Alhamisi 15 Oktoba 2026 - 15:00
Masomo ya kielimu ya Shahidi Hassan Nasrullah hayakuwahi kusimama/ Waandishi na watu wa fikra waitambulishe dunia huduma za Sayyid wa Muqawama.

Hawza/ Ayatullah Najmuddin Murawwij Tabasi amesema kwamba; miongoni mwa vipengele muhimu vya shakhsia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah ni namna alivyoipa umuhimu mkubwa Hawza na juhudi zake za kuvutia na kulea kizazi kipya katika njia ya kujifunza elimu za kidini.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Najmuddin Murawwij Tabasi aliyasema hayo katika mkutano wa kitaaluma wa maandalizi ya kongamano kuhusu mfumo wa fikra na harakati za jihadi za Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, lililokuwa na kaulimbiu isemayo "Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah: Kielelezo cha Muqawama na Mapambano dhidi ya Dhuluma". Mkutano huo ulifanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la Elimu la Imam Khomeini (r.a.) mjini Qum.

Akizungumzia wajibu wa waandishi na watu wenye fikra katika kuitambulisha shakhsia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, Ayatullah Tabasi alisema: “Ndugu zangu wapendwa, ninapendekeza kwamba kila mmoja wenu ambaye ni mwandishi, mzungumzaji au mtu mwenye fikra, atumie uwezo na vipaji vyake kuitambulisha shakhsia hii na kufafanua huduma zake. Ninafahamu kwamba wengi wenu mna uwezo wa kufanya hivyo, na mnaweza kuwaelezea wananchi vipengele mbalimbali vya shakhsia yake na utendaji wake.”

Akizungumzia juhudi za baadhi ya makundi za kuzuia ujumbe na sauti ya Kambi ya Muqawama isiwafikie watu, aliongeza kwamba; tunaishi katika kipindi ambacho kuna juhudi za kuzuia sauti ya kudai haki na ujumbe wa harakati hii usiwafikie watu duniani.

Alieleza kuwa; tunapozungumzia udhibiti wa habari katika vyombo vya habari, mojawapo ya maeneo ambayo nafasi ya waandishi na wanahabari inajitokeza wazi zaidi kuliko hapo awali ni uwanja huo wa kuufikisha ujumbe kwa watu.

Nafasi ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah katika mabadiliko ya Lebanon na dunia

Mwalimu huyo wa Hawza ya kielimu ya Qum, huku akisisitiza umuhimu wa kujifunza kwa kina historia ya Lebanon na matukio yanayohusiana na Hizbullah, alisema kwamba; mtu atakayechunguza kwa usahihi historia ya Lebanon na kipindi cha shughuli za Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, atatambua athari kubwa ambayo mtu huyo alikuwa nayo katika mabadiliko ya Lebanon na hata katika mizani ya kisiasa na kimkakati ya kikanda na kimataifa.

Akizungumzia nafasi ya Muqawama katika kubadilisha mizani ya nguvu katika eneo hilo, aliongeza kwamba; Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah aliweza kusimama imara na kwa nguvu mbele ya utawala wa Kizayuni, na kuonesha taswira tofauti kuhusu udhaifu na uwezekano wa utawala huo kushindwa. Alifafanua kwamba; athari za msimamo huo havikuishia kwa Israel pekee, bali pia viliathiri mataifa yenye nguvu yaliyokuwa yakiuunga mkono utawala huo.

Ayatullah Tabasi, huku akigusia historia ya uvamizi na mauaji yaliyofanyika nchini Lebanon, alisema kwamba; katika vipindi mbalimbali, vikosi vya Israel viliingia katika maeneo tofauti ya Lebanon na kuwaua kishahidi wananchi wengi. Hata hivyo, Muqawama wa Lebanon uliweza kubadilisha mizani ya nguvu kupitia msimamo wake thabiti na kusimama kidete dhidi ya uvamizi huo.

Waandishi na wanaharakati wa mitandao ya kijamii waitambulishe dunia huduma za Shahidi Nasrallah

Ayatullah Tabasi, huku akisisitiza wajibu wa kiutamaduni na kihabari wa wasomi na watu wenye uwezo katika jamii, alisema kwamba; leo hii, watu ambao ni waandishi, wanaohusiana na vyombo vya habari au wanaofanya shughuli katika mitandao ya kijamii, wana wajibu wa kutumia uwezo huo kuitambulisha shakhsia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah.

Aliendelea kusema kwamba kila mmoja anaweza kulichunguza suala hilo kwa mtazamo wake maalumu. Mtu mmoja anaweza kuchunguza huduma zake kwa Uislamu, mwingine akaeleza nafasi yake katika kuimarisha nafasi ya Ushia, huku mwingine akichunguza vipengele vya kielimu, kiroho, kimaadili na kimapambano vya shakhsia yake. Alisisitiza kwamba juhudi zote hizo zikikusanywa pamoja, zinaweza kuwapa wananchi taswira pana na yenye ukamilifu zaidi kuhusu shakhsia hiyo.

Shahidi Nasrullah aliipa umuhimu wa pekee elimu ya Mahdawiyya

Ayatullah Tabasi, huku akizungumzia masomo na tafiti nyingi za Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah kuhusu Mahdawiyya, alisema kwamba; mojawapo ya mada alizokuwa akizifuatilia kwa umakini mkubwa ni masuala yanayohusiana na Imam Mahdi (a.j.).

Alieleza kwamba wakati mwingine mtu hushangazwa na wingi wa masomo na kiwango cha ufuatiliaji wa shakhsia fulani katika uwanja huo, hasa anapozingatia kwamba Shahidi Nasrallah alikuwa mstari wa mbele katika Kambi ya Muqawama, huku taarifa za matukio na masuala muhimu zikiendelea kumfikia mara kwa mara.

Mjumbe wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Kielimu ya Qum aliongeza kwamba; licha ya majukumu mazito aliyokuwa nayo na umuhimu wa kufuatilia masuala ya kisiasa, kijamii na kijeshi, masomo yake ya kielimu na kiroho hayakuwahi kusimama.

Alifafanua kwamba; Shahidi Nasrullah alikuwa akitenga muda kwa ajili ya masuala ya Mahdawiyya na kuzifuatilia kwa umakini mkubwa mada zinazohusiana na sekta hiyo.

Shahidi Nasrullah alikuwa na mapenzi ya pekee kwa Ahlul-Bayt (a.s.) na Imam Hussein (a.s.)

Ayatullah Tabasi aligusia mapenzi makubwa aliyokuwa nayo Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah kwa Ahlul-Bayt wa Mtume (amani iwe juu yao), hasa Mtukufu Sayyid al-Shuhada Imam Hussein (amani iwe juu yake).

Alisema kwamba; Shahidi Nasrallah alikuwa na mapenzi ya pekee kwa Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao) na Imam Hussein (amani iwe juu yake). Kila kiliposomwa kilio cha maombolezo kuhusu masaibu ya Aba Abdillah al-Hussein (amani iwe juu yake), alikuwa akiguswa sana na kutokwa na machozi.

Akizungumzia hali ya mikusanyiko ya maombolezo nchini Lebanon katika miaka iliyopita, alisema kwamba; hapo zamani, kuandaliwa mikusanyiko ya maombolezo ya Imam Hussein (amani iwe juu yake) katika baadhi ya maeneo ya Lebanon, hasa Beirut, kulikabiliwa na vikwazo. Alifafanua kwamba wakati huo, mikusanyiko mikubwa ya wazi ya maombolezo kama ile inayoshuhudiwa leo haikuwepo.

Shahidi Nasrullah aliipa umuhimu Hawza za kielimu na malezi ya kizazi kipya

Ayatullah Tabasi, huku akizungumzia namna Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah alivyoipa umuhimu Hawza alisema; kwamba miongoni mwa vipengele muhimu vya shakhsia yake ni namna alivyovipa kipaumbele vituo hivyo vya elimu na juhudi zake za kuvutia na kulea kizazi kipya katika njia ya kujifunza elimu za kidini.

Alieleza kwamba; ingawa hata kabla yake kulikuwa na wanazuoni na shakhsia za kidini zilizokuwa zikifanya kazi katika uwanja huo, juhudi za Shahidi Nasrallah za kukiunganisha kizazi kipya na Hawza za kielimu, pamoja na kuweka mazingira ya kuwalea na kuwaandaa vijana, zilikuwa miongoni mwa sifa mashuhuri za shughuli zake.

Shahidi Nasrullah alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Ayatullah Tabasi, akizungumzia mikutano ya faragha aliyowahi kufanya na Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, alisema kwamba alipata fursa ya kuzungumza naye katika vikao kadhaa vya faragha, ambapo baadhi ya vikao hivyo vilidumu kwa takribani saa nne na nusu.

Alifafanua kwamba mikutano hiyo, pamoja na vikao vya wazi, ilitoa fursa nzuri ya kufanya mazungumzo ya kielimu na kuchunguza masuala mbalimbali.

Aliongeza kwamba katika vikao hivyo, ilikuwa rahisi kutambua namna Shahidi Nasrallah alivyokuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nafasi yake katika eneo hili. Alikuwa akifuatilia kwa makini hali hiyo na kuhakikisha kwamba hakuna madhara yanayoweza kuikumba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Tabasi alihitimisha kwa kusisitiza kwamba; ili kuielewa shakhsia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, ni lazima kuchunguza kwa pamoja vipengele mbalimbali vya maisha yake, vikiwemo vya kielimu, kiitikadi, kiutamaduni, kijamii na kisiasa.

Alibainisha kwamba alikuwa mtu ambaye, pamoja na majukumu yake katika Kambi ya Muqawama, aliipa pia umuhimu wa pekee elimu ya Mahdawiyya, mikusanyiko ya maombolezo ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), malezi ya kizazi kipya, Hawza na uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha