Alhamisi 15 Oktoba 2026 - 12:00
Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa akitetea kwa moyo wake wote Wilayat Faqihi

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hashim al-Haidari alisema kuwa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah hakuichukulia Wilayat Faqihi kama suala linalomlenga mtu binafsi, bali aliiona kuwa ni dhihirisho la Wilaya ya dini na mamlaka ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hashim al-Haidari aliyasema hayo katika mkutano wa kitaaluma wa maandalizi ya kongamano lililopewa jina la Mfumo wa Mawazo na Harakati za Jihadi za Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, lililokuwa na kaulimbiu isemayo "Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah: Kielelezo cha Muqawama na Mapambano dhidi ya Dhuluma". Kongamano hilo lilifanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la Elimu la Imam Khomeini (r.a.) mjini Qum.

Akizungumzia imani thabiti ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah katika kanuni ya Wilayat Faqihi, alieleza kwamba; mojawapo ya sifa muhimu zaidi za shakhsia ya Sayyid Hassan Nasrullah ilikuwa upendo na mapenzi yake makubwa kwa Wilayat Faqihi na kwa Waliyyul-Faqihi wa zama zake.

Alifafanua kwamba; kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi na tano, Sayyid Hassan Nasrullah alisisitiza mara nyingi umuhimu wa kutetea kanuni hiyo waziwazi na bila kuficha chochote. Alikuwa akiamini kwamba katika njia hiyo, hata ikiwa maisha ya mtu yatakuwa hatarini, hapaswi kuacha kuitetea Wilayat Faqihi.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ahdullah nchini Iraq aliongeza kuwa; Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah hakuichukulia Wilayat Faqihi kama suala linalomlenga mtu binafsi, bali aliiona kuwa ni dhihirisho la Wilaya ya dini na mamlaka ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mtazamo wake, Wilayat Faqihi halikuwa tu suala la kisiasa, bali ilikuwa na mizizi katika misingi ya kiitikadi na kidini. Kwa hiyo, aliamini kwamba inapaswa kuelezwa na kufafanuliwa kwa jamii kama mojawapo ya kanuni muhimu za fikra za Kiislamu.

Uhalali wa Muqawama katika fikra za Shahidi Nasrullah ulitokana na Wilaya

Akieleza kwamba Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah aliichukulia Wilayat Faqihi kuwa msingi wa kiitikadi na kidini wa Muqawama, alisisitiza kwamba; kwa mtazamo wake, uhalali wa Muqawama nao ulitokana na Wilaya hiyo. Hivyo, kuitetea misingi hiyo ilikuwa sehemu isiyotenganishika na wajibu wa kidini na kiitikadi.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Haidari aliendelea kusema kwamba; Shahidi Nasrallah aliamini kuwa ili kuielewa kwa usahihi njia ya Muqawama, ni lazima kwanza kuifahamu na kuieleza ipasavyo misingi yake ya kiitikadi. Kwa msingi huo, hakuuchukulia utetezi wa Wilayat Faqihi kama suala la pembeni au suala la kisiasa tu, bali aliona kuwa ni mojawapo ya nguzo kuu za fikra na harakati za Muqawama.

Shahidi Nasrullah alimtii kikamilifu Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ahdullah nchini Iraq, huku akizungumzia kina cha imani na utiifu wa Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah kwa Kiongozi Mkuu Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema kwamba; imani na utiifu wake kwa Ayatullah al-Udhma Imam Khamenei (ra) vilikuwa vya kina na thabiti. Alieleza kuwa hata pale Shahidi Nasrallah alipohisi tu kwamba Kiongozi Shahidi alikuwa na ombi au matarajio fulani kutoka kwake, alikuwa akijitahidi kwa dhati kutekeleza jambo hilo.

Aliongeza kwamba mtazamo wa Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah kuhusu Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulijengwa juu ya imani yake katika nafasi ya kiongozi huyo kama Naibu wa Imam wa Zama (as). Mtazamo huo ulivuka mipaka ya masuala ya kisiasa, mahusiano ya kawaida na kauli za kimazoea za kupeana heshima. Badala yake, ulitokana na imani yake ya kina ya kidini na kiitikadi.

Shahidi Nasrullah alisisitiza uaminifu wake kwa Shahidi Imam Khamenei katika usiku wa Ashura

Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Haidari, akizungumzia jinsi Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah alivyojifunga kikamilifu kwa Wilayat Faqihi na kuwa mwaminifu kwa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema kwamba; kila mwaka katika usiku wa Ashura na siku ya Ashura, mamia ya maelfu ya watu hukusanyika mjini Beirut. Alieleza kuwa katika hafla hizo, Sayyid Hassan Nasrallah alikuwa akisisitiza ahadi na mkataba wake wa uaminifu kwa Imam Khamenei.

Akifafanua kwamba Sayyid Hassan Nasrallah alikuwa akipata msukumo kutoka katika maneno ya kihistoria ya wafuasi wa Hadhrat Sayyid al-Shuhada (as) katika usiku wa Ashura ili kueleza uaminifu wake huo, aliongeza kuwa alikuwa akitamka maneno yaleyale yaliyotamkwa na wafuasi wa Imam Hussein (as) katika usiku wa Ashura. Wafuasi hao walitangaza kwamba hata kama watauawa mara elfu moja na kufufuliwa tena, hawatamwacha kamwe Imam wao peke yake.

Utetezi wa kishujaa wa Jamhuri ya Kiislamu licha ya shinikizo kubwa

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ahdullah nchini Iraq, huku akisisitiza kwamba misimamo ya Sayyid Hassan Nasrallah katika kuitetea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitokana na imani na ushujaa wake, aliwaambia wananchi wa Iran: “Ninachotaka kuwaambia Wairani ni kwamba Sayyid Hassan Nasrallah hakulazimika kuchukua misimamo hiyo, alikabiliwa na shinikizo kubwa, lakini kwa ushujaa na heshima, aliizungumzia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mafanikio yake.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Haidari alisisitiza kwamba licha ya shinikizo kubwa alilokuwa akiwekewa Sayyid Hassan Nasrallah, alikuwa akizungumzia kwa uwazi maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuutetea mfumo ambao, licha ya kuwa chini ya vikwazo na kukabiliwa na shinikizo kubwa, uliweza kupata mafanikio mengi.

Umuhimu wa kuthamini mafanikio ya mfumo na nafasi ya uongozi

Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Haidari, akihitimisha hotuba yake kwa kusisitiza umuhimu wa kuzingatia misimamo na utendaji wa Sayyid Hassan Nasrallah katika kuitetea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alikumbusha kwamba; maneno na misimamo yake vinaonesha kuwa, licha ya shinikizo na vikwazo vyote, alikuwa akizungumzia maendeleo ya Iran yaliyopatikana chini ya uongozi wa Wilayat Faqihi na kuyatetea mafanikio hayo.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ahdullah nchini Iraq, huku akiwakosoa baadhi ya watu kwa kutoupa umuhimu unaostahili uwezo na mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisisitiza kwamba; inafaa wananchi wa Iran wautambue na kuuthamini zaidi mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, mafanikio yake na uongozi wake, huku wakizingatia umuhimu wa rasilimali hizi muhimu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha