Jumatatu 26 Oktoba 2026 - 08:00
Kusimama Imara Mbele ya Vitisho vya Adui ni Dhihirisho la Utukufu wa Mwenyezi Mungu / Dua ya Makarimul-Akhlaq ni Mpango wa Kumlea Mwanadamu Mwenye Kumjua Mwenyezi Mungu

Ayatullah Jaafar Subhani, alipokuwa akifafanua nafasi ya Dua ya Makarimul-Akhlaq ya Imam Sajjad (as) katika kumlea mwanadamu mkamilifu, aliitaja dua hiyo kuwa ni mkusanyiko wenye thamani kubwa kwa ajili ya kukuza maarifa ya Mwenyezi Mungu, tabia njema, pamoja na kupandisha daraja za imani na yakini.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jaafar Subhani, katika darsa ya kwanza ya maadili ya mwaka mpya wa masomo iliyofanyika katika msikiti wa Taasisi ya Imam Swadiq (as), mjini Qom Iran, alifafanua nafasi ya Dua ya Makarimul-Akhlaq ya Imam Sajjad (as) katika malezi ya mwanadamu mkamilifu. Aliitaja dua hiyo kuwa ni mkusanyiko wenye thamani kubwa kwa ajili ya kukuza maarifa ya Mwenyezi Mungu, tabia njema na kupandisha daraja za imani na yakini. Aidha, alifafanua vipengele vya mwanzo vya dua hiyo, nafasi ya kumswalia Mtume Mtukufu (saww), daraja tatu za yakini na sifa za watu wamchao Mwenyezi Mungu.

Dua ya Makarimul-Akhlaq: Mpango wa Kumlea Mwanadamu Mwenye Kumjua Mwenyezi Mungu

Ayatullah Subhani aliongeza kuwa: Dua ya Makarimul-Akhlaq ni miongoni mwa dua zenye athari kubwa na zenye kujenga, zinazopatikana katika kitabu cha Swahifa Sajjadiyya, Dua hii ni dua ya ishirini katika kitabu hicho, ina mambo mengi na ikiwa Mwenyezi Mungu atatuwezesha kuifafanua, tutaweza kunufaika na maarifa yake yenye thamani kubwa.

Akizungumzia mazingira ya kijamii katika zama za Imam Sajjad (as), aliendelea kusema: Imam Ali bin Hussein (as) aliishi katika kipindi ambacho Ahlul-Bayt (as) walikuwa wamepata nafasi ya pekee miongoni mwa watu, hata kwa mtazamo wa wapinzani wao. Hii ni kwa sababu kuuawa kishahidi Imam Hussein (as) kulikuwa na athari mbaya sana katika namna watu walivyoutazama utawala wa Bani Umayya na tawala zao.

Watu walikuwa wakijiuliza ni kwa kiwango gani tawala hizo zilikuwa zimejitenga na njia sahihi ya kibinadamu na kimaadili, kiasi cha kuwaua watu wa familia ya Utume kwa namna ile, kukata vichwa vya mashahidi kutoka kwenye miili yao na kuwachukua wanawake kuwa mateka.

Marji' huyu wa kidini aliongeza kuwa: Matukio hayo yalikuwa na athari mbaya katika mtazamo wa jamii ya Kiislamu kuhusu utawala wa Bani Umayya. Kwa hakika, watu walikuwa wameanza kuelekea kwa Ahlul-Bayt (as), na nafasi yao ya kijamii ilikuwa imeanza kuzingatiwa zaidi kuliko hapo awali, bila shaka Ahlul-Bayt (as) walikuwa na cheo cha Mwenyezi Mungu tangu mwanzo, lakini baada ya tukio la Ashura, mwelekeo wa wananchi kwao pia uliongezeka.

Nafasi ya Kijamii ya Imam Sajjad (as) Baada ya Tukio la Ashura

Ayatullah Subhani, alipokuwa akifafanua nafasi ya Imam Sajjad (as) katika jamii ya wakati huo, alirejelea tukio la kugusa Jiwe Jeusi (Hajar al-Aswad), akasema: Kwa mfano, Imam Ali bin Hussein (as) alipotaka kuligusa Jiwe Jeusi, licha ya msongamano mkubwa wa watu, watu walifungua njia kwa ajili yake. Wakati huohuo, Hisham bin Abdul-Malik alikuwa pia mahali hapo akisubiri watu wamfungulie njia ili aweze kuligusa Jiwe Jeusi, lakini watu hawakumruhusu, Imam Ali bin Hussein (as) alipoingia, watu walijitenga na kumfungulia njia, hivyo akaweza kuligusa Jiwe Jeusi.

Aliendelea kusema: Watu waliokuwapo walimuuliza Hisham kuhusu mtu huyo alikuwa nani, lakini Hisham alijifanya kwamba hamfahamu na akasema kuwa hamjui, katika mkusanyiko huo alikuwapo Farazdaq, ambaye alitunga mashairi ya kumtambulisha Imam na kuieleza vizuri nafasi yake.

Miongoni mwa mashairi aliyoyatunga katika kumsifu Imam huyo ni:

«هَذَا الَّذِي تَعْرِفُ الْبَطْحَاءُ وَطْأَتَهُ * وَالْبَيْتُ يَعْرِفُهُ وَالْحِلُّ وَالْحَرَمُ»

Huyu ndiye ambaye ardhi inatambua nyayo zake, na Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu inamfahamu, kama vile maeneo ya nje ya Haram na maeneo matakatifu ya Haram yanavyomfahamu. Kwa hakika, kupitia mashairi hayo, Farazdaq alisisitiza nafasi inayotambulika ya Imam Ali bin Hussein (as).

Ayatullah Subhani alibainisha kuwa: Baada ya utawala kuhamia kutoka katika tawi la Sufyani la Bani Umayya, katika zama za Yazid, kwenda katika tawi la Marwani, na Abdul-Malik Marwan kushika madaraka, Imam Ali bin Hussein (as) aliendelea kuwa na nafasi ya pekee miongoni mwa watu. Katika mazingira hayo hayo, aliendelea na shughuli zake katika nyanja za Uimamu na jihadi.

Kueneza Maarifa ya Dini Kupitia Dua za Imam Sajjad (as)

Marjaa huyu wa kidini, akizungumzia mojawapo ya shughuli muhimu za Imam Sajjad (as), alisema: Miongoni mwa shughuli muhimu za Imam huyo ni mkusanyiko wa dua alizokuwa akiziandaa na kuzikabidhi kwa wanafunzi wake. Imam alikuwa akiwafundisha dua hizo wanafunzi wake, nao walikuwa wakieneza maarifa hayo katika jamii kupitia mafundisho hayo, na hivyo kuathiri watu. Bila shaka, kupitia njia hii, Imam pia aliweza kushughulikia ukweli na mambo aliyokusudia, pamoja na kueneza maarifa ya kidini katika jamii.

Aliongeza kuwa: Lengo kuu la dua nyingi za Imam Sajjad (as) ni kumlea mwanadamu mwenye maarifa ya Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, hapa neno arifu halimaanishi tu maana yake ya kitaalamu inayotumiwa na makundi mbalimbali, bali linakusudiwa kumaanisha mwanadamu anayemjua Mwenyezi Mungu kwa hakika na anayewafahamu Mitume, huku akiwa amepambwa pia kwa tabia njema.

Dua zote zilizomo katika mkusanyiko huu zinaelekea katika lengo hilo hilo: kumlea mwanadamu mwenye maarifa ya Mwenyezi Mungu na kumkuza mwanadamu mkamilifu katika maana yake halisi.

Ayatullah Subhani alisema kuwa shughuli hii yenyewe ilikuwa ni huduma kubwa aliyoitoa Imam Sajjad (as) katika kipindi hicho. Hata hivyo, shughuli zake hazikukomea katika eneo hilo pekee, bali maisha yake yalishuhudia pia hatua nyingine.

Alisema: Imam Sajjad (as) alikuwa akiwahudumia mafukara na wahitaji, akijibu maswali ya watu na kutoa huduma nyingine za kijamii ambazo zimeelezwa katika taarifa zinazohusu maisha yake.

Imam Sajjad (as) Alikuwa na Uwezo Mkubwa na Roho ya Kuwahudumia Watu

Ayatullah Subhani, akisisitiza umuhimu wa kumfahamu Imam Sajjad (as) kwa usahihi, alisema: Hatutakiwi kufikiri kwamba Imam alikuwa mtu asiye na uwezo au dhaifu. Wakati mwingine, baadhi ya wahadhiri wa majukwaani hutumia kauli kama “Imam mwenye homa.” Hata hivyo, ikiwa kauli hii itatolewa kwa namna inayomchora Imam kuwa mtu dhaifu na asiye na uwezo, basi si kauli inayofaa.

Imam Sajjad (as) alikuwa mtu mwenye uwezo, aliyekomaa na mwenye nguvu pamoja na ustahimilivu. Usiku, alikuwa akibeba kiasi cha chakula mabegani mwake na kukipeleka katika nyumba za wahitaji. Jambo kama hilo haliwezi kufanywa na mtu asiye na uwezo. Badala yake, linaonesha uwezo wake, roho yake ya kuhudumia watu na kujitolea kwake kuwasaidia wahitaji. Imam alikuwa akifanya hivyo kwa namna ambayo haikuacha nafasi ya ria au kujionyesha mbele ya watu.

Aliongeza kuwa: Ikiwa tutaweza kuieleza na kuifafanua Dua ya Makarimul-Akhlaq kwa usahihi, huenda tukaweza kueleza sehemu ya tabia na mwenendo wa Imam Ali bin Hussein (as) kwa marafiki na wasikilizaji wetu, na kuwafahamisha maarifa haya yenye thamani kubwa.

Dua ya Makarimul-Akhlaq Inaanza kwa Kumswalia Mtume na Familia Yake

Ayatullah Subhani aliendelea na mada yake kuu kwa kueleza maneno ya kwanza ya Dua ya Makarimul-Akhlaq, akasema:

Maneno ya kwanza ya dua hii ni:

«بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ، اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَآلِهِ، وَبَلِّغْ بِإِيمَانِي أَكْمَلَ الْإِيمَانِ، وَاجْعَلْ يَقِينِي أَفْضَلَ الْيَقِينِ، وَانْتَهِ بِنِيَّتِي إِلَى أَحْسَنِ النِّيَّاتِ...»

Tafsiri: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Ewe Mwenyezi Mungu! Mteremshie rehema Muhammad na familia yake, ifikishe imani yangu katika daraja ya ukamilifu wa juu kabisa wa imani, ifanye yakini yangu kuwa yakini bora zaidi, na fikisha nia yangu katika nia zilizo bora zaidi...

Imam Sajjad (as) anaanza dua yake kwa kumswalia Mtume. Kwa hakika, dua zake zote zinaanza kwa kumswalia Mtume. Sasa swali linalojitokeza ni: Kwa nini Imam anaanza dua kwa kumswalia Mtume?

Alibainisha kuwa katika riwaya imeelezwa kwamba; hakuna dua kama kumswalia Mtume kwa sababu swala hiyo ni dua ambayo Mwenyezi Mungu huikubali. Mtu yeyote anaposema, “اللهم صل على محمد وآل محمد” — “Ewe Mwenyezi Mungu, mteremshie rehema Muhammad na familia ya Muhammad” — Mwenyezi Mungu huikubali dua hiyo.

Alisisitiza kuwa kumswalia Mtume ni dua isiyokataliwa, na jambo hili limesisitizwa pia katika riwaya. Sasa, ikiwa mtu atamuomba Mwenyezi Mungu haja yake baada ya kumswalia Mtume, nini kitatokea?

Marji' huyu wa kidini aliongeza kuwa: Katika riwaya imeelezwa kwamba mtu akianza dua yake kwa kumswalia Mtume, kisha akaomba haja yake, Mwenyezi Mungu husema: Haifai kwangu kuikubali dua ya kwanza na kuikataa dua ya pili, kwa sababu nimeikubali dua ya kwanza, na matakwa ya rehema na huruma Yangu yanataka niikubali pia dua inayofuata.

Kwa hiyo, kumswalia Mtume mwanzoni mwa dua kuna nafasi ya pekee, na kunaweza kuwa utangulizi wa kuomba haja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu mtu huanza dua yake kwa dhikri ambayo riwaya zimesisitiza kuwa inakubaliwa.

Tofauti Kati ya Kumswalia Mtume Muhammad (saww) na Matumizi ya Maneno ya Qur’ani Kuhusu Mitume Wengine

Ayatullah Subhani, akizungumzia tofauti kati ya kumswalia Mtume Muhammad (saww) na maneno yanayotumiwa kuhusu Mitume wengine, alisema: Jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa katika suala hili ni tofauti kati ya kumswali Mtume Muhammad (saww) na maneno yanayotumiwa kuhusu Mitume wengine. Katika Qur’ani Tukufu tunasoma:

«سَلَامٌ عَلَى إِبْرَاهِيمَ»

Amani iwe juu ya Ibrahim.

Pia tunasoma:

«سَلَامٌ عَلَى مُوسَى وَهَارُونَ»

Amani iwe juu ya Musa na Harun.

Vilevile:

«سَلَامٌ عَلَى إِلْ يَاسِينَ»

Amani iwe juu ya familia ya Yasin.

Hata hivyo, tunapozungumzia Mtume Muhammad (saww), suala hili linakuwa tofauti na lilivyo kwa Mitume wengine. Mwenyezi Mungu anasema:

«إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ»

Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika Wake wanamswalia Nabii.

Aliongeza kuwa: Katika aya hii, Mwenyezi Mungu anazungumzia swala Yake na ya Malaika Wake kwa Mtume, kisha katika sehemu inayofuata ya aya hiyo anawafahamisha Waumini pia wamswalie Mtume.

Kwa hiyo, kumswalia Mtume Muhammad (saww) kunatofautiana na maneno yaliyotumiwa kuhusu Mitume wengine. Kuhusu Mitume wengine, maneno kama “Amani iwe juu ya Ibrahim” yametumiwa. Lakini kuhusu Mtume Muhammad (saww), Mwenyezi Mungu anasema kwamba Yeye mwenyewe pamoja na Malaika Wake wanamswalia Mtume, na anawaamuru watu nao wafuate amri hii ya Mwenyezi Mungu. Jambo hili linaonesha nafasi ya pekee ya Mtume Muhammad (saww) na tofauti ya daraja yake na Mitume wengine katika suala hili.

Kusisitiza Namna ya Kumswalia Mtume Iliyofundishwa na Mtume Mwenyewe (saww)

Ayatullah Subhani, akizungumzia mabadiliko yaliyofanyika katika namna ya kumswalia Mtume baada ya kufariki kwake, alisema: Kwa masikitiko, baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad (saww), Bani Umayya, Bani Marwan na Bani Abbas waliingilia hata namna ya kumswalia Mtume na kufanya mabadiliko katika jinsi ya kuitamka swala hiyo. Namna ya kumswalia Mtume iliyofundishwa na Mtume Muhammad (saww) imenukuliwa katika Sahih Bukhari, na huenda pia katika Sahih Muslim.

Aliendelea kusema: Katika riwaya hizi imeelezwa kwamba watu walimuuliza Mtume Muhammad (saww):

«يَا رَسُولَ اللَّهِ، كَيْفَ نُصَلِّي عَلَيْكَ؟»

Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tunakuswaliaje?

Mtume Muhammad (saww), katika majibu yake, yaliwafundisha namna ya kumswalia kwa kusema:

«اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَآلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَآلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ.»

Ewe Mwenyezi Mungu! Teremsha rehema kwa Muhammad na familia ya Muhammad, kama Ulivyomteremshia rehema Ibrahim na familia ya Ibrahim. Hakika Wewe ni Mwenye kusifiwa, Mtukufu.

Kauli hii imenukuliwa katika Sahih Bukhari, kwa mujibu wa riwaya hiyo, Mtume Muhammad (saww) aliwafundisha watu namna ya kumswalia kwa kutaja jina na nafasi ya familia yake. Kwa hiyo, kumswalia Muhammad na familia ya Muhammad ndiyo namna ya swala iliyopokewa kutoka kwa Mtume mwenyewe (saww).

Marji' huyu wa kidini, akieleza kwamba katika vitabu vya Ahlus-Sunna mara nyingi maneno “Swallallahu alayhi wa aalihi” hayaonekani, alisisitiza kuwa katika vitabu vilivyochapishwa nchini Misri na maeneo mengine, mara nyingi hutumiwa maneno “Swallallahu alayhi wa sallam.”

Hata katika sehemu ambazo majina ya Ahlul-Bayt (as) yanatajwa, majina ya Maswahaba pia huongezwa. Kwa mfano, husemwa:

«اللهم صل على محمد وآل محمد وأصحابه»

Au hutumiwa kauli:

«وعلى آله وأصحابه»

Kwa kufanya hivyo, Ahlul-Bayt na Maswahaba huwekwa pamoja katika kauli hiyo.

Aliendelea kurejelea mawasiliano ya barua aliyokuwa nayo na mmoja wa wanazuoni wa Ahlus-Sunna, akasema: Nchini Qatar kuna mwanazuoni mkubwa wa fiqhi anayeitwa Haj Sheikh Ali Qaradaghi, ambaye nimekuwa nikiandikiana naye barua. Yeye ni miongoni mwa watu ambao wakati wa vita vya Marekani dhidi ya Iran, walitoa fatwa ya jihadi dhidi ya Marekani, kwa kushirikiana na wanazuoni hamsini wa Ahlus-Sunna. Mtu mwenye nafasi kama hiyo ana hadhi ya kielimu na kidini. Ayatullah Subhani, akieleza kwamba Qaradaghi ipo katika nchi ya Azerbaijan na pia katika nchi ya Iraq, alisema: Mtu ninayemkusudia ni Muiraqi.

Aliendelea kusema: Nilimwandikia barua pia na kusisitiza kwamba mnapaswa kukabiliana na uzushi katika dini. Uzushi unaokusudiwa hapa ni kwamba Mtume Muhammad (saww), alipoulizwa na watu kuhusu namna ya kumswalia kwa swali, “Tunakuswaliaje?”, aliwafundisha maneno yafuatayo:

«اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَآلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَآلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ»

Hata hivyo, katika baadhi ya vitabu na matini, kauli hii imenukuliwa kwa namna nyingine, au majina ya Ahlul-Bayt yamewekwa pamoja na majina ya Maswahaba.

Aliendelea kusema: Katika barua niliyoandikiwa kujibu barua yangu, ilisisitizwa kwamba nilichosema ni sahihi na kwamba kuna riwaya mbili sahihi zinazopokea kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) namna hiyo hiyo ya swala niliyoieleza. Kwa hiyo, tunapaswa kukabiliana na uzushi huu hatua kwa hatua na kufufua namna ya kumswalia Mtume Muhammad (saww) ambayo alifundisha mwenyewe.

Marji' huyu wa kidini aliongeza kuwa: Suala hili ni muhimu na lina nafasi kubwa. Inshaallah, tutaieleza haki kupitia dua na swala kwa Mtume. Dua zote za Imam Ali bin Hussein (as), hata Dua ya Makarimul-Akhlaq na Dua ya Mardhiyul-Af'al, huanza kwa kumswalia Mtume. “Ifikishe Imani Yangu Katika Daraja ya Juu Zaidi ya Ukamilifu wa Imani”

Ayatullah Subhani aliendelea kufafanua kipengele kinachofuata cha Dua ya Makarimul-Akhlaq, akasema: Baada ya kumswalia Mtume, Imam Sajjad (as) anaendelea na dua yake kwa kusema:

«اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَآلِ مُحَمَّدٍ، وَبَلِّغْ بِإِيمَانِي أَكْمَلَ الْإِيمَانِ.»

Ewe Mwenyezi Mungu! Mteremshie rehema Muhammad na familia ya Muhammad, na uifikishe imani yangu katika daraja ya juu kabisa ya ukamilifu wa imani.

Ombi la kwanza ambalo Imam Sajjad (as) analitoa katika dua hii ni kwamba Mwenyezi Mungu aifikishe imani yake katika daraja la ukamilifu. Alibainisha kuwa: Kutokana na maneno haya, inafahamika kwamba imani ina daraja na viwango mbalimbali, na haikomei katika daraja moja tu. Imam anaposema, “Na uifikishe imani yangu katika daraja ya juu kabisa ya ukamilifu wa imani,” inakuwa wazi kwamba imani inaweza kutoka katika daraja moja na kupanda hadi daraja la juu zaidi. Hivyo, mwanadamu anapaswa kuendelea katika njia ya kuikamilisha imani yake.

Marji' huyu wa kidini, akizungumzia daraja za imani, alisema: Mara nyingi husemwa:

«أُصُولُ الْإِسْلَامِ ثَلَاثَةٌ: الْإِقْرَارُ بِاللَّهِ، وَالْإِقْرَارُ بِالرَّسُولِ، وَالْإِقْرَارُ بِالْمَعَادِ»

Maana yake ni kwamba misingi ya Uislamu ni mitatu: kukiri kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, kukiri Utume wa Mtume na kukiri kufufuliwa baada ya kifo.

Tunakubali jambo hili, lakini daraja kama hii ni daraja ya mwanzo ya imani, na imani haikomei katika kiwango hicho, katika daraja ya juu zaidi huongezwa pia:

«وَالْقِيَامُ بِالْأَعْمَالِ»

Maana yake ni kutekeleza matendo, matendo pia yanapaswa kuambatanishwa na imani, ikiwa matendo hayataambatanishwa na imani, imani ya mwanadamu itakuwa kavu na yenye upungufu.

Ayatullah Subhani aliendelea kusema: Katika baadhi ya riwaya, zikiwemo zile zilizomo katika kitabu Uyun Akhbar al-Ridha, imeelezwa:

«الْإِيمَانُ مَعْرِفَةٌ بِالْقَلْبِ، وَإِقْرَارٌ بِاللِّسَانِ، وَعَمَلٌ بِالْأَرْكَانِ.»

Imani ni utambuzi wa moyo, kukiri kwa ulimi na kutenda kwa viungo vya mwili.

Riwaya hii imenukuliwa katika juzuu ya kwanza ya kitabu Uyun Akhbar al-Ridha, ukurasa wa 136.

Kwa hiyo, pamoja na kuwa na utambuzi na maarifa ya moyoni, mwanadamu anapaswa kukiri kwa ulimi na kushikamana na mafundisho ya Uislamu kupitia matendo yake, kutekeleza nguzo za Uislamu kunapaswa kufanyika kwa namna ambayo mwanadamu anazingatia amri za dini hata katika mambo madogo, kwa kadiri ya uwezo na nafasi aliyonayo, hadi mwisho wa uwezo wake.

Ayatullah Subhani aliendelea kusema: Imam Sajjad (as) anapomuomba Mwenyezi Mungu aifikishe imani yake katika daraja ya juu kabisa ya ukamilifu, hakusudii kukiri tu kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, Utume wa Mtume na kufufuliwa baada ya kifo. Bali imani inapaswa kufikia ukamilifu kupitia utambuzi wa moyo, kukiri kwa ulimi na kutekeleza nguzo za dini.

Uhusiano Kati ya Imani na Matendo Mema Katika Qur’ani Tukufu

Marji' huyu wa kidini, akizungumzia msisitizo wa Qur’ani Tukufu kuhusu kuambatana imani na matendo mema, alisema: Qur’ani Tukufu pia inasisitiza uhusiano kati ya imani na matendo mema, na katika aya nyingi inayaweka mambo haya mawili pamoja:

«إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ»

Isipokuwa wale walioamini na wakatenda matendo mema.

Kwa mujibu wa kauli hii ya Qur’ani, imani na matendo mema vimeelezwa pamoja. Imani ina daraja la mwanzo, na matendo mema yanapaswa kuambatanishwa nayo ili mwanadamu aweze kusonga mbele katika njia ya kukua na kufikia ukamilifu.

Akiuliza kama kiwango hicho pekee kinatosha, alisema: Je, ikiwa mwanadamu atakiri kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, Utume wa Mtume na kufufuliwa baada ya kifo, na pia akatekeleza amri za dini, atakuwa amefikia daraja ya juu kabisa ya imani?

Jibu ni kwamba imani ina daraja nyingine pia, na mwanadamu anaweza kufikia viwango vya juu zaidi katika njia ya utambuzi na yakini.

Daraja Tatu za Yakini: Ilmul-Yaqin, Aynul-Yaqin na Haqqul-Yaqin

Ayatullah Subhani, akifafanua daraja za juu zaidi za imani, alirejelea aya za Suratul-Takathur, akasema: Ili kufahamu daraja za juu zaidi za imani, tunaweza kurejelea Suratul-Takathur. Mwenyezi Mungu anasema katika sura hii:

«كَلَّا لَوْ تَعْلَمُونَ عِلْمَ الْيَقِينِ، لَتَرَوُنَّ الْجَحِيمَ.»

Sivyo hivyo! Lau mngejua kwa yakini ya elimu, bila shaka mngeiona Jahannamu.

Aya hizi zinaashiria Ilmul-Yaqin na zinaonesha kwamba yakini pia ina daraja mbalimbali. Kwa hiyo, imani haipaswi kubaki katika kiwango cha kukiri kwa ulimi au hata utambuzi na matendo ya nje tu. Badala yake, mwanadamu anapaswa kuendelea katika njia ya kufikia yakini na maarifa ya kina zaidi.

Aliendelea kusema: Daraja ya juu kabisa ya imani ni ile ambayo mwanadamu hufikia kiwango cha yakini kinachomwezesha kuona, akiwa bado katika dunia hii ukweli wa adhabu na Jahannamu ya Barzakh. Hata hivyo, kinachokusudiwa hapa si kuona Jahannamu ya Akhera, bali ni kuona Jahannamu ya Barzakh.

Kwa hiyo, ombi la Imam Sajjad (as) la kutaka imani ifikie daraja ya juu kabisa ya ukamilifu linamaanisha kwamba mwanadamu anapaswa kuendelea katika njia ya kuikamilisha imani yake na kupanda kutoka katika daraja za mwanzo za utambuzi na kukiri hadi katika daraja za juu zaidi za maarifa, yakini na matendo.

Alibainisha kuwa: Daraja ya juu kabisa ya imani inahusiana na watu wanaoutambua ukweli kwa namna ambayo wakati mwingine wanaweza kuona wakiwa bado katika dunia hii miali ya moto wa Jahannamu na hali ya Pepo. Hii pia ni mojawapo ya daraja za imani, ingawa si daraja la mwisho la yakini.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu:

«كَلَّا لَوْ تَعْلَمُونَ عِلْمَ الْيَقِينِ»

Sivyo hivyo! Lau mngejua kwa yakini ya elimu.

Pia anasema:

«لَتَرَوُنَّ الْجَحِيمَ»

Bila shaka mtaiiona Jahannamu.

Na anasema:

«ثُمَّ لَتَرَوُنَّهَا عَيْنَ الْيَقِينِ»

Kisha bila shaka mtaiona kwa yakini ya kuona kwa macho.

Aya hizi zinaashiria daraja za yakini, kwa kawaida wanazuoni huzigawa daraja za yakini katika viwango vitatu: Ilmul-Yaqin, Aynul-Yaqin na Haqqul-Yaqin.

Ayatullah Subhani aliongeza kuwa: Kuhusu moto, wakati mwingine mwanadamu husikia habari zake na kuambiwa kwamba ni kitu chenye miali na kinachozalisha joto, katika daraja hili, kupitia kusikia na kupata taarifa, mwanadamu hupata elimu kuhusu kuwepo moto, hii ndiyo Ilmul-Yaqin. Katika daraja la pili, mwanadamu huutazama moto kwa karibu, daraja hili huitwa Aynul-Yaqin, yaani mwanadamu anauona ukweli kwa macho yake mwenyewe.

Hata hivyo, Haqqul-Yaqin iko katika daraja la juu zaidi, kwa mfano mwanadamu anaukaribisha mkono wake karibu na moto na kuhisi joto lake, katika hali hii anatambua ukweli wa moto si kwa kusikia au kuutazama tu, bali kupitia uzoefu wa moja kwa moja. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba Ilmul-Yaqin, Aynul-Yaqin na Haqqul-Yaqin ni daraja tatu tofauti za utambuzi na yakini.

Kuomba Daraja Bora Zaidi ya Yakini Katika Dua ya Makarimul-Akhlaq

Ayatullah Subhani, akirejea tena vipengele vya Dua ya Makarimul-Akhlaq, alisema: Imam Sajjad (as) anasema katika Dua ya Makarimul-Akhlaq:

«وَبَلِّغْ بِإِيمَانِي أَكْمَلَ الْإِيمَانِ، وَاجْعَلْ يَقِينِي أَفْضَلَ الْيَقِينِ.»

Ifikishe imani yangu katika daraja ya juu kabisa ya ukamilifu wa imani, na uifanye yakini yangu kuwa yakini bora zaidi.

