Alhamisi 15 Oktoba 2026 - 14:00
Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC) Lawakabidhi Viongozi wa Kiislamu Tablet ili Kuimarisha Mawasiliano

Hawza/ Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC) limewagawia viongozi wa Kiislamu katika Mikoa ya Kiislamu ya Kampala, Buganda Mashariki na Buganda Magharibi vifaa vya kielektroniki aina ya Android tablets, kwa lengo la kuimarisha mawasiliano, utafiti na usimamizi wa taarifa. Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Baraza hilo wa Miaka Kumi nchini humo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Mufti wa Uganda, Mheshimiwa Dkt. Sheikh Shaban Ramadhan Mubaje, aliongoza hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika Jumanne, tarehe 13 Oktoba 2026, katika ukumbi wa mikutano wa bodi ya Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda.

Miongoni mwa waliopewa vifaa hivyo ni wasaidizi wa Mufti katika Mikoa ya Kampala, Buganda Mashariki na Buganda Magharibi, makatibu wa mikoa hiyo, wajumbe wa Baraza la Ulama, wawakilishi wa Baraza la Shura na Baraza la Ushauri, pamoja na makadhi wa wilaya kutoka katika mikoa hiyo mitatu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mufti alisema kuwa lengo la kuwapatia viongozi hao vifaa hivyo ni kuwawezesha kupata ujuzi na nyenzo zinazohitajika katika kutafuta, kupata na kusimamia maarifa katika ulimwengu wa sasa unaozidi kutegemea teknolojia za kidijitali.

Aliwataka viongozi waliopokea vifaa hivyo kuvitumia kwa uwajibikaji ili kuboresha mawasiliano, kufanya tafiti na kuhifadhi kumbukumbu muhimu pamoja na taarifa nyingine zenye manufaa.

“Tunawasihi kuvitumia ipasavyo ili kuimarisha mawasiliano, kufanya tafiti zaidi na kuhifadhi aina mbalimbali za data pamoja na taarifa nyingine muhimu,” alisema Sheikh Mubaje alipokuwa akimkabidhi kila kiongozi kifaa chake pamoja na vifaa vyake vya ziada.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Mufti, Mheshimiwa Sheikh Muhammad Ali Waiswa; Naibu Mufti wa Pili, Dkt. Sheikh Hafiz Muhammad Harunah Bukenya; Katibu Mkuu wa UMSC, Hadji Abbas Muluubya Ssekyanzi; Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Fedha na Utawala, Wakili Haj Muhammad Ali Aluma; pamoja na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo na Mipango, Abdul-Razaq Arinda, na viongozi wengine wa Baraza hilo.

Awali, Muluubya alielezea mabadiliko yanayoendelea kufanyika ndani ya Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda, kuwa hayajawahi kushuhudiwa kwa kiwango hicho hapo awali. Aidha, aliwataka viongozi wa Kiislamu kukumbatia utamaduni wa kufanya kazi kwa ushirikiano na kutekeleza majukumu yao kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Alisisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja katika kuendeleza ajenda ya maendeleo ya taasisi hiyo na kuboresha utoaji wa huduma kwa Waislamu.

Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC) Lawakabidhi Viongozi wa Kiislamu Tablet ili Kuimarisha Mawasiliano

Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC) Lawakabidhi Viongozi wa Kiislamu Tablet ili Kuimarisha Mawasiliano

Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC) Lawakabidhi Viongozi wa Kiislamu Tablet ili Kuimarisha Mawasiliano

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha