Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Maleki, Naibu Mkuu wa Hawza ya Qom, amekuwa akifafanua maarifa na ujumbe wa Suratul-Kawthar katika mfululizo wa vikao maalumu.
Katika mjadala kuhusu Suratul-Kawthar, nukuu zaidi ya ishirini na tano kutoka kwa wafasiri wa Qur’ani zimetolewa. Inaonekana kwamba wakati mwingine, kwa kuwasilisha mitazamo hiyo, jambo kuu kuhusu tukio lililosababisha kushuka sura hii husahaulika. Hii ni kwa sababu baadhi ya watu husema kuwa neno Kawthar linamaanisha Qur’ani, hekima, akili au bwawa la Kawthar. Hata hivyo, Suratul-Kawthar yenyewe inafafanua maana ya neno hili, pale Mwenyezi Mungu Mtukufu anaposema:
«إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ»
Hakika anayekuchukia ndiye aliyekatika kizazi na asiye na mwendelezo.
Kauli hii, «إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ», iliyokuja mwishoni mwa sura hii, inahusiana moja kwa moja na mazingira yaliyosababisha kushuka kwake. Tukio lilikuwa hivi: Maadui wa Mtume (saww) walikuwa wakisema kwamba kwa sababu hakuwa na mtoto wa kiume, basi alikuwa abtar, yaani, mtu ambaye kizazi chake kingekatika na baada yake kusingebaki mtu wa kuendeleza njia yake.
Kupitia kushuka sura hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka kumpa Mtume Wake mwenye utukufu mkubwa bishara mbili za kimuujiza. Ya kwanza ni kwamba angejaliwa Kawthar, na ya pili ni kwamba adui yake ndiye angekuwa abtar, asiye na mwendelezo wa kizazi na urithi.
Kwa hiyo, Mtume (saww) alijaliwa Kawthar, huku maadui wake wakawa ndio waliokosa mwendelezo wa urithi wao na wakashindwa kuhifadhi nafasi na ushawishi wao katika historia. Bani Umayya na Bani Abbas, licha ya kuwa na wafuasi wengi, nguvu na rasilimali nyingi, hawakuweza kuacha urithi wa kiroho wenye kudumu na thamani kama ule ulioachwa na Mtume (saww).
Leo hii, hatuoni athari ya mwendelezo wa kiroho wala nafasi yao ya zamani katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo, jina na njia ya Mtume mwenye utukufu mkubwa vimeenea katika sehemu zote duniani.
Mwendelezo na upanuzi huu ulianzia kwa Ahlul-Bayt (as), na katika historia yote umeendelea kupitia wanazuoni wakubwa, Mara'ji' wa kidini na watu mashuhuri wenye ushawishi katika ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwao ni Imam Khomeini (ra), Imam Shahidi, Sayyid Hassan Nasrullah na Shahidi Sadr, ambao kila mmoja katika kipindi chake ameleta athari muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu.
Hiyo ndiyo maana halisi ya ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume Wake (saww), alipomwambia kwamba atakuwa na Kawthar, huku adui yake akiwa hana mwendelezo.
Kutokana na maelezo haya, inabainika kwamba mojawapo ya mifano iliyo wazi na kamilifu zaidi ya Kawthar ni Bibi Zahra al-Mardhiyyah, Fa'tima Zahra (sa), ni kana kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anamtolea Mtume Wake bishara akimwambia: Usihuzunike wala kuwa na wasiwasi; tutakujalia Bibi Fa'tima Zahra (sa), mwanamke ambaye kupitia kizazi chake watatokea Imam Hassan (as), Imam Hussein (as), watoto wake wengine na hatimaye Mtukufu Hujjat (ajf).
Aidha, wanazuoni na watu wengi mashuhuri kutoka katika kizazi cha Mtume (saww) watajitokeza katika vipindi mbalimbali vya historia. Hawa ni watu watakaoujaza ulimwengu mambo ya kiroho na maarifa ya Mtume mwenye utukufu mkubwa pamoja na Ahlul-Bayt wa Mtume Watoharifu (as).
Suratul-Kawthar ni sura fupi, lakini yenye utukufu mkubwa sana. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
«إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ * فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ»
Hakika Sisi tumekujalia Kawthar. Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje mnyama wa kuchinja.
Maana yake ni kwamba, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amemjaalia Mtume Wake Kawthar, basi anapaswa kuswali kwa ajili ya Mola wake na kutoa dhabihu.
Kwa kuwa neema hii ni kheri nyingi, na mojawapo ya mifano yake mikuu ni Bibi Fa'tima Zahra (sa), inapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa neema kubwa kama hii. Hivyo, mtu anatakiwa kuswali, kutoa dhabihu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kuu ya Kiungu.
Pamoja na bishara hii, Suratul-Kawthar pia ina ahadi nyingine, nayo ni kwamba maadui wa Mtume (saww) watakuwa abtar, yaani, watakosa mwendelezo na urithi wenye kudumu.
Leo hii, tunashuhudia jinsi watoto na kizazi cha Mtume mwenye utukufu mkubwa wanavyoendelea kuangaza nuru katika ulimwengu ambao giza na dhuluma vimetanda katika sehemu kubwa za maeneo yake.
Imam Khomeini (ra) alianzisha Mhimili wa Muqawama, ambao unasimama dhidi ya madola dhalimu na wenye kiburi wanaotawala zama hizi. Hawa ni watu ambao, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mazungumzo haya, hawana chembe ya ubinadamu, na katika matukio yanayohusishwa na Kisiwa cha Epstein wameonesha sura ya ukatili na kukiuka heshima na utu wa mwanadamu.
Miongoni mwa watu waliosimama dhidi ya mikondo hii na kupinga nguvu zao alikuwa mmoja wa kizazi cha Mtume (saww) na uzao wa Bibi Fatwima Zahra al-Mardhiyyah (sa).
Hii ni mojawapo ya dhihirisho la ukweli wa Kawthar; neema ambayo mwendelezo wake utaendelea kuwepo. Katika kila zama, watoto na kizazi cha Bibi Fa'tima Zahra (sa) watasimama dhidi ya dhuluma na ukandamizaji, watavunja giza na kuandaa mazingira ya kudhihiri kwa mtoto wa Bibi huyo, Mtukufu Hujjat (ajf).
Kwa sababu hiyo, watu wote wapendwa wanapaswa kuitafakari kwa kina sura hii fupi, lakini iliyojaa maarifa, ili waendelee kuhifadhi matumaini yao kuhusu mustakabali, ushindi wa haki na kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa ujumbe wa sura hii ni kwamba maadui wa Mtume (saww) na wapinzani wa njia ya Bibi Fatwima Zahra (sa) wamehukumiwa kutoweka katika kila kipindi cha historia. Hakutakuwa na jina wala alama itakayobaki ya dhuluma zao, na hatimaye watatupwa katika jalala la historia. Hii pia ni mojawapo ya ahadi ambazo tunaweza kuzipata kutokana na Suratul-Kawthar.
Maoni yako