Jumapili 25 Oktoba 2026 - 14:25
Ujerumani Yakaribia Kukumbwa na Wimbi Jipya la Maandamano ya Wanafunzi/ Wito Watolewa wa Maandamano ya Kitaifa Oktoba 31

Hawza/ Vyama vya wanafunzi na Chama cha Mrengo wa Kushoto nchini Ujerumani vimeunga mkono maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 31 Oktoba. Maandamano hayo yanalenga kudai ongezeko la bajeti ya elimu, uboreshaji wa miundombinu ya shule na kuboreshwa mazingira ya kujifunzia. Wakati huohuo, hali hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa majimbo kuhusu uwezekano wa kuenea maandamano ya wananchi yanayofanana na yale ya Ufaransa.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Ujerumani inakaribia kuingia katika kipindi cha maandamano ya wanafunzi yaliyopangwa kufanyika tarehe 31 Oktoba. Maandamano hayo, yanayoungwa mkono na vyama vya wanafunzi pamoja na Chama cha Mrengo wa Kushoto, yanalenga kudai maboresho katika elimu, ulinzi wa mazingira na hali ya maisha. Wakati huohuo, viongozi wa majimbo wanaonya kuhusu uwezekano wa kuenea kwa maandamano ya wananchi.

Shirika moja la wanafunzi nchini Ujerumani pamoja na chama cha upinzani cha Die Linke vilitangaza siku ya Alhamisi kuunga mkono maandamano yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba. Maandamano hayo yanalenga kudai kutengwa fedha zaidi, kuongezwa uwekezaji katika sekta ya elimu na kuboreshwa hali ya shule, vyombo vya habari ndivyo vilivyoripoti taarifa hiyo.

Baraza la Shirikisho la Wanafunzi wa Ujerumani limeunga mkono maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 31 Oktoba katika miji kadhaa ya nchi hiyo. Isabel Seltenreich, msemaji wa baraza hilo, alitangaza jambo hilo katika mahojiano na gazeti la Rheinische Post.

Aliongeza kuwa wanafunzi wana haki ya kushiriki maandamano hayo na wana sababu za kutosha za kujitokeza mitaani ili kudai kuboreshwa kwa mfumo wa elimu.

Harakati za vijana na wanafunzi zinazojulikana kwa majina ya “GenZ regelt’”, linalomaanisha “Kizazi cha Z kinachukua mambo mikononi mwake,” na “GenZ steht auf”, linalomaanisha “Kizazi Z kinaamka na kusimama kidete,” zimeanzisha kampeni kupitia mtandao ili kuwahamasisha wafuasi kuunga mkono maandamano hayo.

Harakati hizo pia zinataka kuimarishwa ulinzi wa tabianchi, kuchukuliwa hatua za kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha, pamoja na kupinga huduma ya kijeshi ya lazima. Mpango huu umekataa waziwazi matumizi ya vurugu.

Isabel Seltenreich alisema kuwa Baraza la Shirikisho la Wanafunzi wa Ujerumani linaunga mkono madai mengi yanayotolewa pia katika maandamano yanayofanyika nchini Ufaransa na Italia.

Alisema: “Miongoni mwa madai hayo ni kuboreshwa vifaa na miundombinu ya shule, kuhakikisha kunakuwa na idadi ya kutosha ya walimu, kupunguza idadi ya wanafunzi katika madarasa, kuboresha mazingira ya kujifunzia, na kuunda mfumo wa elimu unaotoa fursa sawa kwa vijana wote, bila kujali mazingira yao ya kijamii.”

Hata hivyo, akirejelea hali ilivyo nchini Ufaransa na Italia, alionya kuhusu hatari ya harakati hizi kutekwa na kutumiwa na makundi mbalimbali ya kisiasa kwa ajili ya malengo yao.

Msimamo wa Isabel Seltenreich wa kuunga mkono harakati za maandamano uliungwa mkono pia, kwa kiasi fulani, na Ines Schwerdtner, mwenyekiti mwenza wa chama cha upinzani cha Die Linke.

Katika ujumbe wa video aliouelekeza kwa Chama cha Kidemokrasia cha Kisoshalisti cha Wanafunzi (SDS), Schwerdtner alisema kuwa; Ujerumani inapaswa kuwa na uwezo wa kuiga mambo yanayokwenda vizuri nchini Ufaransa, yaani, harakati mbalimbali za kijamii kukaribiana na kushirikiana.

Schwerdtner alitangaza kuunga mkono wanaharakati wa SDS. Kwa sasa, shirika hilo linafuatiliwa na vyombo vya ujasusi wa ndani katika majimbo ya Bavaria na Baden-Württemberg. Alisema: “Nitawatetea, bila kujali ni nani atakayewashambulia; iwe ni polisi au vyombo vya habari.”

Nchini Ufaransa, wanafunzi wamekuwa wakiandamana tangu mwishoni mwa mwezi Septemba wakitaka kuboreshwa miundombinu ya elimu, kuongezwa idadi ya walimu na kuboreshwa mazingira ya kujifunzia. Baadaye, maandamano yanayofanana na hayo yalienea pia nchini Italia. Katika nchi zote mbili, maandamano hayo yameambatana pia na vitendo vya vurugu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha