Jumapili 11 Oktoba 2026 - 20:20
Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf Aishukuru Haram Tukufu ya Imam Hussein kwa Kuwapokea Wagonjwa wa Palestina na Kugharamikia Matibabu Yao

Hawza/ Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi ametoa shukrani zake kwa hatua ya Haram Tukufu ya Imam Hussein (a.s.) ya kuwapokea wagonjwa wa Kipalestina na kugharamia matibabu pamoja na usafirishaji wao bila malipo. Ameitaja hatua hiyo kuwa ni ishara ya nafasi ya Marjaa wa kidini na msimamo wa wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s.) katika kuhusiana na Waislamu wengine.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi, ambaye ni Imam wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, alieleza hayo katika khutuba ya Swala ya Ijumaa iliyotolewa katika Husainiya Kubwa ya Fatimiyya, mjini Najaf Ashraf, ambapo alizungumzia masuala mbalimbali ya ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.

Tunaishukuru Haram Tukufu ya Imam Hussein kwa Kuwapokea Wagonjwa wa Palestina

Akizungumzia hatua ya kibinadamu iliyochukuliwa na Haram Tukufu ya Imam Hussein (a.s.), Sayyid Qabanchi alisema kuwa haram hiyo imetangaza utayari wake wa kuwapokea wagonjwa wa Kipalestina na kugharamia matibabu pamoja na usafirishaji wao bila malipo yoyote.

Akiishukuru Haram Tukufu ya Imam Hussein kwa hatua hiyo, aliongeza kuwa; hatua hiyo ina maana na ujumbe mkubwa kuhusu nafasi ya Marjaa wa kidini na msimamo wa wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s.) katika kuhusiana na Waislamu wengine.

Kuongezeka kwa Bei ya Dola: Serikali Inapaswa Kulipa Mishahara ya Watumishi kwa Dola

Katika sehemu nyingine ya khutuba yake, iliyohusu masuala ya ndani ya Iraq, Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alizungumzia kupanda kwa kiwango cha ubadilishaji wa fedha za kigeni, akibainisha kuwa hali hiyo imesababisha kutoridhika wananchi. Kwa msingi huo, aliiomba serikali kutafakari upya uamuzi huo.

Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi alieleza kuwa mafuta ya petroli yanachangia takribani asilimia 90 ya mapato ya kifedha ya Iraq, huku utalii wa kidini ukichangia asilimia 3 pekee.

Akisisitiza kuwa, licha ya kuwepo matatizo ya muda katika uuzaji na usafirishaji wa mafuta nje ya nchi, ni muhimu kutafuta suluhisho la changamoto hizo, alisema kuwa suala hilo linapaswa kuzingatiwa hasa kwa kuzingatia tangazo la serikali kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz uko wazi kwa meli kubwa za mafuta za Iraq, ambazo mwezi uliopita zilisafirisha mapipa milioni nne ya mafuta.

Katika muktadha huo, aliuliza: “Ikiwa kuna ulazima wa kushusha thamani ya dinari ya Iraq, basi serikali inapaswa kuwalipa watumishi wake mishahara kwa dola.”

Kukosoa Juhudi za Kuunda Muungano Dhidi ya Harakati ya Ansarullah

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alizungumzia juhudi za kuunda muungano wa kikanda na kimataifa dhidi ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Alisema kuwa mkuu wa Baraza la Uongozi la Rais katika serikali ya Yemen iliyojiuzulu anatoa wito wa kuundwa muungano unaojumuisha Israel, Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan, chini ya uongozi wa Marekani, kwa lengo la kukabiliana na Harakati ya Ansarullah.

Aliongeza kuwa; katika mazingira hayo, baadhi ya ndugu katika eneo hilo wameiomba serikali ya utawala wa Kizayuni kujiunga na muungano huo dhidi ya Ansarullah, kwa madai ya kukabiliana na hatari ya kufungwa Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab.

Sayyid Qabanchi alibainisha kuwa hali hiyo inaonesha namna ukoloni unavyojaribu kuifanya Israel ionekane kuwa ni ndugu na mshirika katika juhudi hizo, huku Harakati ya Ansarullah ikichukuliwa kuwa adui.

Alimalizia sehemu hiyo kwa kusema:

إنا لله وإنا إليه راجعون

Khutuba ya Kidini: Ahlul-Bayt (a.s.) Ndiyo Njia ya Wokovu

Katika sehemu ya khutuba yake iliyohusu masuala ya kidini, baada ya kuwausia waumini wamche Mwenyezi Mungu na kuzingatia uchamungu, Sayyid Qabanchi alisema kuwa mada ya khutuba yake ilikuwa: “Ahlul-Bayt (a.s.) ndiyo njia ya wokovu.”

Katika kueleza mada hiyo, alirejea hadithi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) isemayo:

مثل أهل بيتي فيكم مثل سفينة نوح، من ركبها نجا، ومن تخلف عنها غرق وهوى

“Mfano wa Ahlul-Bayt wangu miongoni mwenu ni kama Safina ya Nabii Nuhu. Yeyote atakayeipanda ataokoka, na yeyote atakayeiacha nyuma atazama na kuangamia.”

Wilaya ya Ahlul-Bayt (a.s.) Ni Sharti la Kukubaliwa Matendo

Katika kuendeleza maelezo yake kuhusu umuhimu wa kushikamana na Ahlul-Bayt (a.s.), Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alisimulia riwaya mbili zinazosisitiza umuhimu wa wilaya—yaani, kukubali uongozi na mamlaka ya Ahlul-Bayt (a.s.).

Riwaya ya kwanza imenukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Hussein Zainul-Abidin (a.s.), ambaye amesema:

أفضل البقاع ما بين الركن والمقام، ولو أن عبداً عمّر ما عمّر نوح في قومه، يصوم نهاراً ويقوم ليلاً، ثم لقي الله عز وجل بغير ولايتنا، لم ينتفع بذلك شيئاً

“Sehemu bora zaidi ni eneo lililo baina ya Rukn na Maqam. Lau mja angeishi kwa muda mrefu kama kipindi ambacho Nabii Nuhu aliishi miongoni mwa watu wake, akifunga saumu wakati wa mchana na kusimama kwa ibada wakati wa usiku, kisha akakutana na Mwenyezi Mungu bila kuwa na wilaya yetu, basi asingenufaika na chochote kutokana na ibada hizo.”

Kupitia riwaya hii, Sayyid Qabanchi alisisitiza umuhimu wa wilaya ya Ahlul-Bayt (a.s.), akieleza kuwa ibada nyingi pekee hazitoshi ikiwa mtu hatashikamana na uongozi wao kama inavyosisitizwa katika mafundisho hayo.

Kisha Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alinukuu riwaya ya pili kutoka kwa Imam Ja'far Swadiq (a.s.), inayohusu mmoja wa wanazuoni wa Bani Israil aliyekuwa amejitolea sana katika ibada.

Imam Ja'far Swadiq (a.s.) amesema:

إنّ عبداً من أحبار بني إسرائيل، أي من علمائهم، عبد الله حتى صار مثل الخلال، أي نحيفاً من كثرة العبادة، فأوحى الله عز وجل إلى نبي زمانه: قل له: وعزتي وجلالي وجبروتي، لو أنك عبدتني حتى تذوب كما تذوب الألية في القدر، ما قبلت منك حتى تأتيني من الباب الذي أمرتك

“Hakika kulikuwa na mja mmoja miongoni mwa wanazuoni wa Bani Israil, ambaye alimwabudu Mwenyezi Mungu mpaka akawa mwembamba sana kutokana na wingi wa ibada, kiasi cha kufanana na kijiti chembamba. Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akamfunulia Nabii wa zama zake, akamwambia: ‘Mwambie: Naapa kwa utukufu Wangu, adhama Yangu na nguvu Zangu zisizoshindika! Lau ungeendelea kuniabudu mpaka ukayeyuka kama mafuta yanavyoyeyuka ndani ya chungu, nisingekubalia ibada yako mpaka uje Kwangu kupitia mlango ambao Nimekuamuru uupitie.’”

Kupitia riwaya hii, Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alielekeza fikra za waumini katika umuhimu wa kufuata njia ambayo Mwenyezi Mungu ameielekeza, akisisitiza kuwa juhudi za ibada zinapaswa kuambatana na kufuata mafundisho na mwongozo wa Mwenyezi Mungu.

Khutuba hiyo iliunganisha masuala ya kibinadamu, changamoto za kiuchumi na matukio ya kisiasa ya kikanda na kimataifa na mafundisho ya kidini yanayosisitiza nafasi ya Ahlul-Bayt (a.s.) katika mwongozo na wokovu wa mwanadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha