Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya Kielimu ya Najaf Ashraf, alisisitiza kwamba; matembezi ya Arubaini si tukio la kidini au ibada pekee, bali ni nembo kubwa ya Mwenyezi Mungu yenye nyanja za kidini, kisiasa, kijamii na kiustaarabu, ambayo inaonesha mwendelezo wa kweli wa harakati ya Imam Hussein (as) na ujumbe wa Uislamu katika kupambana na dhulma na utawala wa kitaghuti.
Akieleza kuwa; kutembea kwa miguu kuelekea kwenye Haram Tukufu ya Imam Hussein (as) ni jambo lililohimizwa katika riwaya za Ahlul-Bayt (as), alisema: Ziara ya Arubaini tarehe ishirini ya mwezi wa Safar imesisitizwa wazi katika hadithi za Imam Sadiq na Imam Hadi (as), na katika riwaya imehesabiwa kuwa miongoni mwa alama za Muumini. Kama ilivyokuja katika hadithi maarufu:
"Alama za Muumini ni tano: Kuswali rakaa hamsini na moja, kusujudu juu ya udongo, kufanya Ziara ya Arubaini, kuvaa pete katika mkono wa kulia, na kusema kwa sauti 'Bismillahir Rahmanir Rahim'."
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliongeza: Ziara hii ina mizizi ya kihistoria yenye kina, inayorejea kwenye kurejea kwa msafara wa Ahlul-Bayt wa Mtume Mtukufu (saww) mjini Karbala, pamoja na ziara ya Jabir bin Abdullah Al-Ansari katika kaburi tukufu la Imam Hussein (as). Hata hivyo, falsafa yake ya kweli inapita zaidi ya tukio la kihistoria, kwani inadhihirisha mafundisho ya kujitolea, ushahidi na kupambana na dhulma.
Alisisitiza: Kaburi tukufu la Sayyidush-Shuhadaa (as) katika historia yote limekuwa kitovu cha harakati dhidi ya tawala za kidhalimu, na mapinduzi mengi ya Alawiyyin na wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) yalianza kwa kufanya upya kiapo cha utii kandokando ya kaburi hilo tukufu. Kwa mujibu wake, Mapinduzi ya Ashuraa yaliandaa mazingira ya harakati ya Zayd bin Ali, harakati ambayo hatimaye ilichangia kuanguka kwa utawala wa Banu Umayyah.
Ayatullah Mousawi, akizungumzia nyanja za kisiasa za nembo hii ya kidini, alisema: Ukweli huu ulidhihirika nchini Iraq, hususan wakati wa Intifadha ya mwaka 1977, pale utawala wa Baath ukiongozwa na Ahmad Hassan Al-Bakr pamoja na naibu wake Saddam Hussein ulipopiga marufuku Ziara ya Arubaini. Hata hivyo, wananchi wa Najaf Ashraf na maelfu ya mazuwaru waliinuka dhidi ya uamuzi huo kwa mapinduzi makubwa, ambayo utawala wa Baath uliyakabili kwa ukandamizaji, mauaji na kukamata idadi kubwa ya mazuwaru.
Aliendelea kusema: Baada ya kuanguka kwa utawala wa Baath mwaka 2003 (1381 H.Sh.), maandamano ya mamilioni ya watu ya Arubaini yalidhihirisha pia nafasi yake ya kitaifa. Maandamano hayo yalifanyika sambamba na mijadala kuhusu kuandikwa Katiba ya Iraq. Wakati serikali ya uvamizi ya Marekani ilisisitiza kuwa; Katiba iandikwe na kamati iliyoteuliwa, Marjaiyyah ya Juu ya Kidini chini ya uongozi wa Ayatullah Mkuu Sayyid Ali Sistani, ilisisitiza kuwa Katiba iandikwe na wananchi wa Iraq kisha ipigiwe kura ya maoni na umma.
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliongeza: Paul Bremer, aliyekuwa mtawala wa kiraia wa Marekani nchini Iraq, amekiri katika kumbukumbu zake kwamba aliposhuhudia mamilioni ya watu wakielekea Karbala, alifikia hitimisho kwamba kupuuza matakwa ya Marjaiyyah na wananchi wa Iraq kungeweza kusababisha mlipuko mkubwa wa kijamii. Jambo hilo ndilo lililoilazimisha Marekani kurudi nyuma na kukubali kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu Katiba.
Alisema: Huenda Wairaq wengi wasitambue kiwango cha athari za kimataifa za matembezi ya Arubaini, lakini ulimwengu unayaona kuwa ni tangazo la vitendo la uaminifu kwa Imam Hussein (as), ishara ya kupinga uvamizi, udikteta na dhulma, pamoja na alama ya umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.
Ayatullah Mousawi aliendelea kwa kuashiria mazishi ya mamilioni ya watu ya Imam Shahidi Sayyid Ali Husseini Khamenei (qs), akisema kuwa yalikuwa ishara ya kina cha uelewa wa umma na mshikamano wa mataifa katika kushikamana na malengo ya Umma wa Kiislamu. Alisema: Mataifa leo yana utayari mkubwa zaidi wa kutetea dini na matukufu yao, kama yalivyothibitisha katika kuitetea Iraq dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh, kabla na baada ya kutolewa kwa fatwa ya Jihadi ya Kifaya.
Alisisitiza: Jamii ya Iraq ya leo ina tofauti kubwa na jamii ya zama za Imam Hasan na Imam Hussein (as), kwani ina roho ya mapambano na utayari wa kujitolea. Kaulimbiu maarufu ya mazuwari katika Intifadha ya mwaka 1977 (1355 H.Sh.) iliyosema: "Hata kama mikono na miguu yetu itakatwa, tutakuja kwako kwa kutambaa kifudifudi, ewe Hussein."
ni ushahidi wa ukweli huu, kwa hiyo, uchambuzi wa juu juu kuhusu matembezi ya Arubaini hauwezi kufafanua vipimo vya kiitikadi, kijamii na kisiasa vya harakati hii kubwa.
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad, akizungumzia kuongezeka kwa idadi ya mazuwari kutoka mataifa mbalimbali katika Arubaini, alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya mazuwari baada ya Iraq, ambapo kila mwaka mamilioni ya Wairani hushiriki katika ibada hiyo. Kwa mujibu wake, jambo hili limekuwa chanzo cha wasiwasi kwa Marekani na kuisukuma kufanya juhudi za kuzuia ushiriki huo mkubwa.
Pia akirejelea shambulio lililofanywa dhidi ya mazuwari wa Arubaini katika eneo la Shalamcheh, alisema: Shalamcheh ni kivuko cha mpaka kinachotumiwa mahsusi na mazuwari, na hakuna kituo chochote cha kijeshi katika eneo hilo. Kwa hiyo, kulengwa kwa mazuwari kulikuwa kitendo cha makusudi dhidi ya nembo za Husseini.
Ayatullah Mousawi alisisitiza: Marekani inaziona nembo za Kishia kuwa chanzo cha mwamko wa umma, kudai uadilifu na kupambana na dhulma. Hata hivyo, mradi wa Imam Hussein (as) si mradi wa kisiasa unaohusishwa na mkondo maalumu wa kisiasa, bali ni mpango wa Mwenyezi Mungu unaoendelea katika njia ya uongozi wa Imam Hussein (as) na Hadhrat Waliyul-'Asr (aj), na ndiyo sababu juhudi zote za kuuzuia au kuudhibiti zimeambulia kushindwa.
Maoni yako