Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ali Daamoush, Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Hizbullah, katika mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na Hizbullah ili kutangaza mradi wa makazi katika kituo cha manispaa ya Ghobeiry, katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, alisisitiza: Chaguo la mapambano ya muqawama ni dharura ya kitaifa ambayo, katika kivuli cha uwepo wa uvamizi, mashambulizi na tamaa za Kizayuni dhidi ya ardhi yetu, haiwezekani kamwe kuliacha. Muqawama huu, katika utendaji na kujitoa muhanga kwake, umeandika mashujaa wa kihistoria ambao walimzuia adui kuendelea kuikalia Kusini, na kuweka taswira nzuri zaidi ya kuitetea nchi yetu.
Alisema: Ikiwa adui huyu aliweza kukalia, kuharibu na kubomoa baadhi ya vijiji, na kufikia baadhi ya maeneo, hilo halimaanishi kwamba ameweza kuimarisha uwepo wake katika ardhi yetu; kwa sababu jukumu la muqawama si sawa na jukumu la majeshi ya kawaida. Muqawama hujitahidi kuuchosha uvamizi hadi uutoke nchini, yale yaliyotokea uwanjani ni kutokana na mizani maalumu ya nguvu, kwa vyovyote hayamaanishi kukubali mantiki ya kujisalimisha na kunyenyekea; kwa sababu mizani hii inaweza kubadilika, na Lebanon tayari imewahi kupitia hali zinazofanana ambazo zilibadilishwa kwa sababu ya irada ya watu wetu.
Sheikh Daamoush aliongeza: Serikali ya Lebanon, tangu tarehe 27 Novemba 2024, imeshindwa au imezembea katika kuhakikisha njia za kulinda mamlaka ya kitaifa. Kwa hiyo, haiwezi kuwazuia watu wake kutumia haki hii ya kibinadamu, kimaadili na kisheria. Leo tunaiomba serikali ikomeshe mfululizo wa kutoa misamaha bila malipo na kukiuka Katiba pamoja na Mkataba wa Kitaifa, na badala ya kutegemea chaguo za kigeni ambazo lengo lake ni kudhoofisha misingi ya Lebanon na kuinyang’anya uhuru, mamlaka na uthabiti wake, irejee mikononi mwa wananchi wake.
Aliwataka Walebanon watambue hatari za kipindi ambacho nchi yao inapitia, waweke maslahi ya taifa mbele ya maslahi ya kimadhehebu na kichama, na waboreshe lugha ya maelewano na mazungumzo badala ya hotuba za uchochezi na kueneza chuki; hotuba ambazo huongeza tu ukubwa wa mipasuko na umbali kati ya makundi mbalimbali ya taifa la Lebanon. Kwa sababu, lolote litakalotokea, Lebanon itaendelea kuwa nchi ya watoto wake wote.
Pia alisisitiza umuhimu unaotolewa na Hizbullah kwa ujenzi wa dola imara na yenye uadilifu, iliyojengwa juu ya msingi wa ushiriki wa kitaifa kama ilivyoelezwa katika “Hati ya Makubaliano ya Kitaifa”; dola inayowapa watoto wake wote uhakika, inayobeba wajibu kamili kwao na inayounga mkono chaguo la ukombozi kwa nyenzo zote.
Anaamini kwamba: Ujenzi upya na kuwapatia makazi wakimbizi ni wajibu wa serikali ya Lebanon, na suala hili la kibinadamu na kitaifa linapaswa kutolewa katika hesabu zote za kisiasa. Serikali haipaswi kulishughulikia suala hili kwa mtazamo wa namna hiyo, kwa sababu jambo hilo huzidisha pengo kati ya serikali na wananchi. Hadi sasa, serikali haijaliweka suala hili katika njia ya kushughulikiwa; haijafanya juhudi za kupata fedha, haijatenga mgao unaohitajika katika bajeti, wala haijakamilisha mfumo rasmi wa utekelezaji wa kupitisha utaratibu wa kukadiria hasara na kuhesabu kiwango cha fidia. Rasimu ya pendekezo kwa ajili ya jambo hili bado ipo kwenye droo za serikali, na hadi sasa haijaruhusiwa kutekelezwa.
Alisema: Sisi ndani ya Hizbullah, kwa kutekeleza wajibu wetu wa kisheria wa dini na wa kimaadili, tunaendelea kuwahudumia watu wetu na kutumia juhudi zote zinazowezekana kwa ajili ya heshima na utu wao.
Chochote tunachofanya na kukitoa, hakitoshi mbele ya mama wa shahidi anayenyanyua kwa fahari picha ya mwanawe, akijivunia alichokitoa na akiwa tayari kwa kujitoa zaidi; au mbele ya mtoto anayefunga ahadi na baba yake shahidi ya kuendeleza njia hiyo; au mbele ya familia iliyokimbia makazi yake na kupoteza mali zake zote, lakini haijapoteza imani, azma na irada yake, wala haiachi haki yake halali ya kupinga uvamizi.
