Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Muhammad al-Dulaimi, Balozi wa Jamhuri ya Yemen nchini Iran, alitembelea makao makuu ya Chama cha Mu'talifa cha Kiislamu, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Asadullah Badamchian, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la chama hicho.
Katika mkutano huo, pande hizo mbili zilijadili maendeleo ya hali nchini Yemen na katika eneo la Mashariki ya Kati, uhusiano wa kisiasa na vyama, pamoja na njia za kupanua ushirikiano wa pamoja.
Katika mazungumzo hayo, Muhammad al-Dulaimi alizungumzia hali ya ulimwengu wa Kiislamu na maendeleo ya mambo nchini Yemen, akisema: “Wale walioichafua Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kulikabidhi pazia la Nyumba ya Mwenyezi Mungu na Al-Kaaba kwa Epstein ni ukoo wa Aal Saud. Wale waliomleta mwimbaji mwanamke asiyejisitiri huko Makkah ni ukoo wa Aal Saud, tunafahamu kuwa Chama cha Mu'talifa cha Kiislamu kina uhusiano na vyama na ndugu zetu wa Uturuki na Pakistan, na tunaomba mshirikiane nasi pia katika suala hili.”
Akifafanua mafanikio yaliyopatikana katika uwanja wa mapambano na wanamapambano wa Ansarullah, alisema: “Tumepata ushindi mkubwa kwa kutumia rasilimali chache sana, wakati adui wetu ana wapiganaji 80,000 wenye vifaa bora zaidi na ulinzi wa anga. Eneo lililokombolewa lina ukubwa wa kilomita za mraba 6,000, ambalo ni sawa na nusu ya eneo la Lebanon, na lilitekwa ndani ya siku tano. Aidha, visiwa vinne muhimu pia vilitekwa.”
Balozi wa Yemen aliendelea kwa kuzungumzia wajibu wa Waislamu katika kuwatetea watu wanaodhulumiwa katika ulimwengu wa Kiislamu, akisisitiza: “Hapo zamani, Waislamu walikuwa wakidhulumiwa na kuteswa nchini India, Myanmar na maeneo mengine duniani, nilikuwa nikijiuliza: Tunawezaje kuwasaidia ilhali wako mbali nasi? Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) amesema: ‘Mtu yeyote anayesikia wito wa Mwislamu, lakini asiuitikie wala kumkimbilia kumsaidia, basi huyo si Mwislamu.’ Sasa, kwa kuwepo bahari hizi mbili nyembamba za kimkakati zilizo chini ya udhibiti wetu na wenu, hakuna mtu atakayethubutu kuwatesa Waislamu au kufanya mauaji ya kimbari dhidi yao popote duniani.”
Katika sehemu nyingine ya mkutano huo, Asadullah Badamchian, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Chama cha Mu'talifa cha Kiislamu, alizungumzia maendeleo ya eneo hilo na harakati za muqawama za wananchi, akisema: “Nchini Lebanon, serikali inashirikiana na nchi za Magharibi, lakini wananchi wanapinga na kuendeleza mapambano ya muqawama.”
Akikumbusha mwongozo wa Imam Khomeini (r.a.), aliongeza kuwa: “Imam, ambaye alianzisha Chama cha Mu'talifa cha Kiislamu, alikuwa akisema kwamba; iwapo umma wote wa Kiislamu ungemimina ndoo moja ya maji, Israel ingesombwa na mafuriko.”
Badamchian pia alizungumzia maendeleo ya kimataifa, akisema: “Mwaka huu, katika Umoja wa Mataifa, hotuba za Trump zilikuwa za kipumbavu, ilhali hotuba ya Rais wa Iran ilikuwa ya kihistoria. Mambo yamefikia hatua ambapo ukoo wa Aal Saud unaiomba Marekani kwa kusisitiza iingilie kati, lakini kutokana na matokeo mabaya yanayoweza kufuatia hatua hiyo, Marekani haiingilii kati.”
Mwenyekiti huyo wa Baraza Kuu la Chama cha Mu'talifa cha Kiislamu alihitimisha kwa kusisitiza uungaji mkono kwa mhimili wa muqawama, akisema: “Kila usiku, katika swala yangu ya usiku, ninamuombea Bwana Badruddin al-Houthi, wafikishieni wapiganaji wa Yemen salamu zetu za pongezi.”
Katika mkutano huo, pande hizo mbili pia zilijadiliana kuhusu maendeleo ya hivi karibuni nchini Yemen, hali ya eneo la Mashariki ya Kati, suala la Palestina, njia za kuendeleza ushirikiano wa kisiasa na wa vyama, pamoja na kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa pamoja.
Maoni yako