Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, swala la hijabu ndani ya Azerbaijan limebadilika kuwa janga linalokua ndani ya taasisi za elimu, walimu na wanafunzi waliovaa hijabu wamezuiliwa kuingia shuleni, na video zilizochapishwa zinaonesha wasichana wakisubiri nje ya shule na walimu wakiagana nao huku wakilia.
Mabadiliko haya yamerudisha mjadala kuhusu uhuru wa imani na haki ya elimu. Wengi wanasema mavazi ya shule hayapaswi kuwa kisingizio cha kuwazuia wasichana kupata elimu.
Baraza la Mawaziri la Azerbaijan mnamo tarehe 21 Septemba, lilipitisha marekebisho ya sheria ya mavazi shuleni; hatua ambayo mamlaka ilielezea kama kuimarisha kipengele cha sekulari katika elimu ya umma. Sheria hizo zinapiga marufuku kuvaa chochote kinachoongeza au kutofautisha mwonekano wa sare ya shule, au chochote ambacho kwa mtazamo wa mamlaka kinakiuka kanuni ya elimu ya kisekulari.
Marekebisho haya yalifuata amri ya Rais Ilham Aliyof mwezi Juni iliyopita kuhusu kuanzishwa sare moja za shule za umma; lakini utekelezaji wake katika nchi ambayo idadi kubwa ya wakazi ni Waislamu umeibua mjadala mpya kuhusu mipaka ya mfuatano wa mavazi shuleni na uhusiano wake na uhuru wa kuvaa hijabu.
Machozi na Ukandamizaji
Machozi ya walimu na wanafunzi si alama tu ya kuaga kwa muda; matukio hayo yaliibua uzito wa mgogoro ndani ya shule. Wasichana na walimu waliovaa hijabu walizuiwa kuingia, jambo ambalo lalisababisha maandamano na mwitikio mkali wa hasira, na kuifanya tena masuala ya uhuru wa imani na haki ya elimu kuwa sehemu ya ajenda ya umma.
Mwalimu mmoja wa Azerbaijan alisimulia kwamba aliombwa kuondoa hijabu yake; kabla ya kuagana akiwa na machozi machoni, alisisitiza kuwa hijabu sio kikwazo kwa utekelezaji wa majukumu yake ya kazi na alisisitiza msimamo wake wa kulinda haki zake na haki za watoto kupata elimu bila kuwacha misingi yake ya dini.
Athari za mjadala huu hazikuishia tu kwa walimu. Watumiaji wa mitandao ya kijamii waliripoti kuhusu marufuku kwa wanafunzi waliovaa hijabu kuingia shuleni, na video pamoja na picha zilizotangazwa na wanaharakati zilionesha wasichana wakiendelea kusubiri nje ya kuta za shule au katika viwanja vya shule baada ya kushindwa kuingia darasani kwa sababu ya hijabu.
Mapambano Shuleni
Kadiri mjadala ulivyoenea, wanafunzi katika baadhi ya shule walionesha mshikamano na walimu na wenzao waliokuwa wamezuiliwa kuingia kwa sababu ya kufunika kichwani, na baadhi yao walilia kwa sauti madai ya uhuru wa kuvaa hijabu.
Wanaharakati pia walisambaza picha na video za wanafunzi waliovaa hijabu wakionesha kutoridhishwa kwao kwamba mavazi ya kidini yatumike kama kisingizio cha kusababisha wasichana kutoka kwenye elimu.
Baadhi ya machapisho mitandaoni yaliripoti juu ya kupewa muda hadi mwanzoni mwa wiki kuamua kuhusu hijabu; pamoja na madai ya shinikizo juu yao, ikiwemo onyo kwamba kushikamana na hijabu kunaweza kuathiri mustakabali wao wa kielimu.
Habari juu ya kuingia mama wa mmoja wa waliouliwa katika vita vya Karabakh kwa sababu ya hijabu pia ilisababisha msisimko miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Mjadala wa Hijabu na Uhuru wa Imani
Katika muktadha wa mabadiliko haya, hasira katika mitandao ya kijamii dhidi ya kile wanachokiita wanaharakati “kupunguza uhuru wa imani ndani ya Azerbaijan” ilizidi. Waliitaka mamlaka ieleze kwa uwazi sababu za marufuku ya hijabu katika taasisi za elimu na wahakikishe haki za wanafunzi na walimu kufanya ibada zao bila kubaguliwa au kuwanyanyasa kwa kukosa haki ya kuingia darasani.
Weblog kadhaa zinaamini kuwa kuvaa hijabu haipaswi kuwa kisingizio cha kuwazuia wasichana kupata elimu na walisisitiza kuwa haki ya elimu haipaswi kutokuwa na mzozo na uhuru wa imani; sheria za shule hazipaswi kutumika kama chombo cha kuwabagua wanafunzi kutokana na uchaguzi wao wa kidini.
Mjadala huu pia umegusa nafasi ya mashirika yanayohusika na haki za wanawake; watumiaji walitaka kujua msimamo wa mashirika hayo kuhusu marufuku ya kuingia shuleni kwa waliovaa hijabu, wakisisitiza kwamba utetezi wa haki za wanawake na uhuru wao wa kuchagua unapaswa kuhusisha pia wale walioteuliwa kuvaa hijabu kwa hiari yao.
Wakati mjadala ulipozidi, watumiaji waliripoti upungufu wa mtandao nchini Azerbaijan, hasa kwenye majukwaa kama Instagram, TikTok na programu nyingine zinazowezesha kubadilishana video.
Maoni yako