Katika kauli hii, Imam hakutosheka tu na kuomba kuongezewa imani, bali pia anamuomba Mwenyezi Mungu aifikishe yakini yake katika daraja bora zaidi.

Alisisitiza kuwa: Mwanadamu anapaswa kufikia daraja ya utakatifu, uchamungu na ibada za usiku katika njia ya imani na matendo, kiasi kwamba pazia ziondoke mbele ya macho yake na aweze kutambua ukweli ambao umefichika kwa watu wengine. Hali hii inaweza kufikia kiwango cha kumwezesha kuona, akiwa bado katika dunia hii ukweli fulani kuhusu Jahannamu ya Barzakh.

Maelezo ya Amirul-Muuminina (as) Kuhusu Wacha Mungu: Ni Kana Kwamba Wanaiona Pepo na Jahannamu

Marji' huyu wa kidini, akirejelea kipengele kimoja cha Nahjul-Balagha, alisema: Mtu mmoja alimwomba Amirul-Muuminina Ali (as) amwelezee watu wamchao Mwenyezi Mung, katika kumjibu Imam alianza kueleza sifa za watu wacha Mungu, na katika sehemu moja ya maelezo hayo akasema:

«فَهُمْ وَالْجَنَّةُ كَمَنْ قَدْ رَآهَا فَهُمْ فِيهَا مُنَعَّمُونَ، وَهُمْ وَالنَّارُ كَمَنْ قَدْ رَآهَا فَهُمْ فِيهَا مُعَذَّبُونَ.»

Wao na Pepo ni kama mtu ambaye tayari ameiona, kiasi kwamba ni kana kwamba wananeemeshwa ndani yake; na wao na Moto wa Jahannamu ni kama mtu ambaye tayari ameuuona, kiasi kwamba ni kana kwamba wanateswa ndani yake.

Watu wacha Mungu wana uhusiano na uelewa wa Pepo na Jahannamu kiasi kwamba ni kana kwamba wanaviona, wanaiona Pepo kana kwamba watu wa Peponi tayari wanafurahia neema zake, na wanaiona Jahannamu kana kwamba wale wanaoadhibiwa ndani yake tayari wamekumbwa na adhabu hiyo.

Aliendelea kusema: Kauli hii inaonesha kwamba mojawapo ya sifa za watu wacha Mungu ni kuwa na daraja ya juu ya imani na yakini. Ni daraja ambalo pazia za kughafilika huondoka, na mwanadamu hutambua ukweli uliofichika katika mtazamo wa kawaida.

Bila shaka, katika hali za kawaida, watu hawaoni ukweli huu kwa sababu kuna vizuizi vilivyowekwa mbele ya macho yao. Hata hivyo, baadhi ya watu, kupitia kujitakasa nafsi na kupanda katika daraja za imani, hufikia nafasi ambayo vizuizi hivyo huondolewa mbele yao.

Simulizi ya Mmoja wa Wafuasi wa Imam Swadiq (as) na Daraja ya Juu ya Uhakika

Ayatullah Subhani aliendelea kwa kurejelea simulizi kuhusu mmoja wa wafuasi waaminifu wa Imam Swadiq (as), akasema: Katika riwaya kuhusu mmoja wa wafuasi waaminifu wa Imam Swadiq (as), imesimuliwa kwamba kulikuwa na tanuri lililokuwa limewashwa mbele ya Imam, Imam akamwambia mmoja wa wafuasi wake aingie ndani ya tanuri hilo. Mtu huyo alisimama bila kusita, akaelekea kwenye tanuri na kukaa ndani yake, lakini hakupata madhara wala kuungua.

Imani inayomfikisha mwanadamu katika daraja ya yakini ya namna hii humfanya atende kwa namna inayotofautiana na hesabu na tathmini za kawaida zinazoonekana kwa macho.

Kujitakasa Nafsi na Kuacha Baadhi ya Starehe: Njia ya Kupandisha Daraja za Imani

Marji' huyu wa kidini huku akisisitiza ugumu wa kufikia daraja za juu za yakini, alisema: Hapa tunapaswa kuzingatia kwamba kufikia daraja kama hii si jambo rahisi, nafasi hii inahitaji kujitakasa nafsi, kufanya ibada za usiku, kuvumilia magumu, kujinyima baadhi ya mambo kwa hiari na kuacha baadhi ya starehe.

Mwanadamu anapaswa kuachana na baadhi ya matamanio ya nafsi yake ili kuandaa mazingira ya kufikia daraja za juu zaidi za imani na yakini. Kwa hiyo, tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie imani na yakini ya namna hii; imani ambayo haitabaki katika kiwango cha madai na kukiri kwa ulimi tu, bali itaingia ndani kabisa ya nafsi ya mwanadamu na kuathiri tabia na maisha yake.

Ayatullah Subhani aliendelea kueleza jambo jingine kuhusu sifa za watu wacha Mungu, ambazo pia zimetajwa katika maneno ya Amirul-Muuminina (as):

«عَظُمَ الْخَالِقُ فِي أَنْفُسِهِمْ، فَصَغُرَ مَا دُونَهُ فِي أَعْيُنِهِمْ.»

Muumba amekuwa Mkuu katika nafsi zao, na kila kitu kisichokuwa Yeye kimekuwa kidogo machoni mwao.

Alieleza kwamba kauli hii inaashiria mojawapo ya sifa muhimu zaidi za watu wacha Mungu. Utukufu wa Mwenyezi Mungu hupata nafasi kubwa katika nafsi na roho zao, kiasi kwamba mambo ya kidunia na ishara za nguvu na utajiri hupoteza thamani na mvuto wake wa awali mbele ya utukufu wa Mwenyezi Mungu. Kwa hakika, mtu mcha Mungu ni yule ambaye Mwenyezi Mungu ni Mkuu machoni pake, huku kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu kikionekana kidogo mbele yake. Kauli ya Amirul-Muuminina (as) inaeleza maana hii kwa uwazi kabisa: Mwenyezi Mungu ana utukufu mkubwa katika nafsi na roho za watu wacha Mungu, na kila kitu kisichokuwa Yeye huonekana kidogo machoni mwao.

Kusimama Imara Mbele ya Vitisho vya Adui ni Dhihirisho la Utukufu wa Mwenyezi Mungu

Marji' huyu wa kidini aliendelea kwa kurejelea simulizi moja kutoka katika zama za utawala wa Bani Marwan, akasema: Katika kipindi cha utawala wa Bani Marwan, Ziyad bin Abihi alikuwa mjini Kufa na akamwita mmoja wa wafuasi wa Amirul-Muuminina (as) kwa nia ya kumuua. Alipomwita mtu huyo mbele yake, mwanamume huyo alisema kwamba bwana wake alikuwa amemjulisha kuwa Ziyad angemuua kwa namna hiyo: angemkata mikono na miguu, kisha angemtundika msalabani. Ziyad bin Abihi akamjibu kwamba, kwa hakika, angefanya mambo hayo yote. Jambo la kuzingatiwa katika simulizi hili ni kwamba mwanamume huyo, hata alipokuwa mbele ya adui yake, alizungumzia yaliyokuwa yakimsubiri siku za usoni na kueleza yale aliyoyasikia kutoka kwa bwana wake.

Ayatullah Subhani aliongeza kuwa: Mfano huu unaweza kuchunguzwa katika muktadha wa mazungumzo kuhusu utukufu wa Mwenyezi Mungu katika nafsi za watu wacha Mungu. Hii ni kwa sababu mtu ambaye Mwenyezi Mungu ni adhimu machoni mwake haingiwi na hofu wala kuyumba mbele ya vitisho vya kidunia na nguvu za nje za maadui.

Utambuzi wa Kiroho na Kuepuka Kuchukua Mali za Watu Bila Ruhusa: Simulizi la Ayatullah Haeri

Ayatullah Subhani alirejelea simulizi kuhusu marehemu Ayatullah Haeri, alisema: Imesimuliwa kwamba Ayatullah Haeri aliwahi kwenda katika bustani moja, alipoona zabibu za bustani hiyo, alitamani kuzila. Mtu mmoja aliyetambua jambo hilo alivuka ukuta wa jirani, akachuma kiasi cha zabibu na kuziweka mbele ya Ayatullah Haeri, hata hivyo Ayatullah Haeri hakula hata zabibu moja. Sababu ya tabia hiyo ilikuwa nini? Katika simulizi hii, sababu imetajwa kuwa ni yakini na utambuzi wa ndani wa kiroho aliokuwa nao. Yaani, alitambua kwamba zabibu hizo zilikuwa mali ya mtu mwingine na kwamba haikuruhusiwa kuzichukua na kuzila bila ruhusa ya mwenye bustani. Kwa mtazamo wetu, tunachoona ni vishada vichache tu vya zabibu, lakini yeye alikuwa akitambua undani na ukweli wa jambo hilo.

Umuhimu wa Kuendelea Kupanda Kutoka Imani ya Mwanzo Hadi Daraja za Juu za Yakini

Katika kuhitimisha hoja zilizojadiliwa katika darsa hiyo ya maadili, Ayatullah Subhani alisema: Kwa hiyo, tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Imam Ali bin Hussein (as) anavyoomba katika Dua ya Makarimul-Akhlaq, aifikishe imani yetu katika daraja ya juu kabisa ya ukamilifu na ainyanyue yakini yetu hadi katika daraja bora zaidi la yakini.

Kupitia dua hii, Imam Sajjad (as) anatufundisha kwamba mwanadamu hapaswi kuridhika na daraja ya imani aliyofikia, bali anapaswa kuendelea daima katika njia ya kukua, kupata maarifa, kuwa mcha Mungu na kuimarisha yakini yake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha