Jumapili 11 Oktoba 2026 - 21:50
Msimamo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi unatokana na mafundisho na Sunna za Mwenyezi Mungu

Ayatullah Abdullahiy, huku akisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kujitahidi kufafanua vipengele vinavyodhihirisha nguvu na utukufu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema: “Kutegemea nguvu za Mwenyezi Mungu ndiyo siri ya maendeleo na uimara wa taifa na nchi ambayo, kwa mujibu wa vipimo na hesabu za Mwenyezi Mungu, inahesabiwa kuwa nchi yenye nguvu kubwa zaidi duniani.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Mahmoud Abdullahiy, katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, huku akizungumzia umuhimu wa kufanya uchambuzi wa kina na sahihi wa ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu uliotolewa katika maadhimisho ya Wiki ya Ulinzi Mtakatifu, ambapo alisisitiza kwamba; “Kwa mujibu wa vipimo na hesabu za Mwenyezi Mungu, Iran ndiyo nguvu ya kwanza duniani,” alisema: “Kabla ya jambo lolote jingine, wajibu wa vyombo vya habari unavitaka vituo vya habari na waandishi wa habari kujitahidi kwa dhati na kwa kiwango kinachostahili kuwafahamisha wasikilizaji na wasomaji kuhusu maudhui ya ujumbe huu. Hii ina maana kwamba hata misimamo na kauli za watu mashuhuri wa kigeni walioutaja mfumo wetu kuwa ni mfumo wenye uhai, unaoendelea na wenye ufanisi, zinapaswa kuripotiwa kwa uwazi, huku ukweli huu ukiwekwa bayana.”

Muqawama wenye mizizi katika imani ya Mwenyezi Mungu

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza alisisitiza pia: “Watu wa Muqawama na mapambano wanamtegemea Mwenyezi Mungu, ambaye ameumba mfumo mzima wa ulimwengu na ambaye ‘مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ’ — funguo za mbingu na ardhi ziko mikononi Mwake.

“Sababu na mambo yote yaliyomo ulimwenguni yako chini ya mamlaka Yake na yanaendeshwa kwa mujibu wa mipango Yake, kwa sababu Yeye ndiye Muumba, Mola na Karimu. Mtazamo huu unatokana na mafundisho ya Mwenyezi Mungu, na watu hawa wanamtegemea Mola ambaye uendeshaji wa ulimwengu uko mikononi mwa uwezo Wake.”

Ayatullah Abdullahiy alisema: “Kwa kuzingatia uzoefu wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu, hata tukirejelea kipindi cha kabla ya Mapinduzi hayo, pamoja na uzoefu wa vita vya miaka minane vya Ulinzi Mtakatifu, ambapo ulimwengu wote wa kimaada na mataifa makubwa yalikuwa yakimuunga mkono adui, tulishuhudia msaada wa Mwenyezi Mungu.

“Hasa katika kila ushindi mkubwa uliopatikana na mfumo wetu, kama vile ushindi wa kukombolewa kwa Khorramshahr, operesheni ya Karbala 5 na ushindi mwingine mbalimbali, madola ya kibeberu yaliweza kutambua nguvu na uwezo wa Iran, licha ya nchi hiyo kuwa katika hali ya kudhulumiwa na kukabiliwa na mashinikizo makubwa. Hali hiyo iliyafanya madola hayo kuingiwa na hofu, kwa sababu yaliona kwamba maendeleo ya Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu yalikuwa yakiupa msaada mstari wa Muqawama katika kukabiliana na ubeberu duniani.”

Siri ya maendeleo na uimara wa taifa la Iran mbele ya maadui

Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi wa Iran alisema pia: “Hata hivyo, swali muhimu linalojitokeza ni hili: Ni sababu gani iliyowezesha maendeleo haya na uimara mbele ya mashinikizo yote ya adui? “Jibu ni kwamba; hali hii ilitokana na sababu moja tu, nayo ni kwamba wananchi walimtegemea na kujiegemeza kwa Mola na Mwenyezi Mungu, Mmiliki wa ulimwengu.”

Aliongeza: “Tunakumbuka kwamba wakati Waziri Mkuu wa wakati huo wa Japan alipomfikishia Kiongozi wetu Shahidi ujumbe kutoka kwa Rais wa Marekani, ambaye anadai kuwa nchi yake ni dola kuu yenye nguvu kuliko mataifa yote, Kiongozi wetu mwenye hekima hakuuona ujumbe huo kuwa na umuhimu wowote. Alisema kwamba hamuoni mtu huyo kuwa anastahili hata kuzungumziwa. “Msimamo huu thabiti uliojaa nguvu na mamlaka unaonesha wazi tegemeo lile lile la kiroho na la Mwenyezi Mungu ambalo watu wenye msimamo wa kupinga dhuluma na wanaomtegemea Mwenyezi Mungu huwa nalo.”

Mwalimu wa masomo ya juu ya elimu ya kidini katika Hawza ya Qum alikumbusha pia: “Vilevile, wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kuuawa kishahidi kwa mpiganaji mkubwa Sayyid Hassan Nasrullah, tulikuwa tukishuhudia kwamba kila alipozungumza, maadui walikuwa wakitetemeka kwa hofu. Maneno yake yalikuwa yakiwachochea watu huru duniani kuchukua hatua, na alikuwa akitambuliwa kama shujaa wa Umma wa Kiarabu.

“Je, ushawishi na nguvu hizi zilitokana na kuwa na vifaa na rasilimali nyingi za kimaada? Hapana! Bali, zilitokana na ukweli kwamba alikuwa mwanadamu mwenye imani na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu hiyo, msaada na neema za Mwenyezi Mungu zilikuwa pamoja naye.”

Msimamo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi unatokana na mafundisho na Sunna za Mwenyezi Mungu

Ayatullah Abdullahiy, akihitimisha mazungumzo yake, alisema: “Kwa hiyo, inabainika kwamba maneno na misimamo ya sasa ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu inatokana na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na Sunna za Mola. “Sunna hizo zimekuwa zikijidhihirisha wazi katika kipindi chote cha historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na tangu mwanzo wa Uislamu, kupitia harakati za Mtume Mkuu wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), utume wake, harakati ya mapambano ya Ashura na katika vipindi vingine mbalimbali vya historia, aidha uzoefu wetu wa kihistoria unathibitisha ukweli wa mafundisho hayo.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha