Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, katika hatua mpya ya mapambano inayoonesha msimamo thabiti wa wananchi wa Morocco juu ya msimamo wao wa kihistoria usioyumba kuhusu kadhia ya Palestina, miji mingi nchini Morocco imeshuhudia katika siku za hivi karibuni shughuli kubwa za wananchi za kuadhimisha mwaka wa tatu wa vita vya “Tufani ya Al-Aqsa”, kufuatia wito wa “Jukwaa la Morocco la Kuiunga Mkono Palestina na Kupinga Uhalalishaji wa Mahusiano” pamoja na “Kamati ya Morocco ya Kusaidia Masuala ya Umma”.
Matukio haya yameonesha tena upinzani mkali wa Wamorocco dhidi ya aina zote za kuhalalisha mahusiano na utawala wa Kizayuni, na kutangaza mshikamano kamili na mapambano ya kishujaa ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza na Palestina yote inayokaliwa kwa mabavu.
Washiriki wa shughuli hizi, huku wakieleza fahari yao kwa uthabiti wa wananchi wa Palestina na kujitolea kwao katika kukabiliana na uvamizi endelevu wa Kizayuni, walisisitiza kwamba; kumbukumbu ya Tufani ya Al-Aqsa itaendelea kubaki kama kipindi muhimu katika historia ya kadhia ya Palestina na nembo ya kushikamana na haki halali za watu wa Palestina za uhuru na kujitegemea.
Meknes: Maandamano Makubwa ya Wananchi
Katika mji wa Meknes, kufuatia wito wa sekretarieti ya eneo ya “Jukwaa la Morocco la Kuiunga Mkono Palestina na Kupinga Uhalalishaji wa Mahusiano”, maandamano ya wananchi ya kupinga, kwa ajili ya kuwaunga mkono watu wa Palestina, yalifanyika kuanzia saa kumi na moja jioni. Maandamano hayo makubwa yalianzia katika uwanja wa kihistoria wa “Al-Hadim” kuelekea katikati ya mji wa “Hamriya”, yakipita katika njia iliyofurika wananchi waliotoa hisia zao za ghadhabu kubwa dhidi ya uhalifu unaoendelea wa utawala vamizi wa Kizayuni.
Katika maandamano hayo, kauli mbiu zenye nguvu na athari kubwa zilitolewa, zikieleza kupinga kuhalalishwa uovu huu wa mahusiano, na kusisitiza nafasi ya msingi ya kadhia ya Palestina katika dhamiri ya wananchi wa Morocco.
Mohammed Al-Ghafri, mmoja wa wanaharakati katika uwanja huu, alisisitiza: Uamuzi wa kuhalalisha mahusiano na Wazayuni ni uamuzi wa maovu. Pia alilaani kwa ukali uamuzi wa kuinua kiwango cha mahusiano ya kidiplomasia kati ya serikali ya Morocco na utawala wa Kizayuni.
Al-Ghafri alionya kuhusu athari hatari za uamuzi huu, ambao unakwenda kinyume na mwelekeo, matakwa na matarajio ya wananchi wote wa Morocco. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mapambano ya kufuta uhalalishaji wa mahusiano na utawala wa Israel, na huku akikariri ahadi ya kudumu na msimamo thabiti, alisema: “Tutabaki katika jukwaa, mitaani na katikati ya medani; tutaendelea kupambana bila kuchoka hadi kuhalalishwa mahusiano na Israel kufutwe, na Palestina ikombolewe kikamilifu kutoka mto hadi bahari.”
Taza na Oujda: Muendelezo wa Mapambano na Uhamasishaji Endelevu wa Wananchi
Maandamano hayakuishia katika mji mkuu wa Morocco pekee, bali yalienea hadi katika miji mingine. Mji wa Oujda ulishuhudia mkusanyiko wa mshikamano uliofanyika kufuatia wito wa “Jukwaa la Morocco la Kuiunga Mkono Palestina na Kupinga Uhalalishaji wa Mahusiano” mjini Oujda. Washiriki walitoa kauli mbiu za kuunga mkono mapambano ya Wapalestina na kusisitiza ulazima wa kuendeleza uhamasishaji wa wananchi ili kuzitetea haki halali za watu wa Palestina.
Katika muktadha huo, Uwanja wa “Istiqlal” katika mji wa Taza ulikuwa mwenyeji wa mkusanyiko mkubwa wa mshikamano, kufuatia wito wa “Kamati ya Morocco ya Kusaidia Masuala ya Umma”. Sauti za ghadhabu za wananchi zilisikika kupitia kauli mbiu za kupinga kuinuliwa kiwango cha uwakilishi wa kidiplomasia wa utawala wa Kizayuni nchini Morocco.
Shughuli hiyo ilimalizika kwa dua za kuwatakia wapiganaji wa Ghaza na maeneo yote ya Palestina ushindi na uthabiti.
Mikusanyiko hii na maandamano haya yanasisitiza tena kwamba kadhia ya Palestina itabaki kuwa kadhia ya kitaifa ya watu wote huru wa Morocco, wanawake kwa wanaume.
Maoni yako