
Tano: Kuwapa nafasi watu wenye vipaji katika taaluma za majaribio na za vitendo, ikiwa ni pamoja na kuunganisha viwanda na vyuo vikuu tangu miaka ya mwanzo ya masomo ya chuo kikuu, pamoja na kurahisisha uanzishaji na uendeshaji wa biashara zinazotegemea maarifa ya kisayansi, kuna nafasi muhimu katika kutumia elimu na kukuza wasomi mahiri. Kuelekeza uwezo wa sayansi na teknolojia ya nchi katika mwelekeo mmoja, na kuimarisha uhusiano kati ya wasomi mahiri, vituo vya sayansi na utafiti, kampuni zinazotegemea maarifa ya kisayansi, viwanda na hata kampuni changa, sambamba na kuungwa mkono na taasisi za serikali katika mnyororo mzima wa maarifa hadi matumizi ya bidhaa, kunaweza kuleta matokeo makubwa.
Juhudi hizo zinapaswa kuelekezwa katika masuala muhimu ya sasa na ya baadaye ya nchi, kuanzia maji, udongo, chakula na nishati hadi akili unde. Hatua hiyo inaweza kuunganisha na kuhamisha shughuli za walimu na wanafunzi kutoka katika maabara za vyuo vikuu na vituo vya utafiti hadi kwenye karakana na viwanda. Ukuaji wa haraka na wa kiwango kikubwa utafanikiwa pale ambapo manufaa ya kiuchumi na soko la kibiashara la bidhaa na huduma zitakapounganishwa na motisha na azma ya wasomi mahiri. Hali hiyo itaunda uhusiano endelevu na wa kudumu kati ya taasisi za elimu na utafiti, sekta ya viwanda na soko la walaji.
Vilevile, ushiriki wa moja kwa moja na wenye ufanisi wa wasomi mahiri kutoka katika taaluma mbalimbali za nadharia na majaribio, katika vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya dini, katika ngazi za kupanga mipango na kuunda sera, utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi. Viongozi wana wajibu wa kutumia kwa kiwango kikubwa uwezo wa mtu mmoja mmoja, busara na hekima ya pamoja ya wasomi mahiri waliojitolea. Ikiwa njia hii itafuatwa kwa usahihi, kitovu na vituo vikuu vya maarifa, hasa katika baadhi ya matawi ya sayansi za msingi, vitahamia hatua kwa hatua kutoka nchi za Magharibi kwenda Iran.
Katika miaka isiyo mingi ijayo, nchi hii itakuwa kitovu cha marejeo ya kisayansi na kiteknolojia. Aidha, lengo lililotajwa hapo awali na Kiongozi wetu mwenye hekima na shahidi mtukufu, Mwenyezi Mungu ainyanyue daraja yake, la kuifanya lugha ya Kiajemi kuwa miongoni mwa lugha zinazotumika kama marejeo ya kisayansi duniani, litafikiwa.
Inshaallah, kwa baraka za damu ya mashahidi waliotoa maisha yao katika nyanja za umahiri, na kwa dua njema za bwana na kiongozi wetu, Imam Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake, msukumo wa kina na wa kasi wa kisayansi wa wasomi mahiri na watu wenye hekima wa taifa, pamoja na maendeleo ya Iran katika nyanja zote ili izidi kuwa imara, vitafanikishwa na kufungua njia ya kufikia ustaarabu mpya wa Kiislamu na Kiirani.
Sayyid Mujtaba Hussein Khamenei
4 Aban 1405 Hijria Shamsia/ 27 Oktoba 2026
Maoni yako