Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf, katika hotuba za Swala ya Ijumaa za tarehe 5 Tir 1405 H.Sh., zilizosadifiana na tarehe 10 Muharram 1448 H (11 Muharram nchini Iran), alifafanua vipengele vya kiitikadi, kisiasa na kikanda vya harakati ya Ashura, na kusisitiza nafasi kuu ya mapinduzi ya Imam Hussein (as) katika kujenga utambulisho wa kidini, kisiasa na kijamii wa wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (as).
Akieleza kwamba tukio la Ashura halikuwa tukio la kihistoria tu, bali ndio msingi wa kuundwa kwa uwepo wa kiitikadi, kisiasa na kitamaduni wa Mashia katika historia yote, alisema: Wafuasi wa madhehebu ya Hussein daima wamekuwa wakikabiliwa na aina mbalimbali za mashinikizo, dhuluma na juhudi za kufutwa katika jamii, na hali hiyo ndiyo iliyozuia kutimia kwa mfumo wa utawala wa haki ambao Amirul-Muuminin Imam Ali (as) aliweka msingi wake.
Ayatullah Mousawi aliongeza: Kujitahidi kusimamisha uadilifu wa Mwenyezi Mungu na kuasisi serikali inayojengwa juu ya misingi ya maadili ya Kiislamu si uchaguzi wa kisiasa pekee, bali ni wajibu wa kisheria kwa Umma wa Kiislamu na viongozi wake, kwa sababu hiyo, juhudi za mageuzi, kujituma kwa kuendelea, na mapambano ya kisiasa yenye ufahamu na busara kwa ajili ya kulinda maslahi ya Umma na kuhifadhi Uislamu lazima yaendelee.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad, akizungumzia hali ya ndani ya Iraq, alisisitiza umuhimu wa kuzuia kurejea kwa udikteta na ukiritimba wa madaraka kwa jina lolote lile. Alisema: Dhabihu na kujitolea kwa wananchi wa Iraq katika miongo iliyopita havitaruhusu udikteta kuzalishwa tena, wala maslahi ya vyama au ya watu binafsi kupewa kipaumbele kuliko maslahi ya jumla ya nchi.
Ayatullah Mousawi pia alikosoa kuendelea kwa ufisadi wa kifedha na kiutawala katika taasisi za serikali na kusema: Kufichuliwa mara kwa mara kwa mafaili makubwa ya ufisadi kumeongeza zaidi ulazima wa kuchukuliwa hatua za kisheria na kuwafikisha mahakamani watu wote waliohusika katika mafaili hayo, bila kujali nafasi au madaraka yao.
Aidha, akizungumzia suala la uchumi na mafuta nchini Iraq, alionyesha wasiwasi wake kuhusu baadhi ya mikataba ya mafuta iliyofungwa na kampuni za kigeni na kusema: Baadhi ya makubaliano hayo hayalindi maslahi ya taifa la Iraq, hivyo ni lazima yaangaliwe tena kwa lengo la kulinda haki za wananchi na rasilimali za taifa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba zake, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alizungumzia maendeleo ya kikanda pamoja na uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani, akisema: Maelewano ya hivi karibuni katika eneo yanaashiria mabadiliko muhimu ya kimkakati, na mizani ya nguvu katika eneo hilo inabadilika kwa kasi; mabadiliko ambayo athari zake za moja kwa moja zitaonekana katika mustakabali wa eneo.
Pia, akirejelea maendeleo ya Lebanon, aliwapongeza wanamapambano wa Muqawama kwa kusimama imara na kuendelea kuonesha upinzani mbele ya mashinikizo ya kikanda na kimataifa.
Mwishoni mwa hotuba zake, Ayatullah Mousawi, akielezea vipengele vya kiroho vya Ashura na uhusiano wake na utamaduni wa kusubiri kudhihiri kwa Imam Mahdi (as), aliwahimiza waumini kuwa na matumaini, kujitahidi, kujiandaa kuisaidia haki na kusimamisha uadilifu. Aidha, alimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azilinde nchi za Kiislamu dhidi ya fitina na vita, na ayajaalie mataifa ya eneo hilo usalama, uthabiti na utulivu.
Mwishoni, aliwaombea rehema na maghfira waumini wote wa kiume na wa kike pamoja na mashahidi wa Umma wa Kiislamu, na akamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aijaalie Iraq na nchi nyingine za Kiislamu heshima, usalama, kheri na mafanikio.
Maoni yako