Sheikh Daamoush alifafanua: Tunachofanya si mbadala wa wajibu ulio juu ya serikali, wala hatutafuti ndani yake faida yoyote ya kisiasa au ya kijamii. Hii ni ahadi na wajibu wa kidini na kimaadili kwa watu wetu wavumilivu, na tunaweka juhudi kubwa katika kutimiza wajibu huu. Wao wanayajua hayo na wanafuatilia juhudi zetu kwa subira na imani, katika muktadha huu, hatuoni kuwa ni sahihi kuzungumzia ukubwa wa jumla wa fedha katika kila hatua zilizopangwa.
Aliongeza: Ninasema hapa kwa wapendwa wetu wote: Kwa hakika ninyi ni kama alivyowataja Sayyid wa Mashahidi wa Umma, watu wenye heshima zaidi, utukufu zaidi na thamani zaidi. Mmeushangaza ulimwengu kwa kujitoa kwenu kukubwa na kuwavunja moyo maadui wa nchi yetu, ambao wamekata tamaa ya kuweza kuishinda irada yenu. Mlivumilia mashambulizi ya “Israel” na madhila mengi ya ndani, lakini mlibaki kuwa wenye kujali zaidi nchi yenu, amani yake ya ndani na kuishi pamoja kwa jamii zake mbalimbali. Hakuna yeyote aliyeweza kuwapeleka katika chaguo tofauti na lile mliloliamini: chaguo la Lebanon moja, iliyoungana, na kuishi humo kwa heshima na utu.
Aliendelea: Ninawaambia wale wenye chaguo zilizofeli, zilizojengwa juu ya dhana na ndoto zisizo na msingi, pamoja na wale walioweka dau juu ya udhaifu wetu na kurudi nyuma kutoka katika haki yetu, wakiachia huru kauli za chuki na uchochezi, na wakadhani kuwa hatuwezi kukabiliana na adui pamoja na athari za mashambulizi yake: Ninawaomba mzipitie upya hesabu zenu potofu na dau lenu lililoshindwa; kama ambavyo mnapaswa kupitia upya juhudi zenu za kukata tamaa na zisizo za kimaadili za kudhoofisha ari ya watu wetu kwa kutumia maumivu ya kukimbia makazi. Wale walioweka dau juu ya mzingiro dhalimu wa Marekani na kuutangaza, wakidhani kuwa vikwazo na kampeni za uongo za vyombo vya habari zingetuzuia kujitahidi kukidhi mahitaji ya kusimama imara. Hawakuishia hapo; baadhi ya taasisi rasmi, kwa maagizo ya pande za kigeni, pia zilitekeleza mzingiro huo ili kuzuia msaada usiwafikie waathiriwa, lakini juhudi zote hizo zilivunjika mbele ya irada ya watu wetu, na ikathibitika kwamba hakuna miongoni mwazo iliyoweza kututenganisha na wajibu wetu wa kupunguza maumivu ya watu wetu.
Mjumbe huyo mwandamizi wa Hizbullah aliongeza: Leo tunathibitisha tena kwamba sisi ni muqawama ambao haukwepi majukumu yake, na tunatoa mfano wa heshima katika kubeba wajibu huu, tunafanya kila jambo ili watu hawa wabaki wenye heshima na kuinua vichwa vyao; na, Mwenyezi Mungu akipenda, wataendelea kuwa hivyo.
Alieleza: Kwa kutegemea ahadi iliyorejelewa na Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, ya kutoa msaada wa kifedha kwa watu wetu waliojitoa mhanga, leo tunatangaza “Mpango wa Makazi” kwa ajili ya wakimbizi, au wale ambao nyumba zao zimebomolewa au kuharibiwa vibaya kiasi cha kutofaa tena kukaliwa.
Sheikh Daamoush alieleza: Lengo la mpango huu ni watu wenyewe moja kwa moja, hasa aliyeathirika ambaye amelazimika kuondoka katika makazi yake ya sasa yaliyobomolewa au kuharibiwa, na hana makazi mbadala. Huu ni mpango unaomwezesha kukodisha nyumba kwa ajili yake na familia yake, pamoja na kununua samani za nyumbani; sawa na mpango tulio utekeleza baada ya mashambulizi ya Israel mwaka 2024.
Mwisho, alisisitiza kwa kusema: Misaada na vigezo tulivyoweka kwa ajili ya mpango huu vinategemea uwezo uliopo. Vinginevyo, watu wetu wote wanastahili tuwape kila kitu, na hata tukifanya hivyo, bado hatutakuwa tumetekeleza haki yao kikamilifu.
Maoni yako