Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Muhammad Mahdi Shabzendehdar, ambaye ni Katibu wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu na mwanachama wa Baraza la Walinzi wa Katiba la Iran, aliyasema hayo Jumanne usiku, tarehe 21 Mehr 1405 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 13 Oktoba 2026, katika darsa ya maadili iliyofanyika katika Shule ya Faydhiyya mjini Qum.
Katika hotuba yake, alijikita katika mihimili mitatu: “Kujitakasa nafsi na mwenendo wa kiroho,” “Mambo muhimu katika masomo na maisha ya mwanafunzi wa Hawza,” na “Wajibu wa wanazuoni wa dini katika mazingira nyeti ya nchi.”
Akifafanua wasia wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kwa Amirul-Muuminina Ali (a.s.), alisema kuwa; kutekeleza mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.) ndio njia ya kuaminika ya kufikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho. Alisisitiza umuhimu wa kuzitunza ndimi zetu, kuzingatia uchamungu, kuimarisha maarifa kuhusu Mwenyezi Mungu na kujipamba na tabia njema.
Mwanazuoni huyo wa Hawza ya Qum pia alifafanua nafasi ya mila za kielimu za Hawza, huku akisisitiza umuhimu wa wanafunzi kufanya maandalizi ya masomo kabla ya vipindi, kujadiliana masomo na wenzao, kuandika maelezo ya darsa za walimu, kupitia upya masomo na kuhifadhi matini za kielimu. Aidha, alitaka matumizi ya mbinu mpya za ufundishaji yaendane sambamba na kuhifadhi mila bora za kielimu zilizothibitika kuwa na manufaa katika Hawza.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alitaja utayari wa kutoa uhai, mali na heshima kwa ajili ya dini, kusimama imara mbele ya maadui na kutekeleza majukumu ya kijamii ya wanazuoni wa dini kuwa miongoni mwa wajibu wa watu wa Hawza.
Maelekezo ya uhakika ya mwenendo wa kiroho yanapaswa kupatikana kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) na Maimamu (a.s.)
Ayatullah Shabzendehdar, akieleza kuwa kujiunga na Hawza ni neema kubwa, alisema: “Wanadamu wote, hasa ndugu zetu wapendwa wanaojiunga na Hawza na kupata neema hii ya kuingia katika kambi za wanaoiunga mkono dini ya Mwenyezi Mungu na kuwa miongoni mwa askari wa Hadhrat Baqiyyatullah (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), kwa kawaida hufuata wito wa maumbile yao ya asili na roho zao safi kwa kutafuta kuinuka kiroho. Wanataka kutoka katika hali ya chini ya ulimwengu wa kimaada na kupaa hadi kufikia daraja ambayo:
حَتَّى تَخْرِقَ أَبْصَارُ الْقُلُوبِ حُجُبَ النُّورِ فَتَصِلَ إِلَى مَعْدِنِ الْعَظَمَةِ
Hadi macho ya nyoyo yatakapopenya pazia za nuru na kufika kwenye chanzo cha utukufu.”
Aliongeza kwa kuuliza: “Ni ipi njia ya kufikia vilele hivyo vya juu? Wanafunzi wa Hawza wanaoheshimika huja kwetu wakitafuta maelekezo ya kufuata katika safari yao ya kiroho. Wakati mwingine huenda kwa wanazuoni wakubwa na kuwaomba maelekezo hayo. Hata hivyo, maelekezo ya uhakika, yenye kuaminika na yasiyo na upotovu wala mikengeuko, ni yale yaliyotolewa na Mtume wetu mkuu (s.a.w.w.) na Maimamu waongofu (a.s.).”
Kusema kweli: Ushauri wa kwanza wa Mtume (s.a.w.w.) kwa Amirul-Muuminina Ali (a.s.)
Ayatullah Shabzendehdar, akieleza kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alitoa maelekezo sita katika riwaya hiyo, alisema kuwa agizo la kwanza ni:
أَمَّا الْأُولَى فَالصِّدْقُ، وَلَا تُخْرِجَنَّ مِنْ فِيكَ كَذِبَةً أَبَدًا
Au:
وَلَا تَخْرُجَنَّ مِنْ فِيكَ كَذِبَةٌ أَبَدًا
Alifafanua kuwa matamshi hayo yote mawili ni sahihi.
Alisema kwamba jambo la kwanza ni kuzitunza ndimi zetu ili kamwe, kama Mtume (s.a.w.w.) alivyosisitiza, tusiseme uongo au kauli isiyolingana na ukweli kupitia midomo na ndimi zetu.
Aliongeza kuwa katika mazingira mbalimbali, hasa ya kisiasa, wapo watu ambao hawana kizuizi chochote katika ndimi zao. Kauli moja tu wanayotoa inaweza kuwashusha katika daraja ya chini kabisa na kuharibu hadhi yao.
Uchamungu wa kujizuia na mambo yenye shaka ni sharti la kufikia daraja za juu za kiroho
Ayatullah Shabzendehdar alisoma agizo la pili katika riwaya hiyo kama ifuatavyo:
وَالثَّانِيَةُ الْوَرَعُ، وَلَا تَجْتَرِئْ عَلَى خِيَانَةٍ أَبَدًا
Agizo la pili ni kujichunga, na usithubutu kamwe kufanya khiyana.
Alieleza kuwa jambo la pili ni wara‘, yaani kiwango cha juu cha kujilinda na mambo yanayoweza kumwingiza mtu katika maasi au kumweka mbali na radhi za Mwenyezi Mungu.
Alifafanua kwamba wara‘ ni daraja lililo juu zaidi ya uadilifu. Mtu mwadilifu ni yule anayetekeleza wajibu wake na kujiepusha na mambo yaliyoharamishwa, lakini mtu mwenye wara‘ huchukua tahadhari hata dhidi ya mambo yanayoizunguka mipaka hiyo, ili asije akaangukia katika makosa.
Kumwogopa Mwenyezi Mungu na kumcha kutokana na kutambua utukufu Wake
Ayatullah Shabzendehdar alilitaja agizo la tatu la Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kama ifuatavyo:
وَالثَّالِثَةُ الْخَوْفُ مِنَ اللَّهِ عَزَّ ذِكْرُهُ كَأَنَّكَ تَرَاهُ
Agizo la tatu ni kumwogopa Mwenyezi Mungu, ambaye jina Lake ni tukufu, kana kwamba unamuona.
Akifafanua sehemu hiyo ya riwaya, alisema kwamba mtu anapokaribia kufanya kosa au dhambi, anapaswa kumwogopa Mwenyezi Mungu kwa kiwango ambacho ni kana kwamba anamuona.
Alifafanua kuwa; Mwenyezi Mungu mwenyewe si wa kuogopwa kwa maana ya kuwa na hofu ya udhaifu, kwani Yeye ni Mwingi wa huruma. Badala yake, hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba Mwenyezi Mungu ni:
أَشَدُّ الْمُعَاقِبِينَ فِي مَوْضِعِ النَّكَالِ وَالنَّقِمَةِ
Mkali zaidi katika kuadhibu panapostahili adhabu na kulipiza kisasi.
Kwa hiyo, kumcha Mwenyezi Mungu kunapaswa kutokana na kutambua utukufu Wake, mamlaka Yake na uzito wa matokeo ya kumuasi.
Kuwa tayari kutoa uhai, mali na heshima kwa ajili ya dini
Ayatullah Shabzendehdar, alipokuwa akisoma agizo la tano la Mtume (s.a.w.w.), alisema:
وَالْخَامِسَةُ بَذْلُكَ مَالَكَ وَدَمَكَ دُونَ دِينِكَ
Agizo la tano ni kutoa mali yako na damu yako kwa ajili ya kuitetea dini yako.
Alisema: “Leo ndiyo wakati wa kutekeleza agizo hili; ni wakati wa kutoa mali yako kwa ajili ya dini yako, kuwa tayari kutoa damu yako na kujitolea kwa uhai na mali yako katika njia ya dini.”
Aliongeza kuwa ikiwa neno «مالَک» litasomwa kwa maana ya mali yako, basi neno maal limeunganishwa na kiwakilishi cha umiliki kinachomaanisha “yako.”
Hata hivyo, alieleza kuwa kuna uwezekano mwingine katika hadithi hiyo tukufu, yaani herufi «ما» ikawa ni mawsulah, inayomaanisha “kile ambacho” au “kila kitu ambacho.”
Kwa mtazamo huo, kauli «ما لَکَ» ingemaanisha “kila kitu ulicho nacho.” Hivyo, agizo hilo halihusu uhai na mali pekee, bali linahimiza mtu kuwa tayari kutoa uhai wake na kila kitu alicho nacho kwa ajili ya dini yake.
Kuzingatia Sunna ya Mtume (s.a.w.w.) katika swala, saumu na sadaka
Ayatullah Shabzendehdar alisoma agizo la sita kama ifuatavyo:
وَالسَّادِسَةُ الْأَخْذُ بِسُنَّتِي فِي صَلَاتِي وَصَوْمِي وَصَدَقَتِي
Agizo la sita ni kufuata Sunna yangu katika swala yangu, saumu yangu na sadaka yangu.
Alifafanua kuwa maana yake ni mtu kuifanya njia ya Mtume (s.a.w.w.) kuwa mwongozo wake katika kuswali, kufunga saumu, kutoa sadaka na kuwasaidia watu wenye mahitaji.
Kisha Mtume (s.a.w.w.) alifafanua zaidi kwa kusema:
أَمَّا الصَّلَاةُ فَالْخَمْسُونَ رَكْعَةً
Ama kuhusu swala, ni rakaa hamsini.
Ayatullah Shabzendehdar alieleza kwamba rakaa hizo hamsini zinajumuisha rakaa za swala za wajibu za kila siku pamoja na rakaa za swala za sunna zinazoswaliwa kila siku.
Mwisho wa darsa hiyo, mwanazuoni huyo anayefundisha masomo ya juu ya Hawza ya Qum alisoma dua akisema: “Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie sote tawfiki ya kuitumikia kwa ikhlasi dini yetu tukufu ya Uislamu, na Inshaallah, awajaalie wanafunzi wote wa Hawza, wanazuoni na watu wote wa Hawza kupata radhi za Mtukufu Baqiyyatullah (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).”
Maoni yako