Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, jamii inayodai kuwa ya Kiislamu itakuwa ya Kiislamu kwa maana halisi ya neno pale tu ambapo nguzo zake zote zitakuwa zimejengwa kwa kuufuata mwenendo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w) si shakhsia ya kihistoria tu, bali ni kiumbe “kinachofanana na galaksi”, na ni taa inayong’aa kwa ajili ya wanadamu wote hadi mwisho wa historia. Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, kwa kutoa misingi 20, anatutska kuuchunguza mwenendo huu “hata kwa kiwango cha milimita” ili kuujenga ulimwengu wa leo.
Maandishi haya ni marejeo ya misingi hiyo kwa ajili ya kuchora ramani ya njia ya kufikia jamii ya Kinabii.
Ayatullah Shahidi Imam Khamenei (Mwenyezi Mungu autakase moyo wake na kuutukuza) anaamini kwamba jamii itakuwa ya Kiislamu kwa maana halisi pale itakapoulinganisha mwenendo wake na mwenendo wa Mtume.
Katika makala hii, kauli 20 zilizochaguliwa kutoka katika hotuba za Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi kuhusiana na “Mtume Mtukufu” zimeangaliwa upya:
1. Mtume Mtukufu ni kiumbe kinachofanana na galaksi, na ndani yake kuna maelfu ya nukta zinazong’aa za fadhila. 01/01/1385
2. Mtume ni mfano kamili ambaye Mwenyezi Mungu hakumuumba kiumbe mwingine yeyote katika ulimwengu wa uwepo aliye mkamilifu zaidi kuliko yeye. Yeye ni mlinganiaji wa wanadamu wote kumuelekea Mwenyezi Mungu na ni taa inayong’aa inayowaongoza wanadamu katika njia yao. 01/01/1385
3. Mtume wa Uislamu alikuwa mwalimu wa kila wema na mwalimu wa uadilifu, ubinadamu, maarifa, udugu, ukuaji, ukamilifu na maendeleo endelevu ya mwanadamu hadi mwisho wa historia. 18/02/1383
4. Kwa Mtume, ibada ya Mwenyezi Mungu iliambatana na kuwatumikia viumbe. 01/01/1385
5. Mtume alikuwa mwenye kujiheshimu na kujilinda na maovu ya kimaadili; katika mazingira yale yaliyokuwa yameharibika kimaadili ya Waarabu kabla ya Uislamu, wakati wa ujana wake, Mtume huyo mkubwa alijulikana kwa usafi wa maadili na haya. 23/02/1379
6. Mtume Mtukufu hakuwahi kusahau tabia ya kuwa karibu na watu, upendo na upole kwa watu, pamoja na juhudi za kuweka uadilifu miongoni mwao; aliishi kama watu wengine na katikati ya watu. 05/07/1370
7. Mtume alipokuwa pamoja na watu, daima alikuwa mwenye furaha na uso wa bashasha. Alipokuwa peke yake, ndipo huzuni, majonzi na hofu aliyokuwa nayo vilipojitokeza. 23/02/1379
8. Mwenendo wa Mtume ni kwamba, alikuwa karibu na mafukara, wanyonge na watu wa aina hiyo. Hakuyapa umuhimu mambo ya nje na vitu ambavyo kwa mwonekano vinaweza kuwa sababu ya utukufu, fahari na hadhi. 03/10/1398
9. Waislamu katika jamii ya Kiislamu wanapaswa kutoka katika hali ya kutojali hali za wenzao. Miongoni mwa vipengele vya maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni kubadilisha mazingira ya kutojali kuwa mazingira ya upendo, ushirikiano na udugu, na kujenga jamii ya watu wanaoshirikiana wao kwa wao. 28/07/1368
10. Mtume wa Uislamu alikuwa jasiri, na hakuna safu kubwa ya maadui iliyoweza kumtikisa au kumtisha. 23/02/1379
11. Mtume hakuwahi kulegea hata kwa muda mfupi katika uwanja wa kulingania watu na jihadi. Kwa nguvu aliiongoza jamii ya Kiislamu mbele, mpaka akaifikisha katika kilele cha heshima na nguvu. 05/07/1370
12. Katika siku ya heshima, katika siku ya udhalili, katika siku ya shida, katika siku ya faraja; katika hali zote kumkumbuka Mwenyezi Mungu, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kumuomba Mwenyezi Mungu — hili ndilo somo kubwa ambalo Mtume ametufundisha. 05/07/1370
13. Maadili ya kiuongozi ya Mtume yalikuwa hivi: mbele ya vishawishi vya adui, alikuwa macho na mwenye tahadhari; mbele ya Waumini, alikuwa mnyenyekevu. 23/02/1379
14. Kwa uthabiti wa Mtume, katika mahali ambapo hakuna akili yoyote iliyoweza kudhani kwamba jambo hilo lingewezekana, hema la ustaarabu wa kudumu wa mwanadamu lilisimikwa katikati ya jangwa kame la Arabia:
«فَلِذَلِكَ فَادْعُ وَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ»
“Basi kwa ajili ya hayo, lingania na simama imara kama ulivyoamrishwa.” 23/02/1379
15. Mtume aliifanya historia yote itawaliwe na fikra yake na akaacha athari kubwa juu yake. 28/02/1380
16. Katika dini na utamaduni wa Mtume Mkuu hakuna kusimama, kubaki nyuma, kushikilia misimamo migumu na ya kizamani, wala kukata tamaa; Mtume wetu alipambana dhidi ya kukata tamaa. 01/01/1385
17. Jina, kumbukumbu, maisha, mwenendo na mafundisho ya Mtume vinaweza kuutoa Umma wa Kiislamu katika hali ya kulegea na kuupa uchangamfu. 22/12/1386
18. Sisi Waislamu, tukimzingatia na kumchunguza kwa kina Mtume Mtukufu na kutaka kujifunza kutoka kwake, tutapata ndani yake kile kinachotutosheleza kwa ajili ya dini na dunia yetu. 21/11/1390
19. Maisha ya Mtume yanapaswa kuchunguzwa kwa umakini mkubwa, hata kwa kiwango cha milimita. Kila muda katika maisha haya una tukio, funzo na dhihirisho kubwa la utu wa mwanadamu. 09/05/1387
20. Jamii yetu ya Kiislamu itakuwa jamii kamili ya Kiislamu kwa maana halisi ya neno, pale tu itakapojilinganisha na kuoanisha mwenendo wake na mwenendo wa Mtume. 05/07/1370
Zingatia: Tarehe na Miaka iliyoainishwa hapo ni kulingana na miaka ya Hijria - Shamsia.
Maoni yako