Alhamisi 15 Oktoba 2026 - 13:00
Ukweli wa utu wa mwanadamu unavuka mipaka ya kuwa mwanamume au mwanamke/ 
Msijiuze kwa thamani iliyo chini ya Pepo.

Hawza/ Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli amesisitiza kwamba Banu Umaiyya, na baada yao Banu Abbas pamoja na watawala wengine, walikuwa wakiyahusisha matukio na qadhaa na qadar ya Mwenyezi Mungu ili kuhalalisha dhuluma zao na kulinda mamlaka yao, kwa lengo la kujionesha kuwa hawawajibiki kwa matendo yao. Hata hivyo, Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao) walikuwa wakifafanua kwamba mwanadamu anawajibika kwa matendo na mienendo yake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kikao cha kila wiki cha darsa ya maadili cha Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli kilifanyika asubuhi ya jana, Jumatano, tarehe 22 Mehr 1405 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 14 Oktoba 2026, katika Msikiti Mkuu wa Qum. Kikao hicho kilihudhuriwa na watu wa makundi mbalimbali ya jamii.

Katika kikao hicho, Ayatullah Jawadi Amuli aligusia maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa furaha Hadhrat Zainab al-Kubra (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake). Pia alifafanua nafasi ya kielimu na kiutambuzi ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), huku akichambua maneno ya Hadhrat Zainab mbele ya Ubaidullah bin Ziyad na kuelezea nafasi ya Bibi huyo katika kupambana na fikra za kuamini kwamba mwanadamu hana hiari katika matendo yake, pamoja na kufafanua wajibu wa mwanadamu kwa matendo yake.

Maneno ya Bibi Zainab (a.s.): Ufafanuzi wa kielimu dhidi ya fikra za kulazimishwa kimatendo za Banu Umayya

Ayatullah Jawadi Amuli, akizungumzia nafasi ya kielimu na kiutambuzi ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), alisema kwamba; maneno ya Bibi Zainab al-Kubra (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) aliyoyatoa mjini Kufa hayakuwa maneno ya kulia na kueleza masaibu tu, bali yalikuwa na maana ya kina na yalihusu suala nyeti la kiitikadi na kielimu linalohusiana na itikadi.

Akizungumzia historia ya kuenezwa fikra za Jabariyya, yaani imani kwamba mwanadamu analazimishwa katika matendo yake na hana hiari, wakati wa utawala wa Banu Umayya, alisema kwamba; Muawiya alitumia miaka mingi ya utawala wake akijitahidi kuimarisha mamlaka yake na kuhakikisha utawala wake unaendelea. Kwa lengo la kuhakikisha kwamba mambo mema na baraka zinahusishwa na utawala wake, huku mambo mabaya na matatizo yakihusishwa na Mwenyezi Mungu, Muawiya alieneza fikra za Jabariyya.

Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli alisisitiza kwamba Banu Umayya, na baada yao Banu Abbas pamoja na watawala wengine, walikuwa wakiyahusisha matukio na qadhaa na qadar ya Mwenyezi Mungu ili kuhalalisha dhuluma zao na kulinda mamlaka yao, huku wakitaka kujionyesha kuwa hawawajibiki kwa matendo yao. Hali hiyo ilikuwa tofauti na mafundisho ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), ambao walikuwa wakifafanua ukweli wa kauli isemayo:

لَا جَبْرَ وَلَا تَفْوِيضَ وَلَكِنْ أَمْرٌ بَيْنَ أَمْرَيْنِ

Hakuna kulazimishwa kabisa, wala hakuna kukabidhiwa mambo kikamilifu kwa mwanadamu bila ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu, bali kuna hali iliyo kati ya mambo hayo mawili.

Alifafanua kwamba kupitia kanuni hiyo, Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao) walimchukulia mwanadamu kuwa anawajibika kwa matendo na mienendo yake. Alibainisha kwamba Maimamu (amani iwe juu yao), licha ya kuwa katika kilele cha utambuzi, walikuwa wakifafanua masuala ya kina ya kielimu na kiakili, huku wakisimama imara kupinga upotovu wa fikra na itikadi.

Katika kufafanua suala hilo, Ayatullah Jawadi Amuli aligusia mazungumzo yaliyofanyika kati ya Bibi Zainab al-Kubra (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) na Ubaidullah bin Ziyad, alieleza kwamba maneno ya Bibi Zainab mjini Kufa yalikuwa na maana ya kina na lilikuwa jibu la kielimu dhidi ya fikra potovu za Jabariyya.

Alisema kwamba Ubaidullah bin Ziyad alipomuuliza Bibi Zainab: “Je, umeona jinsi Mwenyezi Mungu alivyomtendea ndugu yako?” Au aliposema: “Mwenyezi Mungu ndiye aliyemuua Ali ibn al-Hussein huko Karbala!”, hakuwa akizungumzia yeye mwenyewe, wao au Banu Umayya, bali alikuwa akilihusisha jambo hilo na Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika, alikuwa akizungumza kwa mtazamo wa Jabariyya, yaani fikra inayohusisha matendo ya mwanadamu na matakwa ya Mwenyezi Mungu kwa namna inayomwondolea mwanadamu wajibu wa matendo yake.

Bibi Zainab (amani iwe juu yake) alimjibu kwa kusema:

مَا رَأَيْتُ إِلَّا جَمِيلًا

Sikuona chochote isipokuwa uzuri.

Ayatullah Jawadi Amuli alifafanua kwamba maana ya jibu hilo ni kuwa matendo ya Mwenyezi Mungu ni mazuri, lakini nyinyi ndio wauaji, ni nyinyi mliomsababishia Ali bin al-Hussein kuuawa shahidi.

Kwa hiyo, Hadhrat Zainab (amani iwe juu yake) alivunja fikra za Jabariyya zilizokuwa zikienezwa na Banu Umayya na kufafanua ukweli wa hiari ya mwanadamu pamoja na kuwajibika kwake katiks matendo yake.

Mwanadamu asijiuze kwa thamani iliyo chini ya Pepo

Katika kuendelea na darsa yake, Ayatullah Jawadi Amuli alifafanua hekima mbalimbali kutoka katika Nahjul-Balagha, akieleza ukweli wa uhuru wa mwanadamu, thamani yake na nafasi ya moyo katika safari ya kiroho.

Akifafanua maneno ya Amirul-Muuminina Ali (amani iwe juu yake) yaliyomo katika kitabu cha Nahjul-Balagha, alieleza ukweli wa kuwa huru na thamani ya uwepo wa mwanadamu. Alinukuu maneno yafuatayo:

أَلَا حُرٌّ يَدَعُ هَذِهِ اللُّمَاظَةَ لِأَهْلِهَا، إِنَّهُ لَيْسَ لِأَنْفُسِكُمْ ثَمَنٌ إِلَّا الْجَنَّةَ، فَلَا تَبِيعُوهَا إِلَّا بِهَا

Je, hakuna mtu huru atakayeyaacha mabaki haya kwa watu wake? Fahamuni kwamba thamani ya nafsi zenu si nyingine isipokuwa Pepo; kwa hiyo, msiziuze kwa kitu kingine chochote isipokuwa Pepo.

Ayatullah Jawadi Amuli, huku akifafanua maana ya neno «لماظة» (Lumadhah), alisema kwamba neno hilo linamaanisha mabaki ya chakula yanayobaki katikati ya meno.

Alieleza kwamba nyadhifa nyingi, vyeo na nafasi mbalimbali, iwe ni katika Hawza, vyuo vikuu, siasa au jamii, ni kama mabaki hayo ya chakula. Watu wengine walifika katika nafasi hizo kabla yetu, wakazinufaika nazo na hatimaye wakaondoka.

Alisisitiza kwamba mtu huru ni yule ambaye hajishughulishi na mambo hayo kwa namna inayomfanya asahau thamani ya uwepo wake, bali anatambua thamani yake halisi.

Akisisitiza kwamba thamani ya kweli ya mwanadamu ni Pepo, alisema kwamba: Amirul-Muuminina Ali (amani iwe juu yake) anafundisha kuwa thamani yenu haiko chini ya Pepo; kwa hiyo, msijiuze kwa thamani iliyo chini yake.

Alifafanua kwamba ikiwa mwanadamu ataachana na mambo ya muda mfupi yanayofanana na mabaki ya chakula na kujipima kwa kipimo cha Pepo, atafikiri kwa mtazamo unaoelekea Pepo, na atatamani kheri kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya wengine. Katika hali hiyo, hatawadhuru wengine wala kujinyima mwenyewe kheri.

Moyo: Kitabu kinachopaswa kusomwa

Katika kuendelea na darsa yake, Ayatullah Jawadi Amuli alinukuu maneno ya Amirul-Muuminina Ali (amani iwe juu yake):

الْقَلْبُ مُصْحَفُ الْبَصَرِ

Moyo ni kitabu cha kuona.

Kupitia kauli hiyo, alisisitiza umuhimu wa mwanadamu kuzingatia ukweli wa hali yake ya ndani. Alifafanua kwamba mwanadamu anapaswa kukisoma kitabu cha moyo wake ili kutambua moyo wake unamtaka afanye nini na unaelekea upande gani.

Akizungumzia umuhimu wa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kufanya munajati, yaani mazungumzo ya unyenyekevu na dua kwa Mola, alisisitiza kwamba moyo wa mwanadamu una uwezo wa kufanya munajati na Mola wake. Kupitia kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kutaja jina Lake, mwanadamu anaweza kuvuka umbali wa kiroho unaomtofautisha na Mola wake. Alieleza kwamba umbali wote huo unaweza kuondolewa kwa kuacha mambo yasiyo na thamani ya kudumu, yanayofanana na mabaki ya chakula.

Kadiri mwanadamu anavyosonga mbele katika njia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, ndivyo uhusiano wake na Mwenyezi Mungu unavyozidi kuwa wa karibu. Hatimaye, badala ya kusema “Ya Allah” (Ewe Mwenyezi Mungu), hufikia hatua ya kusema “Allah” (Mwenyezi Mungu).

Ukweli wa utu wa mwanadamu unavuka mipaka ya kuwa mwanamume au mwanamke

Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli alizungumzia ukweli wa roho na nafasi ya mwanadamu katika mfumo wa uumbaji, alisema kwamba katika Uislamu, tofauti ya kuwa mwanamke au mwanamume inahusiana na upande wa kimwili wa mwanadamu, lakini roho si ya kiume wala ya kike!

Akigusia aya za Qur'ani Tukufu zinazozungumzia sifa za waumini na watu wema, alisisitiza kwamba mwili ni ngazi inayoiwezesha roho kupaa; si kwamba sifa za kimwili zina nafasi katika kuamua ukweli wa roho.

Alifafanua kwamba roho ya mwanadamu husonga katika njia ya ukamilifu na kujitenga na vifungo vya kimaada. Kwa mtazamo huo, ukweli wa utu wa mwanadamu hauwekewi mipaka na hali ya kuwa mwanamume au mwanamke, wanadamu wote wanaweza kusonga mbele katika njia ya ukamilifu na kufikia daraja la mwanadamu wa ulimwengu wa Malaikut.

Ayatullah Jawadi Amuli alihitimisha hotuba yake kwa kuwaombea dua waliohudhuria kikao hicho pamoja na watu wote wanaopiga hatua katika njia ya utafiti na ukamilifu wa kielimu.

Alieleza matumaini yake kwamba watu wote watajumuishwa katika dua ya Bibi Zainab al-Kubra (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake), na kwamba mfumo wa Kiislamu utalindwa dhidi ya hatari mbalimbali kwa baraka za uangalizi na upendeleo wa Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), na hatimaye ukatolewa kwa Mtukufu Waliyyul-Asr (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha