Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kitabu kiitwacho Mijadala Mia Moja na Moja ya Kuvutia na Yenye Kusomwa kwa Raha, kilichoandikwa na Muhammad Muhammadii Ishtihardi, kimekusanya mijadala mbalimbali kuhusu masuala ya kiitikadi na kidini, ambacho Shirika la habari la Hawza litakichapisha katika sehemu mbalimbali.
Mmoja wa Masahaba wakubwa wa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa Ammar Yasir, baada ya Mtume (s.a.w.w.), daima aliendelea kushikamana na njia ya Uislamu halisi na kumfuata Imam Ali (a.s.), hadi alipouawa shahidi katika Vita vya Siffin.
Mtume (s.a.w.w.) alimwambia:
“Litakuuwa wewe kundi la waasi.”
Waislamu waliisikia kauli hii, na ikajulikana miongoni mwao kwamba Mtume (s.a.w.w.) alisema hivyo kumuhusu Ammar.
Miaka ikapita tangu tukio hilo, mpaka katika zama za ukhalifa wa Imam Ali (a.s.), vita vilizuka kati ya jeshi lake na jeshi la Muawiya, navyo vikajulikana kama Vita vya Swiffin. Katika vita hivi, Ammar Yasir alikuwa katika safu ya jeshi la Imam Ali (a.s.), na hatimaye, baada ya kujitoa mhanga sana, aliuawa na wanajeshi wa Muawiya.
Wale waliokuwa na shaka iwapo Muawiya alikuwa katika haki au Ali (a.s.), walitambua kupitia tukio hili kwamba, kwa mujibu wa kauli ya Mtume (s.a.w.w.), jeshi la Muawiya ndilo lilikuwa jeshi la kidhalimu, kwa kuwa lilimuua Ammar Yasir, hivyo Muawiya alikuwa katika batili.
Hapo Muawiya aliona tukio hili limevuruga ari ya jeshi lake na limeibua mgawanyiko. Mara moja, kwa kutumia upotoshaji akatangaza: “Ali (a.s.) ndiye aliyemuua Ammar Yasir, si mimi; kwa sababu kama Ali asingemtuma kupigana nami, asingeuawa!”
Kauli hii ya Muawiya iliwapotosha baadhi ya Waislamu.
Imam Ali (a.s.), akijibu upotoshaji huo, alisema mara moja: “Ikiwa maneno ya Muawiya ni sahihi, basi itabidi tuseme kwamba Mtume (s.a.w.w.) ndiye aliyemuua Sayyiduna Hamza (a.s.), aliyeuawa na washirikina katika Vita vya Uhud, kwa sababu alimpeleka vitani!”
Abdullah, mwana wa Amr ibn al-As, alimfikishia Muawiya jibu hili. Muawiya alikerwa, akaghadhibika na kufedheheka sana kiasi kwamba alimwambia Amr ibn al-As, mshauri wake wa karibu mwenye hila: “Mtoe mwanao mpumbavu katika kikao hiki!”
Rejea:
1. U’yun al-Shi‘ah, Juzuu ya 42, ukurasa wa 215
Maoni yako